Ndugu Rais ni kipi ambacho hatujawahi kuandika hapa katika kushauri, kutahadharisha au kuonya? Wanawema wakasema huyu ni nabii wengine wakasema ni mtabiri, lakini tukawaambia ya kwamba hesabu sahihi za mcheza bao hodari majibu yake ni yale yale ya nabii au mtabiri! Mcheza bao hodari anaweza kucheza michezo miwili hata mitatu kabla hajagusa kete yake hata moja. Anachofanya ni kuhesabu tu.
Wahenga waliposema mchimba kaburi huingia mwenyewe walikuwa wanatabiri? Na sisi tuliposema kilichoingia kwa hila kitaondolewa kwa hila ulikuwa ni unabii? Hatukuwaambia kuwa ole wenu nyinyi mnaocheka sasa kwa kuwa siku zenu za kulia zitakuwa chungu zaidi? Kumbe hata Nape anaweza kulia kama masikini na wanyonge wa nchi hii wanavyolia? Ni mwepesi wa kusahau au ni ujinga wa kibinadamu?
Nape Nnauye awaambie Watanzania, ni kipande gani cha ardhi ya nchi hii
ambacho hajawahi kukikanyaga wa mguu wake? Aliizunguka nchi nzima akihubiri fitina na kupandikiza chuki kati ya watu wa Mungu akiwataka wachukiane! Leo mjinga gani atalia na yeye? Walisema mtenda akitendwa huhisi kaonewa! Nape tangulia. Kapumzike kwa amani! Wanakuja wengi nyuma yako!
Ndugu Rais kila kitabu kina ukurasa wa mwisho, Nape anasoma ukurasa wake wa mwisho! Siku za kucheka na kujidai huja na kupita; vivyo hivyo na siku za kulia na kuomboleza! Siku za kucheka usicheke ukapitiliza wala siku za kulia pia usilie ukapitiliza! Nape soma kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu ukurasa wa 60 imeandikwa; “Ala, kumbe! Kila zama na watu wake?” Zama zenu zimekwisha! Kulia na kutapatapa hovyo ndiyo kawaida ya wapiganaji wote wanaopigana vita waliyotumwa na mtu mwovu!
Kwa kuwa wewe ulikuwa hupigani vita ya haki, basi amini usiamini utabaki peke yako! Na aliyekutuma sasa atakaa mbali nawe! Huu ndiyo mwanzo wa mwisho mchungu kwako! Hukujua kuwa siku hazigandi? Siku zinakuja ambazo waliolia kwa muda mrefu watayafuta machozi yao nao walioishi kwa kicheko wataogelea katika huzuni kuu!
Laiti Ikulu ingekuwa na wodi ya wagonjwa sasa ungekuwa na mahali pa kulazwa ukapumzika baada ya kuvuliwa gamba! Lakini ni wewe uliyekuwa unawatangazia Watanzania kuwa Ikulu hakuna wodi ya wagonjwa!
Wanaokusulubu sasa wajifunze kwako kwa maana baada ya nyinyi kuadhibiwa itakuwa zamu yao mpaka hapo nchi itakaporudishwa kwa wananchi!
Ndugu Rais nilipomsikia Nape Nnauye akitumia mdomo ule ule alioutumia kulinyumbulisha neno uchochezi akisema sasa wanahabari ruksa kuikosoa Serikali, nikajua kimemnukia, saa yao ya kuadhibiwa imetimia! Nape Nnauye anapolia sasa hapaswi kulia sasa akumbuke wakati wa furaha!
Aikumbuke furaha aliyokuwanayo wakati ule akizima TV bungeni. Aikumbuke furaha aliyokuwa nayo wakati ule akitetea sheria ya habari ambayo mpaka jana alionesha kuifurahia wakati wenyewe wako mahakamani kutaka marekebisho! Nape akumbuke furaha yake pale alipomfanya Ndugu Rostam Aziz aseme anaachana na siasa uchwara! Sasa zimemtumbukia nyongo! Namwambia atajikuta yuko peke yake!
Ndugu Rais, sasa imedhihirika kuwa Nape alipokuwa anatamba kuwa ushindi utalazimishwa hata kwa goli la mkono alikuwa hajui alichokuwa anakisema. Madhali sasa yamemkuta, awaambie Watanzania kama ushindi wao ulikuwa halali au wa mkono? Unyama aliofanyiwa Godbless Lema leo unamtukuza popote awapo kwa wote walio na hofu ya Mwenyezi Mungu!
Lakini anachofanyiwa Nape Nnauye ni mshahara wa dhambi zake kwa maana malipo ya dhambi sasa ni hapa hapa duniani! Baada ya tukio hili Nape atajikuta yuko peke yake!
Wanaomsulubu Nape sasa kwa kudhani kuwa wameshika kwenye mpini wajue huu ni upepo uvumao. Kuna mahali ulianza na kuna mahali utakoma! Iko siku isiyo na jina nao watakuwa mahali alipo Nape sasa kwa kuwa hakuna makali yasiyokuwa na ncha.
Kuondolewa kwa Nape Nnauye na mikoba yake kurithishwa Harrison Mwakyembe kwa haraka ya ajabu, kunatukumbusha wengine uasi uliosababisha kuanzishwa kwa Chama cha Jamii, CCJ. Kwa wakati huu nafasi ya Samuel Sita katika siasa za nchi hii itaonekana dhahiri kuwa wazi, iwe kwa wema au kwa ubaya! Hawa wawili na wenzao wengine walitambuliwa kama vijana wa Samuel Sita. Sita alikuwa na uwezo wa kuasisi fukuto lililowalazimisha watawala dhaifu kumtii! Tuliona uhuni aliofanya katika sakata la Richmond uliosababisha vita hewa dhidi ya ufisadi, vua gamba na katika mchakato wa katiba mpya! Akitokea mtu akasema Harrison Mwakyembe amewekwa mlangoni tayari kumfuata Nape kutoka wa kupinga atatoa sababu zipi? Hata kumzuia Tundu Lissu tu kuwa Rais wa TLS ameshindwa!
Samuel Sita aliweza kuutisha utawala dhaifu uliokuwapo akaunda tume dhalili ya Bunge huku akimpa uenyekiti Harrison Mwakyembe. Nao bila aibu wala huruma kwa masikini na wanyonge wa nchi hii walichota mamia ya mamilioni ya shilingi wakidai wanakwenda kuizunguka dunia kuutafuta ukweli kuhusu Richmond. Waliporudi Harrison Mwakyembe aliwaambia
Watanzania kuwa ukweli waliupata. Kisha wakawatengenezea ripoti ya kuhalalisha fedha walizochukua! Ndiyo ripoti ilikuwa ni ya uongo mtupu kwa kuwa alisema walificha ukweli nusu na duniani hakuna ukweli nusu.
Niliwaambia laana hii haitawatoka juu ya vichwa vyao mpaka siku zao za mwisho! Huyu aliyekiri kutosema mengine ndiyo leo amekabidhiwa wasanii!
Ndugu Rais, ni nani hakuona wasanii walivyogeuka mtaji au silaha nzito katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015? Ni nani hakuona fedha nyingi zilizotumika kuwaleta pamoja na kuwalipa ili kumfanyia kampeni mgombea wa urais wa CCM ambaye kinadharia alikuwa amekwishajulikana? Bahati mbaya hakuwa! Faida yote hiyo ikamwendea aliyeteuliwa na chama!
Ili kuleta utulivu ikalazimu Nape awe waziri ili alinde hiyo silaha yake (wasanii) kwa matumizi ya baadaye. Nia ya urais ingali, ukimwondolea kamanda wake kitaeleweka? Kumbadilishia na huyo aliyekiri kutoa ripoti ya ‘ukweli nusu’ ya Richmond atamkubali? Orodha ya kwanza ya watuhumiwa wa dawa za kulevya ilikuwa wasanii watupu, Nape alisimama kuitetea silaha ya ‘boss’ huyu ataweza? Wasaliti walioondolewa wamekubali hivyo wameenda makwao kulala? Tukisema aliyoyataka Baba wa Taifa yanakaribia kutimia mtatuita watabiri?