Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amekagua mradi wa Kitalu Nyumba wa kilimo cha mbogamboga na matunda wenye thamani ya Sh. 30 Milioni unaotekelezwa Manispaa ya Singiga.
Akikagua mradi huo leo Septemba 17, 2022 amesema ameridhishwa na utekelezaji wake na kueleza kwamba Manispaa ya Singida ni miongoni mwa wilaya zilizofanya vizuri kati ya wilaya 117.
Ndalichako amesema mradi huo unafadhiliwa na ofisi ya Waziri Mkuu kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alielekeza kubuniwa kwa miradi itakayoweza kuwakomboa vijana kiuchumi na kuwapa ujuzi.
“Miradi ya namna hii inatekelezwa katika mikoa 17 ambapo pia tumezifikia halmashauri za wilaya 117 na vijana takribani 12,000 wamenufaika na mafunzo ya mradi huu wa kitalu nyumba na fedha ambazo zimetumika kwa ajili ya mafunzo hayo ni Sh. 5.3 Bilioni” amesema Ndalichako.
Ndalichako amesema vijana wamekuwa wakifurahia mradi huo na kuwa wataendelea kumpigia hodi Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kusaidia mradi huo wa kuwawezesha vijana.
Aidha Ndalichako amesema programu ya kuwajengea ujuzi vijana kwa mwaka 2022/ 2023 Serikali imetenga Sh. 9 Bilioni na katika mafunzo wanayotegemea kuyafanya ni maeneo maalumu ambayo wanafuga samaki kama kule Ziwa Victoria.
Alisema katika mwaka huu wa fedha wanatarajia kujenga vituo Atamizi vitano ambavyo vitakuwa na vifaa vya usindikaji na uchakataji wa mazao mbalimbali na kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana wanapewa fursa ya kuomba mkopo ili kuongeza thamani ya mazao hayo na Serikali itapitia maombi hayo kuona kama yatakidhi vigezo.
Ndalichako alisema kumekuwa na tabia ya vijana kushindwa kurejesha mikopo ya asilimia 10 wanayopewa na halmashauri hivyo kutokana na hali hiyo hivi sasa wamependekeza wawe wanakopeshwa vifaa kulingana na mahitaji yao na baadaye kurejesha mkopo huo.
“Nina waagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi kuhakikisha wanatoa mikopo hiyo kwa vijana kwani ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kila robo ya mwaka mnatakiwa kufanya hivyo” amesema Ndalichako.
Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2022/ 2023 kupitia mfuko wa Waziri Mkuu zimetengwa Sh.Bilioni 1 kwa ajili ya kuwakopesha vijana hivyo wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo.