Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kuwa na mashine bora 24 zinazopima makundi ya damu.

Mitambo hiyo ya kisasa zaidi ulimwenguni inahusika pia kupima maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo homa ya ini na virusi vya ukimwi.

Afrika Kusini ndilo taifa la kwanza Afrika kuwa na mashine hizo bora. Aidha, imethibitishwa kuwa, Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kwa kuwa na mashine bora ya kisasa zaidi ya kupima mionzi ya saratani kwa wanawake.

Uchunguzi unathibitisha kwamba mashine hiyo inatumika katika Hospitali ya Ocean Road, iliyojengwa mwaka 1897, Ilala jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amethibitisha yote hayo jijini Mwanza hivi karibuni akisema tayari serikali imekwisha kuzindua mashine hizo kwa ajili ya kuboresha afya za raia nchini.

Waziri Mwalimu amesema mashine 12 kati ya hizo 24 zitatumika kupima makundi ya damu mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, na kulingana na wizara hiyo, mashine moja ina uwezo wa kuchukua sampuli za damu 600 na kupima ndani ya saa mbili hadi tatu.

“Mashine hizi zinapima maambukizi ya H.I.V, homa ya ini A na B, pamoja na ugonjwa wa kaswende,” Waziri Mwalimu amesema na kuongeza kuwa Tanzania inahitaji zaidi ya chupa 500,000 za damu salama kila mwaka.

Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi iwapo serikali ina mpango wa kuanza kuuza damu nje ya nchi, baada ya kujitosheleza mahitaji ya ndani, Waziri Mwalimu akasema: “Ndoto yangu ni kuona Tanzania tunajitosheleza damu salama na kuanza kuuza nje ya nchi. Narudia kutoa karipio kwa watumishi wa hospitali za serikali. Ni marufuku kuuza damu kwa mgonjwa. Ukigundulika hatua stahiki zitachukuliwa bila kuchelewa.”

Akijibu swali kuhusu hospitali binafsi kuuza damu kwa wagonjwa wakati serikali inazuia uuzwaji wa damu, amesema: “Ipo changamoto. Hospitali za serikali tunatoa damu bila malipo. Lakini kwenye hospitali za watu binafsi wao wanauza damu. Tunaangalia namna ya kutatua hii changamoto.”

Ameelekeza kuanzia sasa kila mtu anayechangia damu mara tatu apewe kitambulisho cha kielektroniki na kwamba vitambulisho hivyo vitasaidia anapouguliwa au kuugua asilazimike kuita ndugu kumtolea damu hospitalini.

Magdalena Lyimo, Kiongozi wa Benki ya Taifa ya Damu Salama nchini amesisitiza jamii kuongeza kasi katika uchangiaji damu.

Amesema uwapo wa mashine hizo 24 za upimaji makundi ya damu, utasaidia ugunduzi wa haraka wa magonjwa na serikali imekusudia kuboresha maradufu sekta ya afya.

Kulingana na mahitaji ya damu nchini, serikali imeisifu taasisi ya The Desk and Chair Foundation katika ushirikiano wake kwenye uchangiaji damu.

Wizara ya Afya imesema taasisi hiyo inastahili kuigwa kwa kusaidia jamii, huku serikali ikiahidi kutositisha ushirikiano wake na taasisi hiyo ya kiraia.

“The Desk and Chair Foundation nawapongeza. Mmekuwa mstari wa mbele kusaidia uchangiaji damu,” amesema Waziri Mwalimu. Taasisi hiyo imekabidhiwa tuzo ya kutambua mchango wake wa kuwezesha uchangiaji damu salama ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza.

Tuzo hiyo imekabidhiwa na Waziri Mwalimu kwa Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Sibtain Meghji, katika Maadhimisho ya Siku ya Kuchangia Damu Salama Ulimwenguni ambayo kitaifa yamefanyika jijini Mwanza.

Kwa upande wake, Sibtain Meghji, ameipongeza Serikali ya Rais John Magufuli, akisema: “Jitihada hizi zinaokoa maisha ya wanadamu. Naipongeza serikali kwa utoaji wa bima kwa watoto. Ila bima ya watu wazima bado ni ghali.

“Lakini Mheshimiwa Waziri, nashauri angalau asilimia fulani ya fedha za bima za magari au pikipiki, zingekuwa zinapelekwa kusaidia gharama za ukusanyaji damu salama,” amesema Meghji.

Mwenyekiti huyo wa The Desk and Chair Foundation, amezishukuru taasisi ambazo ni washirika wake, ikiwamo Aga Khan kwa kusaidia zoezi la uchangiaji damu.

“Hatutarudi nyuma,” amesisitiza Meghji huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kujitokeza kutoa damu ili kuokoa maisha ya watu hospitalini.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema mahitaji ya damu duniani ni makubwa, na kila dakika damu salama imekuwa ikihitajika.

Mwakilishi wa WHO nchini, Dk. Anthony Kazoka, amesema msisitizo ni kila watu kujitolea kutoa damu na WHO itaendelea kuwa mstari wa mbele kushiriki uchangiaji wa damu.