Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa siasa wa vyama vingi.
Tangu kurejeshwa kwa mfumo huo mwaka 1992, yamekuwapo manufaa mengi. Tutakuwa watu wa ajabu endapo tutabeza kazi nzuri na ya kutukuka iliyofanywa na baadhi ya wapinzani makini katika baadhi ya maeneo nyeti nchini.
Pengine ni kwa sababu hiyo, Rais John Magufuli, amekuwa akiwasifu baadhi yao. Miongoni mwao ni David Kafulila [kabla ya kurejea CCM], ambaye msimamo wake juu ya EPA umelisaidia taifa.
Licha ya kuwapo umuhimu wa kuendelea kuwa na upinzani imara, hali ilivyo sasa ni kama walioshika madaraka ya dola hawana furaha. Tunaona mivutano mingi ndani na nje ya Bunge isiyo na tija. Huu si mwelekeo mwema.
Kinachopaswa kufanywa na Serikali ya chama kinachotawala ni kuyapokea, kuyasikiliza na kuyachambua yale yanayosemwa na upande wa upinzani. Kuwaona wapinzani kama maadui wa Serikali ni kujaribu kupoteza maana njema ya Kikatiba ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kwa mfano, kwa sasa baadhi ya wapinzani na hata walio CCM wanaamini kuwa mfumo huu wa kuweka kila kitu kwenye kapu moja la maendeleo hauwezi kuikwamua nchi hii kimaendeleo.
Kuamini kuwa nchi hii itajengwa kila kitu kwa maelekezo kutoka, ama Dodoma, au Dar es Salaam pekee, hatuamini kama kuna tija. Nchi hii ni kubwa. Kuzinyang’anya mamlaka Serikali za Mitaa ni kufifisha kasi ya maendeleo.
Kama tatizo ni ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma, tunashauri utafutwe utaratibu wa kimfumo wa kukabiliana na hali hiyo kama waonavyo upande wa Upinzani. Kudhani kwamba kila mradi wa maendeleo sharti uombewe fedha kutoka sehemu moja ya utawala kunaweza kuwahisha maendeleo, ni kuukwepa ukweli.
Haya maneno yanayosemwa na upande wa upinzani, bila shaka hata ndani ya CCM wapo wenye mtazamo huo, lakini wanakaa kimya kwa kuwa wamekubali kuwa waoga. Hao ndiyo huwa mbele kuzungumza pindi mambo yanapokwenda mrama. Huo ni unafiki.
Tunaishauri Serikali isiwaone wapinzani au wanaoikosoa kuwa ni maadui. Badala yake ipokee ushauri, iutafakari na mwishowe ichukue uamuzi kulingana na hoja au ushauri wenye tija kwa taifa. Tunatoa mwito kwa wanasiasa wote kukisoma kijitabu cha TUJISAHIHISHE kilichoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1962. Endapo tutayazingatia yaliyomo kwenye kijitabu hicho, hakika tutaiona Tanzania mpya yenye kujengwa na Watanzania wote bila ubaguzi. Tusiogope kukosoana.