Machi, mwaka huu, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais John Magufuli, aliliagiza Shirika la Nyumbu lianze kutengeneza magari ya zimamoto.
Hoja ya Rais Magufuli ilikuwa kwamba mpango huo ulenge kupunguza gharama kubwa za ununuzi wa magari hayo kutoka ng’ambo.
Siku chache baadaye, alimteua Balozi Luteni Jenerali mstaafu, Wyjones Kisamba, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumbu.
Ndoto ya kiongozi huyo ya kuona magari ya zimamoto yanatengenezwa, sasa inaelekea kutimia baada ya mmoja wa Watanzania waasisi wa Shirika la Nyumbu, na kwa sasa akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Equator SUMAJKT Company Ltd, Robert Mangazeni, kufanikiwa kuleta teknolojia ya utengenezaji wa magari hayo kutoka kwa washirika wake nchini Urusi.
Kwa teknolojia hii mpya, Tanzania itakuwa nchi ya pili kwa Afrika, baada ya Afrika Kusini kutengeneza magari ya zimamoto.
“Nilipomsikia Rais Magufuli akiagiza zimamoto zianze kutengenezwa hapa nchini nilifarijika sana, na kauli yake aliitoa ikiwa ni wiki chache baada ya kupewa tuzo ya heshima nchini Urusi kutokana na kazi yangu kubwa ya ubunifu wa gari la zimamoto,” anasema Mangazeni alipozungumza na JAMHURI na kuongeza:
“Kuhusu teknolojia ya magari ya zimamoto tumesaini mkataba wa ushirikiano na kampuni kubwa ya ST AUTO iliyoko Moscow, Russia ambayo huunganisha magari ya zimamoto zaidi ya 400 kwa mwaka yakiwamo makubwa na madogo.
“Ni imara kwa matumizi ya mijini na vijijini, kwenye viwanja vya ndege, bandari na kadhalika. Injini zake ni kubwa na imara (V8) na differential zake ni 6×6 na 8×8. Ujazo wake wa maji ni kuanzia lita 500 hadi 15,000 – hii inategemeana na mahitaji ya mtumiaji,” anasema Mangazeni.
Mangazeni anasema yeye na Watanzania wenzake, wakiwamo askari wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa upande wa uhandisi mitambo walianzisha Kampuni ya Equator Automech Ltd. Kabla ya kuanzisha kampuni hiyo walikuwa waasisi wa Shirika la Nyumbu wakiwa vijana wa awali kupata mafunzo katika mataifa ya Ireland, Canada na Russia.
“Nia ya mafunzo hayo ilikuwa ni kuhamishia teknolojia (technology transfer) hapa nchini kwa ajili ya maendeleo yetu. Wastaafu na wadau wengine tulianzisha Kampuni ya Equator Automech Ltd na kuingia ubia na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT). Baada ya kuingia ubia huo tukaunda Kampuni mpya ya Equator SUMAJKT Ltd. Equator Automech Ltd inamiliki asilimia 70; na zinazobaki ni za SUMAJKT,” anasema Mangazeni.
Safari ya mafanikio
Mangazeni anasema mafanikio ya kuleta teknolojia ya utengenezaji magari ya zimamoto hapa nchini yametokana na juhudi zake za miaka zaidi ya tisa akishirikiana na wenzake nchini Russia.
“Nimetuzwa tuzo ya ubunifu kwa kubuni na kufanikisha kuweka kifaa kiitwacho roof monitor katika magari ya zimamoto ambayo hayakuwa na kifaa hicho hapo awali. Roof monitor niliyoibuni hufanya kazi sambamba na ground monitor kwa wakati mmoja katika tukio la kuzima moto.
“Katika ngazi hiyo nilifanya kwa kushirikiana na wahandisi wa Kampuni ya ST-Auto iliyoko Moscow nchini Russia mwaka 2012. Baada ya kufanikisha kazi hiyo, ST-Auto wameendelea kuitumia roof monitor hiyo katika magari ya zimamoto waliyounda kwa kuwa imeonyesha ufanisi mkubwa na wa kustaajabisha katika utendaji kazi tofauti na kabla ya hapo.
“Kutokana na tuzo niliyotunukiwa na ST-Auto, wamekubali kutupatia na teknolojia ya kuunda magari ya zimamoto (technology transfer) kwa Equator SUMAJKT bure bila malipo. Hii imetokana na mchango wangu, na kwa kweli hii ni zawadi kwa nchi yangu.
“Tuzo niliyopewa inakwenda pamoja na kutoa mafunzo kwa mafundi na wahandisi wa Tanzania bure, na wamekubali kuunda vifaa vya zimamoto kwa kutumia viwanda vya hapa nchini (localization).
“Sababu ya kutupatia nafasi za masomo kwa Watanzania kusoma bure ni kwa kuwa wananitambua na wanatumia teknolojia yangu mimi Mtanzania,” anasema Mangazeni.
Anasema kutokana na ushirikiano wa Equator SUMAJKT na ST-Auto wamefanikiwa kuunganisha gari moja kwa kutumia chesesi ya ZIL yenye uwezo wa kubeba maji ya ujazo wa lita 3,000 na povu (foam) lita 300 za kuzimia moto.
“Gari hilo tumeliuza katika Kampuni ya SUMAJKT Guard Ltd. Kwa sasa ndilo gari lenye ubora wa hali ya juu katika magari ya zimamoto hapa nchini.
“Umahiri wa gari letu ulionekana wakati wa mafuriko mwaka jana [2018] katika Jiji la Dar es Salaam. Gari lenye teknolojia yetu ndilo lenye uwezo wa kuingia ndani ya maji likiwa limebeba waokoaji na vifaa vya uokoaji. Magari mengine yote ya zimamoto yalishindwa.
“Utaona kitu ambacho tumefanikiwa kukileta nchini kina manufaa makubwa, na kwa kweli tunamuomba Mheshimiwa Rais Magufuli ajue ndoto yake ya kutengenezwa zimamoto hapa nchini imeshatimia,” anasema Mangazeni.
Anasema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni shahidi wa gari hilo, kwani ameshafika kiwandani na kujionea teknolojia ya utengenezaji wa magari hayo.
Punguzo la bei
Mangazeni anasema agizo la Rais Magufuli la kuhakikisha magari ya zimamoto yanaundwa hapa nchini lililenga zaidi kupata magari yaliyo bora, lakini yenye bei inayohimilika.
Ni kwa sababu hiyo, Mangazeni anasema: “Magari tutakayoyaunganisha katika kiwanda chetu kutakuwa na punguzo kubwa la bei ya magari ya zimamoto tofauti na makampuni mengine yaliyokuwa yakiuza hapo awali.”
Anatoa mfano kuwa gari lenye uwezo wa kubeba lita 6,500 ambalo mwaka 2014 lilinunuliwa kwa dola 442,000 (Sh bilioni 1.038), kwa gari la zimamoto la ujazo kama huo la Equator SUMAJKT aina ya KAMAZ HP 260 6×6 la mwaka 2019 wameliuza kwa dola 335,000 za Marekani (Sh milioni 770.5).
Anasema gari jingine [tunahifadhi mahali lilipo] la mwaka 2012, lilinunuliwa kwa dola 907,667.50 za Marekani (Sh bilioni 2.133); lakini gari la aina hiyo – lenye ubora wa hali ya juu wanaweza kuliunganisha kwa punguzo la asimilia 50.
“Teknolojia yetu ni rahisi na imara kwa watumiaji na tukubali kwamba teknolojia ya zimamoto inabadilika kwa haraka duniani, kwa hiyo na sisi Watanzania tunatakiwa kwenda na mabadiliko mapya ya teknolojia ya zimamoto,” anasema Mangazeni.