Ndege ya kijeshi iliyokua imembeba Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima, sambamba na watu wengine tisa imepoteza uelekeo wake na kutojulikana ilipo
Taarifa kutoka ofisi ya rais imesema ndege hiyo ilianza safari yake majira ya saa tatu asubuhi ya Jana kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Lilongwe, na ilipoteza mawasiliano kwenye maeneo ya milimani upande wa kaskazini mwa nchi hiyo na kupelekea kushindwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu kama ilivyotarajiwa.
Akizungumza kwa njia ya televisheni Jumatatu jioni Waziri wa Habari wa Malawi, Moses Kunkuyu amesema Serikali inasubiri maelezo zaidi kuhusu tukio hilo kutoka kwa jeshi ambalo kwa sasa lipo katika jitihada za kuisaka ndege hiyo.
Kufuatia taarifa hiyo Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, amesitisha safari yake ya kikazi iliyokua imepangwa aelekee huko Bahamas, na ametoa maagizo kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo kuhakikisha wanafanya jitihada za kuitafuta ndege hiyo katika msitu wa Chikangawa.
Chilima amekuwa makamu wa rais tangu 2020. Alikuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa Malawi wa 2019 na kushika nafasi ya tatu. Uchaguzi huo ulimalizika kwa kumpa ushindi mpinzani wake Peter Mutharika lakini ulibatilishwa na Mahakama ya Katiba ya Malawi kwa sababu ya kasoro zilizojitokeza.