Binadamu ni kiumbe mwenye maumbile na sifa tofauti na wanyama wengine. Ana hulka inayomwongoza kujifunza kutoka kwa jamaa yake au jamii yake. Ana dhamiri inayomwezesha kutofautisha kati ya mambo yanayostahili kutendwa au kutotendwa katika jamii anamoishi.
Aidha, binadamu ana nafsi, yaani ile hali ya kujijua kuwa ni binadamu na kuwajua binadamu wenzake. Silka aliyonayo inaweza kuwa ya woga au ujasiri. Sifa zote hizi zinamwezesha binadamu huyu kufanya mema au maovu kwake binafsi au kwa wenzake ndani ya jamaa au jamii anamoishi.
Kutokana na hulka, dhamiri, nafsi na silka aliyozaliwa nayo binadamu huyu anathubutu kujifanyia au kuwafanyia watu mambo mema katika umoja wao na kutwaa heshima, au kujifanyia na kuwafanyia watu maovu katika umoja wao na kukosa heshima. Hapa ninazungumzia umoja kama jamii.
Huyu kiumbe binadamu kwa vile ana nafsi ya kujitambua, ana akili (dhamiri) ya kufikiri na kubuni jambo, hulka ya kumuweka katika tabia ipi, ana wajibu wa kutumia sifa zake kwa umakini ili kuleta utangamano katika jamii.
Sifa na heshima ya binadamu kuwa muungwana na mstaarabu, ukweli unatokana na jinsi anavyotumia viungo vya mwili wake mbele ya jamii. Anapochunga matamshi na matendo mema kama mwongozo wake katika maisha, anajijengea utukufu. Kinyume cha tabia na mwenendo huu, ukweli anajipalia ushenzi ambao ni sifa mbaya.
Zaidi ya maelezo haya, binadamu huyu ni kiumbe cha Mwenyezi Mungu. Ameumbwa na kuletwa duniani apate kumwabudu Mwenyezi Mungu na kufanya mema. Hana ukamilifu wa kufanya mambo ila ana upungufu. Upungufu wake si sababu ya kuwafanyia binadamu wenzake ubaya.
Silka aliyozaliwa nayo ichungwe na dhamiri ili kuweka daima uamuzi mwema. Hulka na nafsi zitawale tabia na mwenendo mzuri. Kadhalika viungo vya mwili wake vitii maagizo na maamrisho yake. Kamwe binadamu asiruhusu silka kutawala maovu.
Ingawa binadamu amepewa sifa nyingi bora na kumtofautisha na wanyama na wadudu, wakati fulani hujifanya ameghafirika na kufanya maasi na maovu kwa binadamu wenzake. Anatumia akili na uwezo alionao kuhatarisha au kuvunja amani.
Binadamu ni mwepesi mno kutumia ulimi vizuri kuwavuta watu walio mbali kumfuata na kumsikiliza na hapo hutwaa sifa njema. Cha kushangaza na kusikitisha, anatumia ulimi wa pilipili kuwatia hofu na kuwatenganisha watu. Anatumia maneno machafu na yenye kiburi ndani yake.
Katika lugha yetu ya Kiswahili tunao msemo: “Kiburi si maungwana.” Kwa maana si ustaarabu wala uungwana kwa mtu kuwafanyia wengine kiburi. Uungwana na ustaarabu ni kutumia ulimi kutamka maneno mazuri kwa mkubwa, mdogo na mamlaka.
Mara kadhaa nimepata kuona na kusikia baadhi ya watu, hasa wanasiasa asubuhi wanatumia ulimi mzuri kuwavuta watu, na inapofika jioni wanatumia ulimi wa pilipili kuwatenganisha watu. Hii maana yake nini? Cheo au madaraka uliyonayo si cheti wala shahada ya wewe kutumia ulimi wa pilipili.
Awe ni raia au kiongozi anapokuwa na ndimi mbili; nzuri na mbaya, ni dhahiri shahiri ana nia ya kuvuja umoja. Nia ya watu ni kujenga, kuimarisha na kudumisha umoja, si kuvunja umoja. Kumbuka kubomoa ni rahisi na kujenga ni ghali. Leo duniani watu welevu na makini wanajuta kuvunja umoja wao baada ya kutumia ulimi wa pilipili.
Hapa nchini ninaona kama ziko dalili za baadhi ya watu wana shabikia matumizi ya ndimi mbili: ulimi mzuri na ulimi wa pilipili katika shughuli za kisiasa, kiuongozi na kimichezo. Wakati dunia ilipokuwa ushenzini watu waliona ulimi wa pilipili ni ujasiri, kumbe ni ujinga na ubwege. Matokeo ni hasara.
Leo dunia imestaarabika na watu wanatumia ulimi mzuri katika kujenga na kudumisha umoja wao katika lengo la kujiletea maendeleo yao kiuchumi, kisiasa na kijamii. Nawaomba na kuwasihi wale wenye hamu na shauku ya kutumia ulimi wa pilipili waache. Tafakari.