Ndugu Rais, kama wapo wenzetu waliodhani kuzuia Bunge kuonekana kwa wananchi moja kwa moja kutawafanya wasijue yanayofanyika ndani ya Bunge, sasa wakiri kuwa hawakufikiri sawa sawa. Lisiporekebishwa hili kabla ya uchaguzi mkuu ujao itakuwa ni kwa hasara yetu wenyewe!
Udhaifu wa Bunge katika sakata la CAG, timamu gani hakuuona? Baada ya kijana wetu mahiri Stephen Masele kujitetea Bunge lilioga fedheha likabaki tupu! Huku akicheka, Spika akasema, “Natamani ningefunguka kidogo kuhusu…bahati mbaya kijana wetu huyu hajitambui na hajielewi na kwa sababu ana nguvu…’’ Hawa ndiyo viongozi wetu. Jambo la hatari wao wanachekelea! Wanaomjua Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wanasema wangemkuta akiwa kiongozi angesema, ‘bhosi ni manzi ga nyanza’, yaani wote wawili kama wangekuwa ni bidhaa, wasingepitishwa na TBS, hawatufai!
Aliandika kitabu, Binadamu na Maendeleo, akasema, “Uongozi maana yake siyo kuwakemea watu, siyo kuwatukana watu au kikundi cha watu usiokubaliana nao. Wala siyo kuwaamuru watu kutenda hili au lile. Uongozi ni kuzungumza na kushauriana na watu. Kueleza na kushawishi kwa kutoa mapendekezo yenye manufaa ya kimaendeleo na kutambua kwamba wao ni sawa na wewe. Ni upuuzi kama sisi viongozi tutatumia muda wetu kutukana wanyonyaji hasa kwa kuwa baadhi yetu hatufahamu kazi inayofanywa na baadhi ya hao tunaowatukana’’.
Kila tufanyalo kwa kudhani tunaufifisha upinzani, bila ufahamu tutajikuta tumekuwa dhalili! Kufikiri upya si ujinga. Ujinga ni kung’ang’ana kusukuma kisichosukumika. Plato, mwanafalsafa anayeheshimika sana duniani alisema, “Kuna watu wawili tu wasioweza kubadili mawazo yao. Mpumbavu kuliko wote na mwenye hekima kuliko wote.’’
Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani, tusiwe wavivu wa kufikiri, alituasa Mzee Mkapa! Mwalimu Nyerere anasema, maendeleo tunayoyahitaji ni maendeleo ya watu na siyo maendeleo ya vitu! Akatoa mifano ya ujenzi wa mapiramidi ya Misri na mabarabara ya Kirumi ambayo tunayashangaa hadi leo kuwa yalikuwa ni maendeleo ya vitu siyo maendeleo ya watu.
Anasema ulikuwa ni utamaduni wa wachache na wananchi walio wengi walikuwa kama watumwa walioteseka kwa shughuli za kuleta maendeleo ya majengo na vitu ambavyo hawakuvitumia. Kwa kuwa Mwalimu Nyerere alisema, ni busara kwetu sote kama Taifa kufanya kila tuwezalo ili kizazi kijacho kisije kikatuona na sisi tulifanya upuuzi! Busara si kuukataa ukweli, bali hekima yetu itupatie ujasiri wa kujiuliza maswali makini ya msingi. Kama ni kweli kuwa asilimia arobaini ya bajeti yetu tumeielekeza katika miradi miwili tu ya ujenzi wa Stiegler’ Gorge na ujenzi wa treni yenye mataruma mapana sawa na treni ya TAZARA iliyojengwa na Rais Kaunda wa Zambia na Rais Nyerere, huko siyo kujenga mapiramidi ya Misri na mabarabara ya Kirumi? Wananchi wenyewe waliulizwa wakaridhia kujengwa kwa haya makubwa tunayoyajenga? Isije ikawa leo hii Watanzania wanateseka kama watu wa Misri wakati wanajenga hayo mapiramidi, majengo ambayo hawakuyatumia!
Imetamkwa bungeni kuwa nchi ina upungufu wa madarasa. Shule zetu zina upungufu wa vyoo. Upungufu wa nyumba za walimu kwa asilimia 63. Upungufu wa madawati asilimia 14. Upungufu wa maabara kwa asilimia 84 huku kukiwa na upungufu wa walimu. Kama hivi ndivyo, tunaipeleka wapi elimu ya nchi hii? Hakuna duniani serikali inayoweza kutoa elimu bure.
Fedha zinazotamkwa majukwaani kuwa zimetengwa kwa ajili ya afya ya wananchi ni nyingi mno, lakini ukweli ni kwamba pamoja na zahanati na hospitali za serikali kuwa chache nchini, lakini hakuna dawa wala vifaatiba vya kutosha katika majengo hayo. Wako madaktari bingwa wa kutambua magonjwa na kisha kuandika kwa ufundi aina za dawa katika karatasi na kisha kumkabidhi mgonjwa akajinunulie dawa. Wazee wastaafu wanaoishi kwa kutegemea malipo yao ya Sh 50,000 kwa mwezi kama pensheni, tunapowaambia kuwa hatuwezi kuwaongezea pensheni kwa sababu tunajenga treni na umeme, wanaweza wasitupuuze, bali tujiangalie, tusije tukawa tunajipuuza wenyewe. Mei mosi, Mbeya, wananchi walidai kuwa wakati wa nyongeza ni sasa!
Awamu ya nne ilipoingia madarakani Ndugu Edward Ngoyayi Lowassa akiwa Waziri Mkuu alilitangazia Taifa kuwa kazi ya kwanza itakuwa ni kujenga shule za sekondari katika kila kata!’ Imeonekana! Akasema, “Tukishamaliza, kazi ya pili itakuwa ni kujenga zahanati katika kila kata!’’ Upeo mkubwa unaona maendeleo ya watu! Ole wao waliotunga uongo wa Richmond! Waliikosesha nchi hii na Watanzania kwa ujumla, bahati hii njema! Ukifuta ujinga na wananchi wakawa hawana maradhi, ustawi ambao ndiyo maendeleo yao yanakuja yenyewe bila kutekana wala kutesana au hata kuuana! Kwa fikra za mtu huyu leo Watanzania tungekuwa wapi? Tumebaki kuweweseka masikini sisi, kila tunapolifikiria neno, wapinzani! Kipigo cha mbwa koko alichoshushiwa kijana masikini aliyekuwa anawasemea wananchi wa Makambako kuhusu maji ni ushahidi tosha wa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu!
Bashiru Ally ana hoja kusema, “CCM hatuwezi kuogopa kwenda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama tumejipanga vizuri! Kama tumejenga shule za kutosha zinazoonekana, zenye vitabu bora, vifaa vya kufundishia na walimu wenye morari ya kufundisha, tutaogopa nini? Kama tumejenga zahanati za kutosha zinazoonekana zikiwa na madawa [dawa] ya kutosha, vifaatiba, waganga na wauguzi wenye morari, tutaogopa nini?’’
Bashiru anajua watakachotudai wananchi katika kampeni na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni maendeleo yao, siyo maendeleo ya vitu! Kweli kweli nawaambieni, tukimpuuza Bashiru Ally, ambaye anathubutu hata kulitamka tu, neno, Azimio la Arusha hadharani, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 tutaumbuka! Tunahangaika sana, lakini wananchi watatukataa sisi na mapiramidi yetu tunayoyajenga kwa utamaduni wa wachache huku tukiwafanya wananchi kama watumwa, wakiteseka kwa kujenga ambavyo hawatavitumia! Hizi si fikra zangu bali ni za Baba wa Taifa mwanzilishi wa Taifa hili, aliyejisikia ufahari kuitwa ndugu kati ya ndugu zake wananchi wa kawaida! Tujiulize, mpumbavu ni nani, ni Nyerere aliyesema vyama vingi ni lazima vitakuja au ni sisi tusiotaka vyama vingi?’’