Ndugu Rais, dunia imeshuhudua aliyemua Daudi Mwangosi kikatili akifungwa gerezani kwa miaka 15! Daudi Mwangosi hakuwa anaandamana! Alikuwa anatafuta habari! Kwa polisi wetu lile lilikuwa kosa kubwa ambalo lilimgharimu uhai wake!
Kabla ya kuuawa Daudi Mwangosi alipigwa kinyama, alipigwa kijambazi, alipigwa kishenzi! Alikosa nini? Mpaka leo haijaelezwa alikosa nini. Labda ni kwa sababu hakuna kosa alilotenda!
Kundi la maaskari lilimzingira na kila askari alijitahidi kumpiga Daudi Mwangosi kwa nguvu zake zote! Wengine kwa virungu wengine mateke na ngumi, wengine kwa unyama wao! Walimpiga kila sehemu ya mwili wake! Kosa lake, kutafuta habari! Ah! Unyama gani huu jamani!
Ndugu Rais tuambie, ni nani mwenye ushahidi kuwa Daudi Mwangosi hakuuawa kwa kipigo? Kwamba alikufa hata kabla ya kulipuliwa na bomu? Lakini leo hii muuaji amekuwa ni askari mmoja tu, peke yake.
Alishitakiwa peke yake, akahukumiwa peke yake na sasa amefungwa peke yake. Katika kundi zima lile hakuna aliyeshirikishwa katika kesi hii! Kamanda aliyesimamia unyama ule alipandishwa cheo. Baba, kwa hili, ni kweli dunia hii ni hadaa, lakini ulimwengu ni shujaa. Lazima ipo siku ulimwengu utatuhukumu!
Unyama huu na mwenendo mzima mpaka hukumu ilivyotolewa uwafanye polisi wetu wajitafakari pale wanapotekeleza amri za wakubwa wao. Hukumu ya binadamu imetolewa, lakini kwa Mwenyezi Mungu ataenda kuianza upya. Mbele ya Muumba wetu kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe! Kwa Mungu hakuna ‘afande alinituma.’
Ni vema wengine wakajifunza kwa yaliyompata mwenzao. Wakati huu tuna polisi wa aina nyingi. Tuna polisi panya, tuna polisi mbwa, tuna polisi farasi, tuna polisi matuta yale yaliyolala barabarani na tuna polisi wanadamu. Wakati wa kujitofautisha mnapotekeleza amri ni sasa.
Kama aliyeua angekuwa ni polisi mbwa nani angemshitaki? Hukumu ile imehitimisha safari ndefu ya miaka minne ya vitimbwi vya polisi ikiwa ni pamoja na kumkinga asipigwe picha kwa kumfunika shuka, kumsindikiza na gari la polisi badala ya gari la magereza kama watuhumiwa wenzake na vituko vingine vingi vilivyoashiria mazingira ya kutaka haki isitendeke.
Akisoma hukumu yake, Jaji wa Mahakama Kuu, Paul Kihwelo alisema: “Katika kuangalia ni adhabu gani inafaa kwa mtuhumiwa, Mahakama ilijielekeza katika mambo kadhaa ambayo ni ukubwa wa kosa analoshtakiwa, mazingira ya utendaji kosa, maslahi ya mtu na maslahi ya jamii kwa ujumla.
“Mgongano wa hisia umeonekana katika kesi hii ila Mahakama inampa adhabu ya kwenda jela miaka 15.”
Hukumu hii imepokewa kwa mitizamo mbalimbali. Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu kupitia wakili Benedict Ishabakaki amesema hukumu hiyo ya Mahakama Kuu imetenda haki bila kuegemea upande fulani licha ya nguvu kubwa ya polisi na jinsi ambavyo ushahidi uliokuwa umepelekwa kulenga kumnasua mtuhumiwa. Nguvu kubwa iliyotumika siku zote wakati wa kesi hiyo ni kielelezo tosha kuwa polisi walikuwa wakitarajia mwenzao angeachiwa huru.
Mdogo wa marehemu, Andrew Mwangosi amesema: “Hukumu hii haimaanishi kuwa sisi wanafamilia tumefurahi, hata angefungwa maisha asingemrudisha marehemu. Kesi ya msingi imeisha, tunaishukuru Mahakama ukweli umejulikana na dunia imejua kuwa kifo cha ndugu yetu ni cha aibu na dunia imeona.”
Naye, Rais wa Shirikisho la Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UPTC), Deo Nsokolo alisema: “Tunashukuru Mahakama kwa kutoa haki, sasa dunia imeona kuwa Jeshi la Polisi liliua mwanahabari. Rekodi ya dunia ni kuwa Jeshi la Polisi hapa nchini lilimuua mwanahabari.”
Ndugu Rais, matukio ya polisi kuua raia katika nchi yetu ni mengi. Na utaratibu uliopo kuwa mtuhumiwa anapokuwa polisi eti akamatwe na polisi na kuchunguzwa achunguzwe na polisi kupata ushahidi, unaacha shaka nyingi kwa haki kutendeka.
Matukio kama haya halafu hakuna hatua zinazochukuliwa yataachwa yaendelee mpaka lini? Au mpaka polisi watakapomuua nani ndipo hatua zichukuliwe? Hawa wanaouawa sasa watakaposema sasa basi liwalo na liwe, wakaamua kujitetea ni nani atakuwa ndiye chanzo cha machafuko? Amani ya kweli hailindwi kwa mtutu wa bunduki. Elewa ndugu Rais kuwa nguvu za majeshi ya serikali ndiyo upanga wa mtawala. Kwa mtawala yeyote anayemtanguliza Mungu mbele yampasa ayazingatie maneno ya Bwana Yesu pale aliposema: “Atawalaye kwa upanga, atakufa kwa upanga!”
Kutawala watu wa Mungu kwa kutumia polisi ni kuwatawala kwa upanga. Atakufa kwa upanga. Nchi lazima iongozwe kwa sheria. Huwezi kuzuia haki za raia kwa kutumia hisia zako.
Wakati wake Augustino Mrema, kila alipobebwa waliombeba walipigwa mabomu. Huja wa kufa wangekufa kama Baba wa Taifa asingekuwapo wakati ule. Akitumia busara Mwalimu Nyerere alisema: “Kwa kuwa wanaotaka kumbeba Mrema wapo, waacheni wambebe. Wambebe hata kama watakuwa wanapokezana kama machela (jeneza), waacheni.” Polisi walipotii agizo la Baba wa Taifa, la kuacha kuwapiga mabomu, Mrema naye kama shani hakubebwa tena.
Ndugu Rais, Baba wa Taifa leo hatunaye! Lakini tupo sisi mawe, tusikilize! Sheria za nchi zipo. Polisi wanaopaswa kuchunga sheria za nchi wapo. Kuruhusu au kuzuia mikutano au maandamano si kazi ya polisi. Kazi ya polisi ni kuwakamata wote watakaotumia maandamano au mikutano kuvunja sheria na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Kamwe siyo kuwapiga na hata kuwaua!
Chadema kufanya maandamano na mikutano Septemba Mosi kunahitajika busara kubwa kutoka pande zote mbili. Chadema wafute mawazo maovu ya kusema wanaenda kupambana. Nani hakuona ule umati mkubwa wa kihistoria uliojitokeza kuandamana kumsindikiza Ndugu Edward Lowassa kurudisha fomu? Aliumia nani? Kilivunjika nini?
Upande mwingine ujiulize,kamaKatiba ya nchi na sheria za nchi zinawapa haki ya kufanya hivyo atakayewazuia ajue anavunja Katiba kunyang’anya haki za raia!
Kama tunatosha hakuna sababu ya kuuogopa upinzani.
Wanahabari jitokezeni kutafuta habari. Dada Itika, mjane wa Daudi Mwangosi amewaambia: “Msiogope! Msivunjike moyo mkarudi nyuma! Endeleeni kufichua maovu yote yanayotendwa katika jamii!”