Ndugu Rais, dunia tuliikuta na dunia tutaiacha. Niliwahi kusema kuwa kila mtu kila msiba anaohudhuria humkumbusha misiba yake iliyopita.

Kama umefiwa na baba, mama, mtoto au ndugu aliyekugusa wakati wa msiba unakumbuka zaidi! Msiba umetokea na baba nilikuona. Msiba huu ulinikumbusha siku tulipokuwa tunauaga mwili wa Sir George Kahama katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Baba sikukuona siku ile!

Kwa kumbukizi ya Sir George Kahama niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka Tangulia Sir George Kahama umetuachia kitabu chenye hadithi nzuri! Simu niliyopigiwa kunitaarifu kifo cha Sir George Kahama ilisema, “Mwalimu mkuu sasa tumekwisha! Ndio tumekwisha! Waasisi wa uadilifu na uzalendo wa kweli katika nchi hii sasa wanamalizika!”

Tumebaki kuona unyama, uhuni na kusikia maneno ya kipuuzi yanayotutaka sisi watoto wa baba mmoja tusishirikiane, tusipendane ikibidi tuchukiane, tutekane na kutesana kinyume kabisa na tulivyolelewa katika upendo, umoja na mshikamano na Sir George Kahama na mshirika wake mkuu Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.”

Tuwaache Sir George Kahama na Mwalimu Nyerere, wapumzike kwa amani! Kazi waliotumwa na Mwenyezi Mungu ya kuwaletea wana wa nchi hii amani, upendo na mshikamano wameitimilisha! Wamepigana vita iliyo njema na mwendo wameumaliza. Na sasa wanangojea tuzo kutoka kwa Muumba wao!

Watakumbukwa na vizazi vingi vijavyo na majina yao yameandikwa katika vibao vya mioyo ya masikini na wanyonge wa nchi hii! Waliokuwa wanalia wote wanaomboleza kwa uchungu wa kweli wakionesha kuwa Taifa limempoteza mtu muhimu!

Ndugu Rais, kilichonigusa katika msiba huu wa majuzi ni mkusanyiko mkubwa wa watu wengi. Ukiacha wanafamilia wengi hawakuwa waombolezaji. Unafiki tu uliwapeleka pale.

Wakati jeneza likiteremshwa chini katika kaburi lililochimbwa udongoni viongozi wetu wakuu wote wa sasa na wastaafu, walisimama kushuhudia mwana wa Adamu akirudishwa katika mavumbi kwa maana huko ndiko alikotoka!

Ewe mwanadamu, kumbuka ulitoka kwa udongo utarudi kwa udongo. Haijalishi jeneza lako litakuwa la thamani kiasi gani lakini litafukiwa chini. Sikumbuki katika viongozi wote wale niliowaona kama kuna hata mmoja ambaye jeneza kutelemshwa chini kulimkumbusha siku yake ya kufa. Mara nyingi mwanadamu anapofikiria kifo hufikiria kifo cha watu wengine.

Zamani Wakristu wakati wa maziko tuliimba, “Ewe mtembezi simama na tazama. Nimekufa leo, kesho ni yako zamu…”

Akitoa nasaha zake katika kuuaga mwili wa Sir George Kahama mzee Ali Hassani Mwinyi alisema, “Sisi wote hapa duniani ni mali ya mwenyewe, Mwenyezi Mungu. Tukishapita nyuma yetu zinabaki habari zetu tu mithili ya kitabu. Sir George Kahama ameacha kitabu chenye habari nzuri.

Tujitahidi na sisi ili siku tutakapoitwa nyuma yetu tuache kitabu chenye habari nzuri!”

Alisema hivi tunavyoishi na yote tuyatendayo sasa tunakuwa kama kitabu kinachoandikwa. Kitakamilika na kuanza kusomwa mara tu baada ya kifo chetu. Baba, tunajiandaa kuacha kitabu chenye habari gani?

Katika misiba mingi wanafiki husema mengi ya kumpendezesha marehemu. Lakini wenye haki husema yote mema na mabaya ya marehemu. Katika msiba huu wanafiki walikuwa wengi kuliko waombolezaji. Wakasema marehemu hakuwahi kuyumba, alikuwa na msimamo na aliyasimamia yote aliyoyaamini.

Leo unaisimamia itikadi yako unayoiamini katika chama chako na kesho unabadilisha chama na kuisimamia itikadi tofauti na ile ulioisimamia mwanzo, huko siyo kuyumba?

Zaidi ya nusu ya maisha yako umewatangazia wanadamu kuwa hakuna Mungu na ukaishi bila kufungamana na dini yoyote. Lakini ulipokiona kifo kinakujia ukakiri kuwa wewe ni Mkatoliki. Huku siyo kuyumba? Bado wanafiki wanasema aliyasimamia aliyoyaamini. Ni yapi hayo? Kuwa hakuna Mungu au kwa kuukiri ukatoliki wake?

Kiongozi bila aibu anasema vijana wetu wanatakiwa waige maisha ya mtu huyu ya kutangatanga kifikra. Kama ni kitabu alichosema mzee Mwinyi huyu ameacha kitabu chenye hadithi za kuhuzunisha zitakazomsikitisha kila atakayekisoma. Vijana wetu hawapaswi kukisoma kitabu chake. Kimetuachia habari mbaya.

Ndugu Rais, wako wengi waliotangulia ambao sasa tunasoma vitabu vyao. Ni msomaji gani atakosa kulaani akishasoma kitabu cha Samwel Sita na katiba mpya? Na sisi na utawala wetu hivi sasa tunaandika kitabu.

Tujiulize tunadhani ni sura zipi zitagusa mioyo ya wasomaji wetu? Ni kweli ukishakufa hata watu wote waliobaki wakikulaani hakuna mwenye ushahidi kuonesha kuwa laana yao itakupata, lakini je huku nyuma hatutaacha wanaotuhusu?

Watoto kwa mfano kila wanapopita wanakutana na jamii inayomlaani baba au mama yao. Huku wanasikia, ‘bila baba au mama yake huyu baba yangu au mama yangu asingepotelea kusikojulikana.

Na kule wanasikia, ‘bila baba au mama yake huyu baba au mama yangu asingeshambuliwa na kuachwa na kilema cha maisha. Tutawaacha watoto wetu katika jamii ya visasi?

Ndugu Rais, somo la ‘flowmeter’ zilizoshindikana litaeleweka kwa wasomaji wetu? Leo ni mwaka wa tatu tuko na mamlaka lakini hatujui nchi inaingiza mafuta kwa hakika ya kiasi gani. Kumbuka safari zako za kushtukiza kule bandarini zilivyowatia imani kubwa wananchi wakijua wamempata mkombozi. Ulipotoka wewe alienda Waziri Mkuu wetu. Na kila mlipoenda kutatua tatizo moja mlirudi na tatizo jingine. Wakati mwingine kubwa kuliko mliloendea. Lakini flowmeter zimebaki zimeshindikana!

Tunawapa nafasi ya kuaminiwa na wananchi wale wanaowaambia kuwa tunachofanya ni kupuyanga tu. Somo la ‘Bombadier’ peke yake limeandikwa mara tatu. Moja inasema zinakuja nyingine mpya mbili mwezi Julai. Nyingine inasema Shirika letu la ndege pamoja na Bombadier mpya, linajiendesha kwa hasara.

Na ile Bombadier iliyochafua hali ya hewa na kutishia kuondoka na mtu kwa kudai au kwa kudaiwa, hatima yake eti ameachiwa Mwenyezi Mungu mwenyewe aamue.

Ndugu Rais, vipo vitabu vya akina Idi Amin, Adolf Hitler na wengine. Lakini vipo pia vitabu vya akina Mandela, Nyerere na wengine. Kitabu chetu tunataka kije kiwekwe kwenye shelfu ipi? Baba, moyo wa mtu ndiyo injini ya mtu. Bila Azimio la Arusha, tutapuyanga sana. Tusingoje kuambulia vumbi ndipo tupate fahamu kuwa dunia hadaa, ulimwengu shujaa!

 

PASCHALLY MAYEGA

SIMU:    0713 334239