Tatizo siyo fedha, kwani Mohammed Dewji ‘Mo’ anaweza kuzitoa isipokuwa masharti magumu aliyoipa Simba ndiyo sababu ya kiungo mkabaji wa timu hiyo, Said Ndemla asuesue kusaini mkataba mpya wa kuendela kubaki kikosini humo.
Simba na kiungo huyo hivi karibuni wameshindwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba wa miaka miwili utakaomuwezesha kuendelea kuichezea Simba.
Awali, ilielezwa kuwa dau kubwa la usajili ambalo linalofikia shilingi milioni 70 alilolitaja ili aongeze mkataba wa kuichezea Simba kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara lilikuwa tatizo.
Kwa mujibu wa chanzo kuwa, meneja wa mchezaji ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kipindi cha utawala wa Jakaya Kikwete ndiye anayesimamia mkataba wake.
Mtoa taarifa huyo alisema, katika masharti hayo aliyoyatoa ni lazima yawepo kwenye mkataba ni lazima kiwepo kipengele cha yeye kucheza mechi na siyo kukaa benchi kama ilivyokuwa kwenye misimu miwili iliyopita ya ligi.
Aliongeza kuwa, katika suala la fedha ya usajili tayari wamelimaliza na kufikia muafaka mzuri na kikubwa wanachovutana katika kipengele hicho cha yeye kucheza katika kila mechi bila ya kujali nafasi atakayopangwa.
“Kikubwa anataka kuwepo kwenye timu kwa faida kwa maana ya kupata nafasi ya kucheza kama ulivyoona misimu miwili iliyopita, Ndema aliishia kusotea benchi wakati bado ana uwezo mkubwa wa kucheza, hivyo hataki kitu hicho kijitokeze tena akiwa na Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.
Simba hivi karibuni kupitia kwa Kaimu Rais wa timu hiyo, Salim Abdallah alisema kuwa: “Timu yetu haitamruhusu mchezaji yeyote wanayemuhitaji kuondoka Simba kwa wale waliomaliza mikataba akiwemo Ndemla.”
Ndema ni mchezaji huru hivi sasa kwa mujibu wa kanuni anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine na kusaini mkataba wa kuichezea. Yanga inatajwa kumuwinda mchezaji huyo ingawa duru za ndani ya Simba zinasema kwamba uwezekano way eye kwenda Jangwani ni mdogo.