Na Nizar K. Visram

Kupiga vita umaskini ni ajenda inayozungumzwa sana, hasa katika Bara la Afrika. 

Aghalabu watu hutofautiana katika mbinu za kufikia lengo hilo. Kuna wanaosema ni halali kwa nchi ‘maskini’ kuomba misaada kutoka nchi ‘tajiri’.

Wengine watasema hatuna wajomba wa kuwategemea, kwa hiyo njia pekee ni kutegemea nguvu zetu na maliasili zetu tulizobarikiwa. 

Mwananchi wa Zambia, Dambisa Moyo, ameandika kitabu (Dead Aid) akichambua suala hili kwa kusema kuwa imekuwa kawaida kwa nchi za Kiafrika kutegemea ‘misaada’ ya kigeni. 

Anasema miaka 50 iliyopita tulipewa zaidi ya dola trilioni 1 kama ‘misaada ya maendeleo’. Hata hivyo si tu umaskini ungalipo bali tumegeuka ombaomba kwa kutegemea ‘misaada’ zaidi na zaidi. 

“Kwa maneno mengine misaada imetudumaza, imetufanya tuwe tegemezi na imechangia kuongezeka kwa ufisadi na rushwa katika jamii zetu, anaongeza Moyo.

John Foster Dulles, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mwaka 1956 alisema: “Kile kinachoitwa misaada ya maendeleo tunayotoa kwa kweli si misaada kwa nchi maskini bali inatusaidia sisi wenyewe, ni mkakati wetu wa kutekeleza sera zetu za kimataifa.”

Tunapozungumzia misaada ya kigeni kwa kawaida huwa tunafikiria mashirika mawili ya kimataifa, nayo ni Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF). 

Mwandishi Michael Hudson anasema wakoloni walipovamia Afrika na Asia lengo lao lilikuwa ni kudhibiti ardhi na uchumi kwa kutumia majeshi na kusimika bendera katika nchi zetu. 

Baadaye wakaona si lazima kutumia majeshi na kupandisha bendera zao. Si lazima kuwatuma magavana kuja kutawala makoloni. Njia rahisi ni kutumia fedha kama silaha ili kudhibiti kilimo chetu, ardhi zetu na viwanda vyetu. 

Hudson anasema WB na IMF ni silaha za kifedha zinazotumiwa kuzifanya nchi ‘maskini’ zitegemee nchi ‘tajiri’. Wizara ya fedha ya Marekani nayo imesema WB ni shirika linaloongozwa na Marekani, likiwa na kazi ya kutekeleza mikakati ya kiuchumi na kisiasa ya  Marekani. 

Mbinu moja inayotumika ni kutukopesha kwa masharti kuwa tunabadilisha sera kama vile kubinafsisha mashirika ya umma, kubana matumizi katika huduma za kijamii na kuruhusu soko huria kwa kuruhusu bidhaa za kigeni. 

Nchi takriban 100 zimetekeleza masharti haya. 

Aliyekuwa mchumi mkuu wa WB, Joseph Stiglitz (mshindi wa Nobel), aliandika kitabu kinachoelezea jinsi masharti haya yanavyosababisha umaskini.

Huko Korea Kusini wagombea wanne wa urais walitakiwa kusaini ahadi kuwa iwapo watachaguliwa, watatekeleza masharti ya IMF. 

Brazil nako kabla ya Rais Lula kuchaguliwa alisaini ahadi hiyo. Nchi kama China na Malaysia zilipuuza masharti ya IMF na leo wamepiga hatua kubwa. 

Wanaotetea misaada ya kigeni aghalabu huwa wanatoa mfano wa misaada iliyotolewa na  Marekani kwa nchi za Ulaya Magharibi baada ya Vita Kuu ya Pili. Mpango huu (Marshall Plan) madhumuni yake yalikuwa ni kuzisaidia kampuni za Marekani kupata masoko ya nje.

Kabla ya vita Ulaya ilikuwa ni soko kubwa kwa bidhaa za Marekani. Vita ikaifilisi Ulaya ambayo ilikosa fedha za kuagiza bidhaa kutoka nje. 

Kampuni za Marekani zikaathirika vibaya na ndipo mwaka 1947 Naibu Waziri wa Uchumi akaelezea mpango huo kwa kusema: “Tuwe wakweli bila ya kuficha, tunalihitaji soko kubwa la Ulaya ili kuuza bidhaa zetu.” 

Alikuwa akimaanisha mikopo ya Marekani kwa Ulaya ni kuwasaidia kununua mafuta na chakula vilivyoadimika katika nchi za Ulaya baada ya kumalizika vita. Matokeo yake kufikia mwaka 1950, Marekani ikawa inatawala soko la chakula si tu Ulaya, bali duniani. 

Nchi kama Argentina, kwa mfano, iliyokuwa ikiuza chakula chake nje ya nchi ikalazimika kuagiza kutoka Marekani. 

Graham Hancock alikuwa mchumi aliyeajiriwa na WB akishughulikia misaada na mikopo. Akaacha kazi na akaandika kitabu: ‘Lords of Poverty’ kinachoeleza mbinu walizokuwa wakitumia kuwashawishi watawala wa nchi maskini kukubali masharti ya WB. 

Sharti moja ni kukubali ushauri wa ‘wataalamu’  kutoka WB ambao wanalipwa mishahara minono ili ‘kuishauri’ serikali.

Huo ushauri anaotoa ungeweza ukatolewa na wataalamu wazawa ambao wanalazimika kufanya kazi chini ya bosi kutoka WB.

Haya yanayofanywa na WB yanafanywa pia na mashirika ya misaada ya kimataifa. Nchi tajiri inasaini mkataba wa msaada na kutaka mashirika hayo yaajiriwe kama washauri. 

Nusu ya fedha za misaada zinakwenda kulipa mishahara na marupurupu ya washauri. Mashirika haya ya kigeni yameenea katika nchi za kusini, yakishughulika na miradi ya kila aina kwa kisingizio cha kupambana na umaskini.  

Tukifananisha Afrika na Asia tunaona kuwa misaada zaidi ilikwenda Afrika kushinda Asia. Kwa mujibu wa ripoti ya WB, watu milioni 700 walijitoa kutoka katika umaskini kuanzia 1981 hadi 2010. Kati yao milioni 627 ni nchini China na milioni 73 ni kutoka nchi zilizobaki.

Kwa maneno mengine, asilimia 90 ya watu walioachana na umaskini walitoka China, nchi ambayo haikutegemea misaada. Ni dhahiri kuwa misaada si muarobaini wa umaskini. Wachambuzi wanasema nchi zilizotegemea misaada ndizo zimedidimia badala ya kuja juu. 

Yaani misaada imeshindwa kutibu ugonjwa wa umaskini barani Afrika. Mwaka 1970 asilimia 10 ya watu maskini duniani walikuwa wakiishi Afrika. Leo wameongezeka na kufikia asilimia 75. Watafiti wanasema ifikapo mwaka 2030 watafika asilimia 90.  

Baya zaidi ni pale misaada yenyewe inapotumika vibaya au inapoliwa na mafisadi wachache. Mfano mmoja ni misaada kutumika katika miradi isiyo na tija wala isiyoleta maendeleo kwa wananchi, yaani misaada inapochukuliwa kama mapato ya serikali, hivyo hutumiwa kulipa posho na mishahara au anasa za watawala.

Bara la Afrika hupokea takriban dola bilioni 50 kila mwaka kama misaada. Badala ya fedha hizi kuwasaidia wananchi milioni 600 wanaoishi maisha ya ufukara, huwa zinawatajirisha mafisadi. 

Hii hufanyika si tu katika fedha taslimu, bali hata misaada ya vitu kama chakula na dawa. Kwa mfano,  mwaka 1992 Marekani ilidai inaisaidia chakula Somalia. 

Badala ya kununua chakula kutoka mikoa inayozalisha chakula na kuwapa waliokumbwa na njaa, chakula kilinunuliwa kutoka Marekani na kuingizwa Somalia.   

Matokeo yake wakulima wa Somalia wakakosa soko, hivyo wakaacha kuzalisha. Baada ya muda nao wakawa tegemezi wa chakula kutoka  Marekani. Misaada iliposimamishwa Somalia ikawa soko la chakula kutoka Marekani. 

Mwaka 1997 Shirika la Misaada la Marekani (USAID) likasema:

“Wanaofaidika na msaada wa chakula siku zote ni Marekani. Wakulima wetu wanapata soko la kuuzia mazao yao.”    

Mfano mwingine ni misaada ya dawa. Mara nyingi dawa nzuri inaweza kupatikana kwa bei nafuu lakini wafadhili wanalazimisha dawa iagizwe kutoka kwao na kwa bei ya juu hata kama dawa hiyo haifai. Mfano halisi ni pale wafadhili walipotoa dawa ya ukimwi kwa bei ya dola 15,000 ingawa iliweza kupatikana kwa dola 350.  

Ni kwa sababu lengo la msaada lilikuwa kuzipatia kampuni za Magharibi soko. Ndiyo maana misaada ya Uingereza iliambatana na masharti kuwa nusu ya fedha zitumike kununua bidhaa kutoka Uingereza. 

Pia zaidi ya asilimia 70 ya misaada ya  Marekani hutumika Marekani. Halikadhalika na misaada ya Ufaransa na Japan.  

Mwaka 1970 nchi za Magharibi ziliahidi kutoa asilimia 0.7 ya mapato yao (GNP) kama msaada kwa nchi maskini. Ni nchi nne tu zilizotimiza ahadi hii, nazo ni Norway, Sweden, Denmark na Luxembourg. Yaani jumla ya fedha walizoahidi na kushindwa kutoa ni zaidi ya dola trilioni 3.

Badala yake ilipofika mwaka 2019 wakatoa jumla ya dola bilioni 150. Wengine watasema hizi ni fedha nyingi, lakini ni vizuri tukafananisha na dola trilioni 1.8 wanazozitumia katika silaha za kivita. 

Pia wanatumia mamia ya mabilioni ya dola kama ruzuku kwa kampuni zao za kimataifa. Marekani peke yake inatumia mara 25 zaidi katika vita kuliko misaada. 

Wakati huo huo ni vizuri tukajua kuwa fedha ambazo zinatoka nchi maskini kwenda nchi tajiri ni zaidi kushinda misaada kutoka nchi tajiri. Inakisiwa kuwa kwa kila dola wanayotoa kama msaada wanachukua dola 24. Nchi maskini ndizo zinasaidia nchi tajiri na si vinginevyo. 

Wakati huohuo ni vizuri tukajua kuwa hiyo misaada wanayozungumzia ni pamoja na fedha za kuzijenga nchi walizobomoa. 

Huko Iraq na Afghanistan wamepiga mabomu na kuwaua raia pamoja na kuteketeza hospitali, shule, madaraja, barabara, viwanda na kadhalika. Halafu wanajaribu kujenga baadhi ya vitu hivi na wanadai hiyo ni misaada.

[email protected] 

0693-555373