Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Algiers
Wakuu wa nchi za kiafrika za kiafrika wametakiwa kuweka msukumo wa pamoja ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Algeria Aymen Ben Abdirrahmane alipofungua Mkutano wa dharura wa Taasisi inayoshughulikia makazi Barani Afrika ya Shelter Afrique unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa CIC Abdelatif Rahal jijini Algiers.
Amesema kuwa hivi sasa Bara la Afrika lina idadi ya watu inayofikia bilioni 1.4 na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi hiyo itafikia watu bilioni 2.5 na hii itakuwa ni asilimia 25 ya idadi ya watu wa dunia.
Akasema kuwa hii inaleta mahitaji makubwa ya makazi bora na huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na miundombinu hivyo akasema kuwa viongozi wa Bara la Afrika wanahitaji kushirikiana vilivyo kukabili changamoto za ongezeko hili ikiwemo kukosekana kwa makazi bora.
Akabainisha kuwa inatarajiwa kuwa mabadiliko ya tabianchi katika nchi nyongi za bara la Afrika yatasababisha mafuriko na ukame wa kupindukia na kuathiri maisha ya wananchi wa bara hili.
Hivyo akaueleza mkutano huo unaohudhuriwa na nchi 44 za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, namna pekee ya kukabiliana na hali hiyo ni kila nchi kuwekeza katika upatikanaji wa makazi bora, kuwa na miundombinu ya uhakika na kusaidia upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu kwa watu wa kipato cha chini.
Akazitahadharisha nchi za kiafrika kuwa kama hazitafanyika jitihada za kuondoa makazi holela na kuwezesha upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu barani Afrika, maisha ya watu yatakuwa mabaya na kuongeza umaskini.
Akasema kuwa jutihada zinazohitajika kufanyika ni pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha nafuu za ujenzi na ununuzi wa nyumba, kutumia malighafi za ujenzi zinazopatikana Barani Afrika, kuwa na teknolojia inayosaidia ujenzi wa nyumba nyingi za gharama nafuu na kupunguza riba ya mikopo katika benki.
Akasema kuwa ni kazima nchi za Afrika kuwekeza katika ujenzi wa nyumba katika vijiji ili kupunguza idadi ya watu wanaohamia mijini ambao wanaongeza mahitaji makubwa ya huduma za kijamii na miundombinu imara.
Katika Mkutano huo unaoendelea leo Jijini Algiers, Mtendaji Mkuu wa Shelter Afrique Bw. Thierno-Habib Hann amewasilisha mapendekezo ya Bodi ya Taasisi hiyo ya Makazi Barani Afrika iliyoleta mabadiliko makubwa ya kimfumo ambayo inaanzisha Benki ya Maendeleo ya Shelter Afrique itakayosaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa nchi wanachama na kuongeza uwekezaji zaidi katika teknolojia na miundombinu katika miji ili kuwa na miji bora, salama na kuboresha maisha ya wananchi wa bara la Afrika.
Nchi 15 za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania ndizo zitakazoridhia kwanza mabadiliko hayo kwa kuwa zina hisa zinakubalika katika muundo wa sasa wa Taasisi hiyo yenye nchi wanachama 44 wa Afrika.