Ndugu Rais, nianze kwa kuwapa pole wanawema wote walioguswa na yaliyosemwa juu ya andiko langu katika mtandao.
Ni kweli sina utaratibu wa kuingia katika mitandao mara kwa mara. Hata hivyo kwa haya yaliyotokea na kwa namna yalivyotokea, yamenifariji sana. Si busara kujimwambafai kwa unayowatendea watu. Waache watu ndio waseme.
Kama unaandikiwa meseji nyingi kutoka kwa watu tofautitofauti zinazosema, ‘tunakuombea! Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu kwa haya unayoandika’, kwanini usifarijike?
Hakuna faraja anayoweza akaipata mtu anapotambua kuwa kuna watu wanamjali, awe nao au asiwe nao. Kwa wote walioshiriki mjadala ule pamoja na wale ambao yasemekana hawakusema mema, ninasema Mungu awabariki wote.
Ndugu Rais, usalama wangu ninamtegemea Mwenyezi Mungu peke yake. Na hapa duniani usalama wangu ninakutegemea wewe baba yangu peke yako. Nimeandika mara kadhaa kuwa ninaporudia kuyasoma niliyoandika siku nyingine hujishangaa, kwa maana yako maandiko mengi ambayo huwa sijui niliyapata wapi. Hubaki tu kujiaminisha kuwa ni maneno ambayo Mwenyezi Mungu alitaka yawafikie waja wake kupitia mimi! Muumba ananitumia tu kama chombo chake.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi aliyepita, Abdulrahman Kinana, alipotumwa na rais wa nchi aje kuongea na mimi mtu ambaye sina hata anwani, nilifarijika sana. Alipoingia nyumbani kwangu aliniambia: “Tumekaa, tumejadiliana na tumekubaliana kuwa haya unayoandika ni mazito sana. Hivyo tumeona kuwa hayawezi yakawa ni mawazo ya mtu mmoja. Litakuwa ni kundi kubwa la watu linaandika lakini linatumia jina la mtu mmoja. Lakini leo nimeamini, haya uandikayo ni mawazo yako peke yako. Mayega, una amani kubwa sana katika kifua chako.” Baba utajisikiaje?
Leo nikikaa chini ya mwembe uleule niliokaa kuandika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu miaka zaidi ya 16 iliyopita wakati kwa msomaji anaona kama yaliandikwa jana tu, nayashangaa matendo makuu ya Mungu aliyonitendea yanavyostaajabisha.
Ninapoona wasomi wakuu wakikitumia kitabu hiki kufanikisha malengo yao ya usomi wa juu zaidi, najisemea katika kifua changu: “Jina la Bwana lihimidiwe!” Leo viongozi wasomi, makini wa nchi jirani ya Kenya wanaizunguka nchi yao wakiihubiri habari njema ya BBI iliyosheheni fikra kutoka katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendeleo huu mkubwa kwangu.
Katibu Mkuu wa CCM wa sasa, Bashiru Ali, alipotoa kauli kuwa viongozi watakwenda huko mashambani waliko wananchi wengi na maskini ambao ndio wapiga kura, wakawaeleweshe faida ya hii miradi mikubwa inayofanyika nchini, ilionekana ni kauli iliyotukuka. Lakini sasa inaonekana hakujua alichokuwa anakisema.
Hata aliosema atawapeleka kufundwa muda unakwisha bado hawajafundwa. Bashiru, neno la Baba Bagonza lisije kuonekana kutimilika kwako. Alisema kuna watu waliopata elimu lakini hawakupata maarifa.
Kwa kuwa Bashiru Ali, Phillip Mangula na wenzake si viongozi wanaochaguliwa na wananchi, basi wao ndio waachiwe jukumu la kuinadi miradi hii mikubwa. Kwa kuwa elimu ya Bashiru haijapelekwa vijijini kwa wananchi wapiga kura, ni lugha gani itatumika mpaka waone faida ya miradi hii mikubwa ambayo hata hivyo kwa maisha yao si kipaumbele?
Hawana kosa wanapoamini kuwa hii miradi mikubwa ndiyo iliyoyafanya maisha yao yawe magumu kiasi hiki.
Anayesema dawa zimesambazwa katika hospitali zetu kwa asilimia 90, akumbuke baba alikwisha kusema wananchi si wajinga. Bashiru nenda Shinyanga kule waliko wapiga kura wengi zaidi. Wagonjwa wanaume na wagonjwa wanawake na wagonjwa watoto wanalala katika wodi moja katika Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.
Kaimu Mganga Mfawidhi, Eradius Kweyamba, anasema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ufinyu wa maabara unaosababisha kukosekana kwa chumba cha damu salama, ukosefu wa mashini ya ultrasound, jengo la upasuaji ambalo halikidhi viwango na matundu ya vyoo.
Bashiru achana na hii biashara ya vyuma chakavu unaowaita madiwani. Nenda kawaambie hao wagonjwa na mganga wao, Eradius Kweyamba, kuwa kwa kuwapenda wananchi wake serikali imeamua kuwachimbia umeme wa ziada kule Stiegler’s Gorge uone watakuweka katika kundi la watu wa aina gani.
Kiongozi wa ujumbe wa makatibu wakuu, Prof. Sifuni Mchome, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria alipofika kule ziwani unakochimbwa umeme alisema: “Tunatembelea miradi yote mikubwa, hapa tumemaliza kutembelea mradi wa reli ya kisasa (SGR). Umeme uliopo nchini unatosha. Lakini tukiongezea na huu, umeme wetu utakuwa wa uhakika zaidi na nafuu.” Kama umeme tulionanao nchini unatosha, ulafi huu wa haraka wa nini? Huyu anakiri halioni vazi la mfalme lakini asemeje? Bashiru nenda Songea vijijini kule waliko wapiga kura ukawaulize ni wangapi wanaijua treni kwa kuiona ‘live’? Atakayewaambia juu ya SGR, halafu wao wakamuona ni chizi, watakuwa wamekosea wapi?
Viongozi wetu wa juu wameonekana wakigongesheana miguu. Tukajiuliza, hivi baba akiamua kucheza reggae na wanae kuna ubaya gani? Kule Kenya rafiki yetu mkubwa, Raila Odinga, amepanda juu ya mgongo wa BBI akiizunguka Kenya yote huku akiimba: “No body can stop reggae!”
Wachambuzi wa mambo wanasema huyo anahangaikia urais wa mwaka 2022. Sisi Uchaguzi Mkuu ujao haujatuathiri? Kuwachagua wapinzani nyongefu, dhaifu wengine wakituhumiwa kuwa vibaraka waje kusaidia kupaka rangi kaburi letu bado hatujaathiriwa na Uchaguzi Mkuu ujao?
Marehemu baba yangu hakuwa cha pombe lakini alikunywa pombe kila siku. Akirudi usiku atatuamsha watoto wote. Alikuwa na ‘kangoma’ kadogodogo, basi atakapigapiga kwa mkono mmoja huku akiimba: “Imbalile, imbalile!” Tulilazimika wote kuimba huku tukicheza mpaka alipochoka.
Kwa utoto wetu hatukutambua kuwa baba alikuwa amelewa. Katika ukubwa huu angetuita tungekwenda kumsikiliza baba mlevi? Kwanza baba mwenyewe kwa kutambua utimamu wetu asingetuita.
Wapinzani ambao hatukuwaita, tumekiri utimamu wao? Hawataki kuihadaa dunia na kuwadanganya wananchi wetu kuwa kuna makubaliano yamefikiwa. Kinachotufanya tuogope maridhiano ni nini? Je, si faida zaidi kwetu kuliko wapinzani?
Bila tume huru ya uchaguzi, hakuna uchaguzi huru na wa haki. Dunia na wananchi waambiwe, kile walichokiona katika kugongesheana miguu, ni nini? Ni reggae ya Raila Odinga kuhusu mgongo wa BBI, au ni ulevi tu wa marehemu baba yangu?