Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, ameelekeza kufanyika kwa ukaguzi Maalum juu ya matumizi ya kiasi cha fedha shilingi milioni 694.

Fedha zimetumika kwa ajili ya mradi wa ukarabati wa chuo cha marekebisho na Ufundi Stadi Yombo kwa Watu Wenye Ulemavu, jijini Dar es Salaam kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Prof. Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya vifaa vya ujenzi wakati wa Ukaguzi wa ukarabati wa chuo cha Marekebisho na Ufundi Stadi kwa watu Wenye Ulemavu Cha Yombo.

Waziri Ndalichako ametoa maelekezo hayo baada ya kufanya Ukaguzi wa ukarabati wa chuo hicho na kuonesha kutoridhishwa na gharama zilizotumika kununua vifaa pamoja na ubora wa vifaa vilivyotumika katika ukarabati huo.

“Bei hizi sio za uhalisia kabisa, kuweka Wire mesh kwenye dirisha moja shilingi laki Tano, gharama hiyo ni sawa na gharama ya kutengeneza dirisha kamili jipya” amesema.

Ndalichako amesisitiza yapo mapungufu makubwa ambayo ameyabaini ikiwemo kutozingatiwa kwa makadirio ya Ujenzi (BOQ), hali iliyosababisha kiasi cha fedha zilizotengwa kuisha ikiwa bado ukarabati wa ujenzi wa chuo hicho haujakamilika.

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa ukokotoaji wa gharama hauna uhalisia kwa mujibu wa taratibu za kutumia “Force account”.

“Kila item inayonunuliwa imewekewa labour charge asilimia 30 na Contingency ya asilimia 15 na asilimia 10ya supervison, sasa kwa ununuzi wa extension cable, labor charge na supervision ya nini?”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Prof. Joyce Ndalichako akisisitiza jambo wakati wa Ukaguzi wa ukarabati wa chuo cha Marekebisho na Ufundi Stadi kwa watu Wenye Ulemavu Cha Yombo, Jijini Dar es salaam , wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ngw’ilabuzu Ludigija na Mkuu wa chuo hicho, Bi. Mariam Chellangwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ngw’ilabuzu Ndatwa Ludigija, amesisitiza kuwa ataendelea kufuatilia mradi huo ili gharama zake ziendane na thamani ya fedha zilizotengwa.

Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, katika chuo hicho zinahusika katika ujenzi wa; Majengo ya Mabweni 2, Jengo la Darasa la Kilimo, Majengo 2 ya Nyumba za Watumishi, Jengo la Zahanati, Kituo Cha Kutwa kulelea Watoto na Karakana ya Umeme