Na Deodatus Balile

Leo napata tabu kuandika makala hii. Tabu ninayoipata, kumetokea mtikisiko wa ghafla ndani ya saa 72, sura ya siasa za nchi ya Tanzania zimebadilika mno. Ninaye rafiki yangu nimekumbuka maneno yake. Alipata kuniambia: “Usichezee njiti ya kiberiti, ikiwashwa inaweza kuchoma kijiji au taifa.” Nimeshuhudia njiti ya kiberiti ilivyolichoma taifa.

Sitanii, miezi michache iliyopita tulianza kusikia sauti ya aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, kuwa ameanzisha shule ya uongozi. Wenye akili tukajiuliza ni shule hii hii au kuna zaidi ya shule? Tumekwenda tumesikia yaliyomkuta kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Sitamjadili sana.

Desemba 28, 2021 tukamsikia aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, akishangaa kasi ya nchi kukopa kutoka nje. Akaenda mbali zaidi, akasema ipo siku nchi hii itapigwa mnada. Ndugai amezungumzia deni la taifa kuwa limefikia Sh trilioni 71. Hakufafanua, wala hakusema kuwa wakati Rais Jakaya Kikwete anatoka madarakani deni la taifa lilikuwa Sh trilioni 43 na kati ya hizo alizozitaja yeye, kwamba zilikopwa katika Awamu ya Tano.

Ndugai hakufafanua zaidi kusema ukweli wote kuwa kati ya hizo Sh trilioni 71 alizozisema, Rais Samia Suluhu Hassan hadi wakati huo alikuwa amechangia deni la taifa kwa Sh trilioni 1.3 tu. Oktoba 26, 2021 niliandika makala juu ya deni la taifa. Niliiandika makala ile baada ya kuanza kusikia tetesi za wachache wakipinga mkopo wa Sh trilioni 1.3, ambao umetumika kujenga madarasa 15,000 ya sekondari, vituo 237 vya afya, magari ya kuchimba visima vya maji kila mkoa, magari ya wagonjwa, mashine za kisasa za kupima afya za MRI na mengine mengi.

Sitanii, katika makala ile niliandika kuwa si vibaya nchi kuchukua mikopo, ila mikopo ya kibiashara ni hatari kwa ustawi wa uchumi wa taifa letu. Kabla sijasahau. Makala yangu nilisema Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli hakuwa na sababu ya kuwaaminisha Watanzania kuwa tunanunua ndege, tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, tunajenga reli ya kisasa (SGR), tunajenga barabara, vituo vya afya na mengine mengi kwa kutumia fedha zetu, wakati tulikuwa tunakopa.

Nikitumia takwimu alizozitoa Ndugai, ni wazi kuwa katika miaka mitano pekee, Magufuli alikopa Sh trilioni 26.5 (japo ni zaidi ya hapo). Hapa alikuwa na wasaidizi wake, ambapo baadhi walikuwa wanaishi hotelini hata kama wapo Dar es Salaam au Dodoma ambako ni makazi yao ya asili. 

Nilishauri kupitia makala ile kuwa Rais Samia sasa aangalie uwezekano wa kukopa mikopo yenye riba nafuu, itumike kulipa deni la mikopo yenye masharti magumu kwa maana ya mikopo ya kibiashara, maisha yaendelee.

Kauli ya Ndugai imekuwa kama njiti ya kiberiti iliyowashwa. Rais Samia wiki iliyopita aliliambia taifa kuwa kauli hii inatokana na “stress ya 2025”. Akasema kuna watu walikuwa wanasema Serikali ya Awamu ya Sita ni ya mpito. Na wapo waliokuwa wanasema wazi kuwa si Serikali ya Awamu ya Sita, ni ileile ya Awamu ya Tano ila Rais ndiye wa sita. Akasema bora awaondoe kwenye baraza wakafanye siasa vizuri watakutana 2025. Ndugai kwa upande wake mbinyo umekuwa mkubwa, ikabidi aachie ngazi.

Sitanii, tunapopewa nafasi za kutumikia jamii, tufahamu kuwa waliotupatia nafasi hizi ipo siku wanaweza kuzichukua. Kuna kauli za Ndugai zilikuwa zinakwenda mbali zaidi. Wakati watu walikuwa wakilia kwa biashara kufungwa, vyuma kukaza chini ya uongozi wa Rais Magufuli, yeye akasema “Chuma kinafaa kuliko awaye” na “Atake asitake, tutamwongeza muda.” Uvunjaji wa wazi wa Katiba ya Tanzania. Hili liliwakera mno Watanzania.

Kaka yangu Profesa Palamagamba Kabudi, wala hapa sitazungumzia kauli zake tata kama ile ya kumwita Rais Magufuli “Mheshimiwa Mungu” au kwamba “aliokotwa jalalani” profesa mzima, ila kwa jinsi alivyoendesha siasa za uwaziri, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliacha maswali mengi. Nimesikia malalamiko hata kwenye mikataba ya madini, ila hili bado nalifanyia kazi.

Mawaziri walioachwa ikiwa walikuwa wanafanya kazi ya kumchimba Rais aliyeko madarakani (Samia), basi hawakujielekeza vizuri. Sasa kama alivyosema Rais Samia kuwa wamepewa fursa ya kufanya siasa vizuri, binafsi nasubiri kuona kama wataendelea kuwapo CCM au watajiengua wakaanzisha vyama vyao au kujiunga na vilivyopo vya upinzani.

Sitanii, safu hii ni fupi. Mawaziri mliochaguliwa naamini nitapata fursa ya kuwachambua baadhi yenu huko tuendako. Kubwa hapa mmefahamu Rais anataka kuona nini. Anataka utumishi kwa wananchi badala ya majungu ya kuhesabu awamu na kujipanga nani ataingia Ikulu akitoka yeye. Mmepata fursa ya kutumikia Watanzania, mnayo hiari ya kuitumia au pale alipoweka koma, akishika tena kalamu sentensi inarefushwa au kufutwa. Yetu Macho. Mungu ibariki Tanzania.