Ndugu Rais, kwa unyenyekevu mkubwa naomba nikutume upeleke salamu. Nikutume unipelekee salamu zangu kwa mwanamwema Kassim Majaliwa, jina lake la kati silijui.
Naujua sana ule wimbo wa ‘Njiwa peleka salamu’ lakini wewe si njiwa; nakutuma kwa sababu wewe ndiye baba yetu.
Ukifika mwambie Kassim Majaliwa kuwa watu wa Mungu wanasema, wanamwombea kwa Mwenyezi Mungu ili alisimamie vyema kwa vitendo, agizo lake kwa wakuu wa wilaya.
Alisema, “Nendeni mkawaongoze watu mkitumia busara na hekima.” Abarikiwe sana mwana huyu. Watu wa Mungu hawaongozwi kwa kutishiwa ‘maguvu’ ya polisi. Kutawala masikini kwa maguvu ya polisi ni kutawala kwa upanga.
Yesu alikataza, akasema, “Atawalaye kwa upanga, atakufa kwa upanga.”
Kassim Majaliwa ni Waziri Mkuu wetu. Nimemfahamu baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu. Tumefuatilia maswali yake aliyokuwa anauliza katika safari zake za bandarini na pengine hata ile kauli aliyoitoa kule waliko wazazi wake.
Lakini hii sentensi ya sasa inampa sifa pia hata aliyemteua kuwa waziri mkuu. Nadhani utendaji kazi wa Aggrey Mwanri ulinichanganya maana nasikia walikuwa ofisi moja.
Ndugu Rais, kauli zisizopimwa zitaleta machafuko katika nchi yetu.
Wakati wa kampeni uliwahi kusema, “Wakati mwingine najihisi kama siyo mwanasiasa hasa.”
Kusema nendeni mkachape kazi, atakayeleta ukorofi
mtieni ndani na kusema nendeni mkawatawale wananchi kwa upanga wenye makali, tofauti ya sentensi hizi iko wapi? Wakorofi wawatie ndani.
Atakayekuwa anaamua kuwa huyu ni mkorofi ni nani? Ni huyo huyo atakayemwadhibu kwa kumweka ndani? Du! Na wengine tulivyowaona kwa mavazi yao kazi wanayoijua ni moja tu – kupambana.
Hawajui majadiliano sembuse kutofautiana. Kazi kwao itakuwa ni moja tu, weka ndani. Watawaweka ndani wote, wakorofi na wasio wakorofi. Baba, amani ya kweli hailetwi na mtutu wa bunduki.
Ndugu Rais, soma kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Kimeandikwa zaidi ya miaka kumi iliyopita lakini kitakusaidia sana katika mambo mengi ya uongozi wa nchi yetu.
Ukurasa wa 106 imeandikwa, “Tunataka Rais mwenye uwezo wa kusoma alama za nyakati. Aelewe kuwa nyakati hizi ni nyakati za mabadiliko. Mabadiliko yana tabia yake. Yakiamua kuja huja. Huwa hakuna mjadala wala mbadala. Ni Rais mwenye busara na hekima tu ndiye huyapokea madiliko kwa amani.
“Nyakati za kukosoa utawala mbovu ukaitwa mchochezi zimepita. Nyakati za kumwona mtu mwenye mawazo ya kisiasa tofauti na wewe kuwa ni adui wa nchi au ni hatari kwa usalama wa Taifa, zimepita, kama zilivyopita nyakati za kuomba kura kwa wananchi kwa kuwapigia zumari na gitaa au kwa kunengua viuno kwa taarabu.”
Watu wanataka Serikali ya watu, inayoendeshwa na watu wenyewe kwa ajili ya watu. Rais lazima atambue ukweli kwamba mawazo yanayotawala nchi huwa si ya wanasiasa peke yao na vyama vyao.
Kuna jumuiya na watu binafsi wenye nafasi kubwa kijamii ambao fikra na shinikizo lao huathiri mwenendo wa siasa, utawala na jamii.” Uongozi uliopungukiwa busara na kukosa hekima huwahesabu hata wale wasio na vyama vya siasa, lakini wanapowasemea wananchi wasio na sauti, huhesabiwa nao kuwa ni wapinzani.
Baba, hii nchi ni ya Waswahili. Ukisema kuna watu wanataka kukuzuia usitekeleze ahadi ulizowapa wananchi, Waswahili watacheka ‘hahahaaaaa…mbaazi huyu, umeshindwa kutoa maua sasa unasingizia jua.’ watasema.
Ndugu Rais, hivi tunawaonaje wananchi wetu? Kuwa wako sawa na kondoo, kwamba watanyoosha shingo zao wenyewe waende wakawekwe ndani?
Mwanadamu ameumbwa kujitetea magumu yanapomfika. Wengine kati ya hao wanaoonekana kama kondoo, ni kama nguruwe. Bila pigo la shoka la kisogoni hachinjwi mtu. Jamani, tumepanga wafe Watanzania wangapi? Watakapoamua kujitetea kwa chochote watakachokuwa nacho muasisi wa machafuko nchini atakuwa ni nani? Alaaniwe na nguvu zote mtu huyo.
Kutawala kwa kutegemea ‘maguvu’ ya polisi ndiyo maana ya kutawala kwa upanga. Baba, narudia, Yesu Kristu mwana wa Mungu aliyehai alikataza.
Alisema, “Atawalaye kwa upanga, atakufa kwa upanga.” Atawalaye watu wa Mungu kwa upanga huku mdomoni yakimtoka mate ya kumtanguliza Mungu mbele, anaweza asifaulu kuichanganya nchi kama ambavyo vikundi kama Boko Haramu na al-shabaab vilivyoshindwa kuiaminisha dunia kuwa ni vikundi vya kidini.
Ulimwengu utawahukumu wote wanaolitumia jina la Mwenyezi Mungu kama kichaka cha kuficha dhamira yao ovu. Zamani tulifundishwa kuwa ni dhambi kubwa kulitaja bure jina la Mungu wako.
Mungu wakweli hawezi kulitangulia kundi la watu wanaotaka kuwatawala wenzao kwa upanga.
Mwanamwema Kassim Majaliwa amesema nendeni mkawaongoze watu mkitumia busara na hekima. Kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu Uk. 110 kimeandikwa, “Hakutakuwa na liwali, mkoani wala wilayani”. Mtu yeyote anayewaongoza watu bila ridhaa yao ni mnyapara tu”.
Wakati wa Yesu mtu huyo aliitwa liwali. Baba, wakuu wa wilaya wote uliowaapisha siku ile wamekwenda kuwa ni wanyapara tu. Wanakwenda kuwatawala masikini wa Mungu bila kuwa na ridhaa hata ya mwananchi mmoja kati ya wale wote wanaokwenda kuwatawala.
Mnyapara hahitaji ridhaa ya mtawaliwa. Nina hakika hii mbele ya Mwenyezi Mungu ni haramu. Kweli kumtajataja sana Mungu siyo kumcha Mungu.
Ndugu Rais, wakati nayaandika haya umekuja ujumbe kutoka sehemu ya mbali, mwanamwema ananiuliza, “Mwalimu mkuu, liko wapi Azimio la Arusha?”
Wananchi wengi wanatuona sisi ni visemeo vyao. Matumaini yao
makubwa ni kuwa wakitufikishia vilio vyao tutawafikishia watawala wao. Watawala nao wanapotusikia wanadhani wanawasikia wapinzani.
Nguvu kubwa walionayo wapinzani inatokana na hofu kubwa walionao watawala. Wanapotetemeka kwa sakata la Lugumi Enterprises na kubabaika kwa Bunge ‘live’, wananchi wanawakubali wapinzani siyo kwa kuwapenda bali kwa mwonekano wao tu kama vile wanawatetea masikini.
Kama yupo kiongozi mcha Mungu wa kweli, ambaye kutoka moyoni mwake anamtanguliza Mungu mbele, awarudishie masikini wa Mungu Azimio lao la Arusha waliloachiwa na Baba yao, Mwenyeheri Julius Kambarage Nyerere.