Ndugu Rais, mwishoni mwa miaka ya 1960, tungali vijana rijali na wasomi wazuri, wahitimu wa ‘middle school’ shule ya kati, Rais Julius Nyerere alifanya ziara mkoani kwetu – wakati huo ukiitwa Mbeya.

Wakati ule ukisema Rais Nyerere ilikuwa inatosha. Utaratibu wa kuanza na Mheshimiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu, Mkuu wa nchi kisha usomi wake halafu unataja majina yake yote matatu au wakati mwingine mpaka manne, ulikuwa bado haujaingia.

Sikumbuki lini Nyerere aliitwa dokta. Hata hivyo Nyerere mwenyewe alikuwa anajijua kuwa anatosha katika nafasi ya urais. Hakujaa hofu wala wasiwasi katika macho yake!

Alitaka kusali kanisani kwa sababu ilikuwa Jumapili. Walipomtengea mahali pa peke yake alikataa. Akakaa na waumini wenzake katika ‘benchi’ moja. Akawataka walinzi wake wakae nje akisema ndani ya kanisa mlinzi wake ni Mungu mwenyewe.

Walipotaka kupima hostia yake iliyokuwa akomunike, akawakataza. (Hostia ni mkate unaotolewa katika maadhimisho ya Misa Takatifu kama ukumbusho wa karamu ya mwisho aliyoifanya Yesu Kristo kwa wafuasi wake kabla ya kuteswa na kufa Msalabani). Nyerere alimtanguliza Mungu mbele kutoka kifuani mwake. Kama nchi, hakutunyoosha kwa kutubembeleza wala kwa makali ya upanga! Alitustawisha kwa amani ya kweli, upendo, umoja na mshikamano.

Ndugu Rais, wanao tunapokuja kwako kuomba ututengenezee meza ya maridhiano tunajuta tukikumbuka upendo tuliokuwa nao kati yetu chini ya baba mmoja Rais Nyerere. Alituachia amani na utulivu, upendo, umoja na mshikamano usiokuwa na mfano katika Bara la Afrika na hata duniani kote.

Baada ya yeye kupita wametokea viongozi wengi. Kwa bahati mbaya hajatokea Nyerere mwingine! Ametokea wa kutokea anatuambia viongozi wote waliomfuatia walikuwa wezi watupu. Baba mbona hutuambii wanao huyu mtu, tumsikilize au tumpuuze? Anapanda mbegu ya magomvi miongoni mwetu. Usipotuelekeza wewe baba tumfanye nini mtu huyu, watakapotuelekeza wengine ndiyo utakuwa mwanzo wa kupotea amani yetu.

Tunazidi kukuomba meza ya maridhiano kwa unyenyekevu mkubwa zaidi, kwa kuwa hapa tulipofikishwa sipo. Hakuna aliye na amani kifuani mwake – si mtawala si mtawaliwa. Wote wamejaa hofu. Waliopaswa kutuunganisha ndiyo hao hao wanaotufarakanisha. Tunaongozwa kwa kubaguliwa.

Wengine tusio na hayo tumeachwa tukiwayawaya. Kiongozi bora wa watu hatakiwi kuwa na upande. Hawi na mawazo mufilisi ya kutumia udini, ukabila, ukanda au vyama vya siasa kutaka kuwagawa wananchi. Asiyetumia uelewa mdogo walionao baadhi ya wananchi kuwarubuni. Wanawema eleweni kuwa katika vyama vya siasa vyote vilivyomo ndani na nje ya nchi yetu hakuna hata kimoja ambacho kimewatanguliza wananchi mbele. Viongozi wote wa vyama vyote vya siasa  mawazo yao na matamanio yao yote ni kushika madaraka. Madaraka sasa ni matamu kuliko chochote kwa wenzetu hawa. Rais Nyerere aliondoa utamu wa madaraka na nguvu chafu ya mamlaka kwa kuliweka Azimio la Arusha. Leo miradi mikubwa mikubwa, lakini mradi wa kuwastawisha wananchi moja kwa moja uko wapi? Yuko wapi mwenye hofu ya uwepo wa Mungu awaanzishie wananchi mradi unaogusa maisha yao ya kinyonge moja kwa moja? Kiongozi gani kati ya tulionao leo ambaye akiwaona wanyonge na wananchi maskini wa nchi hii, anamwona Mwenyezi Mungu ndani yao?

Maslahi yao na ya vyama vyao ndiyo kipaumbele chao. Maslahi ya wananchi yanaweza kuja kufikiriwa baadaye au na walio na madaraka ikiwa wataweza kung’ang’ania na kubaki madarakani au na wanaoyatafuta madaraka hayo sasa wakifanikiwa kuwaondoa walioko madarakani, kisha wakawa wao. Eleweni kuwa maisha ya mwananchi siyo kipaumbele cha mwanasiasa wengi. Katika kinyang’anyiro hiki mwananchi unatumika tu kama kivuko dhaifu. Tunakoelekea kwenye uchaguzi wakataeni wote wanaotaka kuwatumia kama ngazi ya kupandia.

Watakaowaambia waacheni hao, tuchagueni sisi, mtakunywa maziwa na asali wapuuzeni kwa sababu nao wanajiita waheshimiwa. Hawajui kuwa mheshimiwa popote duniani ni mtu wa kutumikiwa hata kama haheshimiki.

Mtumishi wakweli anayewatumikia wananchi hawa duni, wakulima na wafanyakazi kwa moyo wa dhati kabisa kabisa, halafu anajiita mheshimiwa! Huyo anatia shaka.

Kuombeana ni jambo jema, lakini maandiko yanasema, unapotaka kumtolea Mungu sadaka nawe ukakumbuka kuna ndugu au watu hupatani nao, iache sadaka yako madhabahuni nenda ukapatane nao kwanza kisha rudi umtolee Mungu sadaka yako.

Mtu kuwaomba watu wamuombee huku ukijua fika kuna watu hupatani nao aelewe kuwa anamchukiza Mwenyezi Mungu. Iko siku atamwadhibu. Ole wao wa kuomba kinyume na maandiko kwa kuwa wanajitakia laana. Nchi hii ni moja na wana wa nchi hii ni wamoja. Mwenye mawazo tofauti na haya, hatufai hata kidogo alituambia hivyo Rais Nyerere!

Wako wanasiasa watakaotaka kuwatumia wananchi kama mtaji katika uchaguzi mkuu ujao. Katika uchaguzi mkuu uliopita wagombea waliowaahidi kuwajengea shule za kutosha na zahanati za kutosha, wawaonyeshe sasa mna macho, mzione. Kila ahadi itekelezwe kikamilifu. Watakaoshindwa kutimiza walichoahidi, wapuuzeni, hawawafai. Nchi hii ina viongozi wengi bora  wanaoaminika kwa kuheshimu ahadi zao.

Mgombea atakayewafaa ni mmoja tu. Yule atakayekuja kwenu na maneno matatu ya kuwatia faraja, ‘Azimio la Arusha!’ Na maneno hayo yasimtoke mdomoni tu, bali yatoke katika kifua chake! Wengine wote ni walaghai tu. Baba siku ya kuwaacha wanao, usijewaacha na hofu, bali katika amani na upendo kama ulivyowakuta.

Wana mtandao walitaka kuiweka madarakani awamu ya tatu. Bahati Baba wa Taifa alikuwa hai akawakemea kwa nguvu kubwa. Wakapotea kwa miaka kumi. Baada ya kifo cha Baba wa Taifa wakaibuka tena na kuiweka madarakani awamu ya nne. Walidumu kwa miaka yote kumi. Lakini leo, siwaoni wananchi wenye vifua vipana kama vya wendawazimu watakaoweza kudumu na watu wasiojulikana kwa miaka kumi. Baba turejeshee tunu yetu ya Taifa, aliyotuachia Baba yetu, Azimio la Arusha!