Ndugu Rais, wanao tumekuona umelala juu ya jiwe. Umetukumbusha Yakobo yule aliyeimbwa na wanakwaya mahiri wa Mamajusi wa Majengo, Moshi.  

Yakobo alikuwa anasafiri kutoka Delisheba akielekea Almara. Njiani alichoka sana, akaamua kulala kwenye jiwe. Tunaambiwa malaika wa Mwenyezi Mungu walikuwa wanamlinda Yakobo usiku kucha. Na wewe baba tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu malaika wake wakulinde!

Jiwe limetajwa mara kadhaa katika Biblia Takatifu. Lakini hata huku uswahilini jiwe au mawe yanatumika kuleta maana tofautitofauti. Ukisikia fulani siku hizi yuko juu ya mawe, jua huyo jamaa kama ni kiuchumi amekwisha kabisa! Mambo kwake yamemwia magumu.

Kulala juu ya jiwe pia kumetajwa katika maandiko. Akiwa bustanini Getsemane, hata alipojua kuwa saa yake imefika, aliwaambia wanafunzi wake: “Kaeni hapa mkisubiri.’’ Akaenda mbele kiasi cha umbali wa kutupa jiwe akalala juu ya jiwe akiomba. Juu ya jiwe hilo, lilimtoka jasho la damu. Kila nikitafakari mambo makuu ya Mungu aliyonitendea ninabaki kutahayari. Nilipojaliwa kuingia katika Bustani ya Getsemane nilikwenda nikalala juu ya jiwe hilo alilolalia Yesu Kristu! Jina la Bwana lihimidiwe! 

Aliyekupiga picha alikosa ujasiri akaficha jina lake. Ameandika kwa herufi kubwa za njano kuwa: ‘Magufuli kwenye tafakari’. Halafu chini yake akaandika: ‘Rais akiwa amejipumzisha juu ya jiwe’. Kutafakari ni kufanya kazi. Kujipumzisha ni kukaa bila kazi. Ikikupendeza baba tuambie mwenyewe juu ya jiwe ulikuwa unajipumzisha au ulikuwa unatafakari?

Nchi yetu hivi sasa imezingirwa na magumu mengi sana ambayo yanahitaji tafakuri sahihi. Mengine tumeyasababisha wenyewe kwa kujifanya tuna shingo ngumu. Waumini wanaoamini katika dini zao wanasema hata ugonjwa huu ni matokeo ya dhambi za wanadamu. 

Sisi wenye kuamini lakini tunachanganya na zetu, tunaamini kuwa Mungu ni mwema. Kwa mapenzi aliyonayo Muumba wetu kwetu, kamwe hatuwezi kumwomba mkate halafu akatupa nyoka. Corona haiwezi kutoka kwa Mungu, lakini haya inayotufanyia Mungu ana makusudi yake. 

Si bahati mbaya, ila sasa Watanzania ugonjwa huu utufundishe kulegeza shingo zetu. Watanzania tumelia sana, na kwa muda mrefu kuwa jamani Mwenge wa Uhuru umepoteza sababu za kuwepo kwake, uzimwe, hatukusikilizwa. Lakini kwa ugonjwa huu watu wameuzima Mwenge bila kutaka. 

Zilipoanza kununuliwa ndege kwa mkupuo, tena kwa fedha taslimu, wazee wastaafu wa TTCL tunaolipwa pensheni ya Sh elfu 50 kwa mwezi mpaka sasa tuliwalilia viongozi wetu kuomba angalau ndege moja icheleweshwe ili kwa pesa hizo tuhudumiwe angalau kwa kulipwa hiyo nyongeza ya Sh elfu 50 iliyokwisha idhinishwa na Bunge. Lakini kwa unyonge wetu hatukusikilizwa! 

Tunawahakikishia watesi wetu kuwa wasituone sasa tunapita kwenye moto kwa kuzuia malipo haya, wajue tumelala kwenye jiwe tu, kesho tutasonga mbele! Hatuombi cha mtu! Tunaomba sehemu ya jasho letu tulilolitoa kwa nchi yetu kabla wao hawa watesi wetu hawajawa! Tumepukutika sana na sasa tumebaki wachache. Kama kilio hiki baba hakitasikika kwenu viongozi wetu wa hapa duniani, tutakwenda kulia mbele ya Mwenyezi Mungu mwenyewe, mbinguni! 

Wanawema, IATA inakadiria kuwa kutokana na corona sekta ya usafiri wa anga itapoteza mapato yenye thamani ya dola zaidi ya bilioni 110 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh trilioni 250. Wakati haya yakijiri, ATCL imetangaza kufuta safari zake zote za kimataifa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona.  Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, ameeleza kuwa nchi nyingi zimefunga anga zake. 

Kwa kukosa ufahamu hatukujua kuwa matajiri wanaoweza hata kutalii tu, hawapandi ndege yoyote na hasa wasiyoijua. Kwa upofu wetu tulidhani ndege zetu zingeenda kukusanya watalii duniani. Tuzingatie maelekezo tunayopewa na viongozi wetu namna ya kujikinga na ugonjwa huu hatari. Umetusaidia kuuzima Mwenge na sasa umetusaidia kuelewa kuwa biashara ya ndege, ni biashara kichaa na hasara kwa nchi! 

Tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu ujao tutambue kuwa kushabikia vyama vya siasa au watu fulani kwa pamoja tuone kuwa ni ujinga. Nchi yetu kwanza! Amani ya nchi yetu ndiyo kiwe kipaumbele chetu wote. Nani tumchague awe rais wetu ajaye? Baba wa Taifa alituachia wosia. Alisema: “Tuchagulieni mgombea atakayekidhi matarajio ya Watanzania.” Alisema Watanzania wanataka uhuru wao wa kutembea na kutoa mawazo yao katika jumuiya zao. Wanataka mgombea atakayewaboreshea wananchi maisha yao katika afya na elimu. Ndugu wa kuwaongoza, kama ndugu Julius Nyerere alivyowaongoza kwa mapenzi makubwa. 

Mheshimiwa wa kutaka kututawala wote tumkatae! Atakayetaka kuitawala nchi kwa mawazo yake mwenyewe, hatufai hata kama nia yake ni kutaka kutushushia mbalamwezi ili tuuguse.

Baba kumbuka, ukiwa waziri na mbunge ulishiriki kupitisha azimio kutaka wazee wastaafu wa TTCL waliokuwa wanalipwa pensheni ya Sh 50,000 kwa mwezi nao waongezewe Sh 50,000 ili nao kima cha chini kiwe laki moja kama wastaafu wengine. 

Tumemaliza miaka mitano bila kuwafanyia ahueni yoyote! Tumekidhi matarajio ya Watanzania kama alivyotuwosia Baba wa Taifa? Hawa sasa wana watoto wenye familia kubwa na jamaa wengi. Wana wajukuu wenye familia kubwa na jamaa wengi. Kwa hili tunajikana wenyewe kwa watu wetu katika Uchaguzi Mkuu ujao!

Itasikika sauti: “Si nyinyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua nyinyi kwa ajili ya waja wangu. Kwa nini mligeuka na kuwa watesi wa waja wangu? Mnaona nilikosea kutowaunganisha wazazi wenu na hawa wastaafu? Kwa nini hamkuwalipa stahili yao kwa kadiri nilivyoikirimia nchi yenu?” Maswali haya atatuuliza Mungu mwenyewe katika vifua vyetu!

Wastaafu tuwaombee wazazi wa watesi wetu afya njema! Anayoyajutia leo mzee Mkapa, yafungue ufahamu wetu tutambue kuwa kuna maisha hata baada ya urais kukoma. Kwa kelele nyingi na nzito zilizokwisha kupigwa mpaka sasa, baba ni busara malipo ya wazee hawa ukafuatilia mwenyewe ili hili lisije likawa ni sehemu ya kujuta kwako wakati utakapokuwa hauna tena mamlaka. 

Unaweza ukashangaa fedha zilikwisha kutolewa lakini wakubwa wamejisetiri nazo. Baba, mateso tunayopitia sisi wastaafu ni mengi sana, lakini Mungu hututetea kwayo nasi tunasonga mbele!