Ndugu Rais nimesema mara zote, ‘nchi yangu kwanza’. Hii ndiyo imani yangu ya jana, leo na siku zote. Nitaililia nchi yangu kwa nguvu zangu zote na kuwalilia maskini wa nchi hii bila kuchoka, ndiyo, nitajililia na mimi mwenyewe mpaka  siku zangu zitakapokoma.

Siku pumzi yangu ya mwisho itakapoutoka mwili wangu!

 

Nimepewa sauti inayosikika na wengi si kwa sababu yangu, bali niwasemee waja wake, wanyonge na maskini wasiokuwa na sauti! Hii siyo kwa bahati mbaya, bali ni kwa makusudi yake Muumba wetu.

Kama kuna mtu aliwahi kutuambia Watanzania kuwa kuna watu huko nje wanatuonea wivu kwa mambo makubwa tunayoyafanya humu nchini mwetu, huyo hakutuambia ukweli.

Au haendi nje kuona hali halisi au ana lake jambo kama wasemavyo Waswahili. Hizi ni fikra za anayefikiri akiwa ndani ya sanduku. Tutoke nje ya sanduku tuione dunia ili siku ya kuadhibiwa kwetu tusiwe na mtu wa kumlaumu, bali tujilaumu sisi wenyewe kwa kiburi chetu.

 

Kwetu tunaofanya kazi zetu binafsi hizi za kupuyanga huwa hatuna likizo. Si hivyo tu, hatuna sikukuu, hatuna Jumapili wala hatuna mapumziko ya kuumwa – wenyewe wanaita ‘ED’. Siku zote ni siku za kazi kwa kwenda mbele. Wanasema mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe! Hilo tunalitekeleza kwa vitendo sisi maskini wa nchi hii kwa kutarajia kuwa iko siku Muumba atatuona na atajibu maombi yetu tuliyomlilia kwa muda mrefu sasa.

Zamani wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ile ya nchi tatu, Nairobi tulikuwa tunaiita, ‘South London’ yaani ni sehemu ya kusini tu ya jiji la London. Sijui baba kama unajua kuwa hata huku kwetu siku hizi hakuitwi Mbagala. Kunaitwa, ‘Dar es Salaam South’. Baba ulilijua hili? Tofauti kubwa iliyokuwapo kati ya Nairobi na Dar es Salaam au tuseme kati ya Kenya na Tanzania ilikuwa ni maendeleo. Kenya walikuwa mbali kwa maendeleo ya vitu. Lakini Tanzania ilikuwa mbali sana kwa maendeleo ya watu hasa kwa kuujali utu wa wananchi wake. Watu kutekwa, kuteswa, kupotea na kuuawa Kenya zilikuwa ni hadithi za kawaida.

Hadithi ambazo kwa Tanzania ya Nyerere zilikuwa ni za kufikirika tu.

 

Tuliposikia habari za kuuawa kwa Tom Mboya, Joshua Mwangi Kariuki, Robert Ouko na wengine Watanzania tuliwaita Wakenya majina ya aibu kama vile, manyang’au. Ni uchungu mkubwa kwa kiasi gani, Mtanzania wa leo unapofika Nairobi na kuwaona Wakenya walewale tuliokuwa tunawaita manyang’au wakikulaani kwa unyanga’u wanaouona ukifanyika nchini kwetu? Wakenya sasa wanaitana ndugu. Ukiwa Nairobi huzioni tena zile tofauti kubwa za kikabila walizokuwa nazo. Viongozi walioko madarakani na viongozi wa upinzani wote sasa ni kitu kimoja. Wanashirikiana kuijenga Kenya moja. Huzioni kabisa tofauti zao za kisiasa kama tulivyozoea. Wamekuwa wote ni ndugu. Wanakwenda kulekule tulikotoka. Sisi tunaenda walikotoka wao. Ni mikosi gani hii tulizaliwa nayo?

 

Maumivu yangu yalikuwa makali zaidi kuona Wakenya wananiona mimi kama mtu niliyetoka kwenye nchi katili ajabu. Nikajiuliza, ni kwanini waione nchi yangu kama nchi inayowajaza wananchi wake mateso na hofu zisizokwisha? Hawa hawa siku chache tu zilizopita walikuwa wanaiona Tanzania kama kisiwa cha amani. Ni nani waliokuja kuiharibu sifa nzuri ya nchi yetu machoni pa Wakenya? Wananiuliza, mnatekwa, mnateswa, mnashambuliwa kwa risasi za moto hadi mnauawa, mlinzi wenu ni nani?

Mlinzi mkuu katika nyumba yoyote ni baba. Jukumu kubwa na la kwanza la serikali ya watu ni kulinda maisha ya wananchi wake. Lakini kama serikali yenyewe na kwa kupitia vyombo vyake imekiri hadharani kuwa watu wanaowateka raia wake na kuwatesa na kuwaua imeshindwa siyo kuwatia nguvuni tu, bali hata kuwajua tu imeshindwa; ni kitu gani kinachobaki kinachoipa serikali hiyo uhalali na sababu za kuendelea kuwapo? Watakapotokea wa kutokea wakasema serikali hiyo kwa kukiri hivyo itakuwa imejitangazia yenyewe kuwa ni serikali isiyo halali, watakuwa wamekosea wapi? Serikali ya watu inawekwa na watu kwa ajili ya watu.

Alisema Obama kuwa serikali zote za kiimla hapa duniani huishi kwa kutegemea hofu na nguvu za dola.

 

Nitasema bila kusita kuwa, viongozi wetu mlio madarakani serikalini, viongozi wetu katika Chama Cha Mapinduzi na viongozi wetu wa vyama vya upinzani wote katika ujumla wenu kwa kuulea uhasama wa kisiasa nchini

mwetu, hamko sahihi hata kidogo. Achaneni na tofauti zenu, acheni kiburi mrudi katika mstari kwa maslahi ya nchi na Watanzania.

Mkishindwa kuirekebisha hali hii mjue mnamkosea Mungu mwenyewe, mnawakosea Watanzania na mnaikosea nchi yetu. Na kwa kuwa hakuna makali yasiyokuwa na ncha kwa hili mjue kuwa hukumu yake Mwenyezi Mungu hamtaikwepa kwa kuwa anawapenda waja wake!

 

Bado nitaendelea kuamini kuwa katika hii miaka yetu michache kuna mahali tumekosea. Tumeikusanya hasira ya Mwenyezi Mungu dhidi yetu kwa kushindwa kuzuia machungu, maumivu na magumu ya waja wake; jukumu ambalo lingekuwa ndiyo uthibitisho pekee kuwa tunazo baraka zake Mungu kwa kushika nafasi tulizonazo hivi sasa.

Ninachosema hapo ni kwamba wanayoyafanya haya sasa wakumbuke kuwa alikuwapo Abeid Amani Karume, alikuwapo Aboud Jumbe, alikuwapo Rashid Mfaume Kawawa, alikuwapo na Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Lakini leo wako wapi? Wamekwishapita! Na wao wajue watapita! Yuko wapi Idd Amin Dada yule aliyesema anainyosha Uganda? Remmy Ongala alisema, wamekuwa nyama ya udongo.

 

Mwanadamu kumbuka, wewe ni mavumbi. Mavumbini ulitoka, na mavumbini utarudi kwa maana imeandikwa, ulitoka kwa udongo na utarudi kwa udongo. Kwa kuwa hakuna makali yasiyokuwa na ncha tusipokubali kuwa tumetenda tofauti na matakwa ya Muumba wetu, tukatubu, mwisho wetu utakuwa mzito sana. Utajaa majuto, vilio na kusaga meno! Vitu ambavyo havitatusaidia kitu!