Ndugu zangu, Watanganyika na Wazanzibar, natumaini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mwenye kutoa neema kubwa na ndogo hamjambo na mnaendelea na mapambano ya kulijenga taifa lililobarikiwa kuliko taifa lolote jirani.
Nimesikia hivi karibuni kuwa mko kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya, eti mnasema itakuwa katiba itakayolijenga upya taifa lenu na kuleta maaridhiano ya pamoja huku ikiwarejesha kuwa wamoja na kujenga misingi imara ya kiutawala kwa Tanzania, itakayodumu hata kwa miaka 50 au 100 ijayo!
Nimesikia kuwa kuna watu wanataka kukwaza zoezi la kupata katiba mpya na bora eti kwa kuwa wanataka kulinda maslahi na vyeo vyao.
Naomba muwakumbushe kuwa wengi wao hawataishi milele kama jinsi dongo la Tanzania litakavyoishi miaka mingi, najua kuwa wengi wanaotaka kufanya hila na ghiriba za kulinda vyeo na maslahi yao kupitia katiba mnayoiandaa wanajua kuwa hawana tena miaka 50 au 100 mbele ya vifua vyao vilivyo beba roho zao.
Najua kuwa wanatamani waishi milele, lakini kwa mapenzi ya Mungu lazima siku moja warudi mavumbini. Lazima wafe na kuzikwa maana kila nafsi lazima ionje mauti. Tanzania haitakufa itaendelea kubaki, wakumbusheni hili walijue.
Pamoja na kwamba wao watakufa na kuiacha Tanzania, kuna ulazima mkiwa mnaiandika Katiba ya Watanzania kuwakumbusha kuwa katiba inatakiwa kubeba maslahi ya Watanzania wengi kwa umoja wao na haitakiwi kubeba maslahi ya wachache kama kakikundi. Wakumbusheni kuwa Tanzania lazima irudi kwenye misingi iliyoipa heshima mbele ya mataidfa mengine.
Wakumbusheni kuwa kwa sasa ndani ya nchi moja kuna mataifa mawili. Moja kubwa la walalaheri wenye vipato vikumbwa na lingine dogo la walalahoi wapiga miayo wenye kipato kiduchu.
Kila Mtanzania mwenye akili timamu akumbushwe umuhimu wa kuwa na katiba bora isiyompendelea mtu yoyote mbele ya sheria au huduma za kijamii maana ndani ya Tanzania ya sasa kuna watu hawaguswi wala kuadhibiwa kwa kuvunja sheria. Wao wanalindwa kwa namna yoyote ile na kuna kundi ambalo lenyewe linaguswa na sheria kwa kasi, nguvu na ari ya ajabu. Makundi haya yote yanaishi kwenye nchi moja lakini ndani ya mataifa mawili. Taifa lisiloguswa na taifa linaloguswa muda wowote.
Umuhimu wa kipekee uwe kwenye kuhakikisha kuwa katiba yenu haichezewi kwa namna yoyote ile, hakikisheni kuwa haihodhiwi na kakundi au kikundi chochote kwa manufaa yao. Kila mtu ajue kuwa katiba ni mali ya Watanzania wote kama jinsi yalivyo madini au rasilimali zozote zilizoko ndani ya ardhi ya Tanzania.
Katiba lazima ilinde rasilimali zenu kwa uwazi na ziwajibike kuwanufaisha ninyi kwanza kabla hazijanufaisha wengine, maana ndani ya nchi yenu kuna kataifa kananeemeka sana kuliko kale kataifa kengine kanakofukuzwa kwenye rasilimali zinazowazunguka eti kupisha wageni.
Amkeni mkomaee kupitia Katiba mpya msiruhusu kale kanchi kenye wazito wenye watoto wanaopata elimu bora kwenye shule bora huku wakiwapuuza na kuwatungia sera ninyi na watoto wenu mliopigika na kuwapeleka zile shule ambazo hazina walimu wa kutosha, vifaa wala maabara ambazo mwisho wake huwa wanaishia kufaulu huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.
Taifa la watu wenye uwezo wa kupata elimu bora peke yao lisiruhusiwe kwenye uso wa dongo la Tanzania kupitia Katiba mpya ili ninyi wananchi
wa Taifa lenye kupata elimu duni na bora elimu muanze kufaidi upya matunda ya elimu bora kwenye nchi yenu. Hakikisheni Katiba mpya inaweka msingi wa haki ya elimu bora kwa kila Mtanzania.
Kuna Taifa moja ndani ya nchi yenu linapigania uwazi na uwajibikaji kuwa tunu ya Taifa, hili ni jambo jema maana kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji kutawaepusha na mikataba ya hovyo na hujuma ya rasilimali zenu. Wambieni watu wa lile taifa lingine la wale wachache kuacha kupigania eti kuhakikisha uwazi hauwi tunu ya Taifa.
Ndugu zangu, wakumbusheni tena jamaa zenu kuwa nchi mbili zilizoungana lazima ziridhiane kwa muafaka wa pamoja na muundo wa muungano. Lazima uwe muungano wenye baraka na muafaka wenye maridhiano ya pamoja bila kuogopa kuzungumza na kutatua kero za muungano ambazo moja ya kero imeshasemwa kuwa ni kutokuwepo kwa nchi inayofichwa jina lake la asili lililotumika kwenye kuungana na nchi iliyoko visiwani.
Nawaandikia waraka huu huku nikiwataka mtambue kuwa nami ni Mtanzania ninayechukizwa na uwepo wa haya mataifa mawili ndani ya nchi yetu.
Huu ni wakati mwafaka kupitia Katiba hii kujenga taifa moja kubwa lenye nguvu ndani ya nchi moja na siyo kuwa na mataifa mawili kama ilivyo sasa ndani ya nchi ya moja.
0713 246 764