Wizara ya Madini imetoa takwimu za mapato ya madini zinazoonyesha nchi ilivyoibiwa kwa miongo mingi.
Waziri wa Madini, Doto Biteko, amesema wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani miaka minne iliyopita, mapato yaliyotokana na mauzo ya madini yalikuwa Sh bilioni 196 pekee kwa mwaka.
“Tumetoka kukusanya mrabaha wa madini wa Sh bilioni 196 kwa mwaka na sasa tunaelekea Sh bilioni 470 kwa mwaka,” amesema Biteko na kuongeza:
“Kiwango hiki kinajumuisha madini yote. Wapo waliodhani baada ya kufungwa kwa muda kwa baadhi ya migodi mikubwa mapato yangeshuka, kinyume chake mapato yamepanda.
“Mapato haya yameongezeka kutokana na Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2017, ujenzi wa ukuta Mirerani na uanzishwaji wa maduka ya madini,” amesema.
Takwimu nyingine ‘zinazoshangaza’ ni za madini ya tanzanite yanayochimbwa sehemu moja tu hapa duniani, yaani Mirerani mkoani Manyara.
“Tumetoka kukusanya tanzanite kilo 166 kwa mwaka (2016/2017) na kufikia tani 1.09 katika kipindi cha mwaka 2018/2019,” amesema.
Biteko amesema: “Wachimbaji wadogo waliitwa wachimbaji haramu, walikuwa wanaitwa wavamizi, na majina mengine mabaya. Wageni walikuwa wanaitwa ndio wachimbaji halali na wachimbaji wanaostahili kuchimba madini.
“Mheshimiwa Rais [John Magufuli] alipoingia madarakani kazi yake ya kwanza ilikuwa kuhakikisha kwamba Watanzania wenyewe wanachimba na kuchangia kwenye pato la taifa.
“Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, maeneo mengi yaliyokuwa yamehodhiwa na watu ambao walikuwa hawayaendelezi, yamefutwa.
“Kwenye mtandao wetu tuna leseni zaidi ya 33,000 na tayari tumekwishafuta leseni zaidi ya 13,167 zilizokuwa zimehodhiwa na watu bila kuendeleza maeneo husika, na hizi sehemu kubwa tutawapatia wachimbaji wadogo, na kwa hiyo suala la wachimbaji wadogo kupewa maeneo si suala tena. Hawakimbii-kimbii tena.”
Biteko amesema mafanikio makubwa katika sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini, kufunguliwa kwa masoko ya madini, ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo ambao awali walibandikwa majina kama wachimbaji haramu na wavamizi; pia kufanya utafiti wa madini na matokeo kuyapeleka kwa wachimbaji wadogo.
Kwenye mafanikio hayo, Biteko amesema: “Jambo jingine la muhimu sana lilikuwa ni wapi wachimbaji watauza madini yao. Wachimbaji walikuwa wanauza kwenye mazingira ambayo walikuwa wanapunjwa sana, na dhahabu yenyewe waliyokuwa wanaipata ilikuwa haieleweki inakwenda wapi. Mchimbaji alikuwa hapati tija lakini nchi ilikuwa haipati stahiki yake.
“Mheshimiwa Rais John Magufuli akaagiza yajengwe masoko ya madini, na ninafurahi kusema kuwa katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya Awamu ya Tano, masoko yamefunguliwa na yamekuwa mfano katika ukanda wetu wa Afrika kutokana na aina ya masoko tuliyonayo ambayo yanawawezesha watu kuuza dhahabu zao kwa amani, uwazi na bei ya bila kupunjwa na hii ni historia – hakujawahi kuwapo masoko ya madini hapa nchini.”
Biteko amesema kwa mageuzi haya katika sekta ya madini, Rais Magufuli atakumbukwa vizazi na vizazi kwa kulinda rasilimali za nchi.
“Tunaendelea kuwaomba Watanzania waendelee kupeleka madini yao kwenye masoko haya. Ukiuza kwenye masoko, kwanza utapata bei halisi, hautauziwa madini feki na utalipa kodi za serikali,” amesema.
Maeneo mengine ambayo Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Madni ijielekeze ni kwenye utafiti katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji.
“Ukienda kule Katavi ambako Mheshimiwa Rais alikuwa na ziara hivi karibuni; maeneo mbalimbali tumefanya utafiti, tumefanya utafiti Buhemba (wilayani Butiama, Mara). Data tulizozipata tumewapatia wachimbaji wadogo ili ziweze kuwasaidia kwa sababu tunataka kuwahamisha watoke kwenye uchimbaji wa kubahatisha waende kwenye uchimbaji wa uhakika,” amesema.
Mapato Mirerani yapaa
Taarifa za kijiolojia hadi sasa zinaitambua Mirerani, Manyara nchini Tanzania kuwa ndiko mahali pekee katika sayari hii kunakopatikana madini ya tanzanite.
Kwa upekee huo, Tanzania imekuwa ikijivunia madini hayo, lakini bila kupata faida yoyote kwa taifa. Kenya, Afrika Kusini na India zinawika duniani kote kama ndio ‘wazalishaji’ wakuu wa vito hivyo ilhali wakiwa hawana hata chimbo moja. Katika mji wa Jaipur nchini India, watu zaidi ya 500,000 wamepata ajira kutokana na kukata madini hayo.
Biteko ameeleza mapinduzi makubwa yaliyofanywa ndani ya miaka minne katika upande wa vito vya tanzanite.
“Baada ya Mheshimiwa Rais kuona kuna utoroshaji mkubwa wa madini ya tanzanite, aliagiza Wizara ya Madini ichukue hatua mbalimbali, akaagiza ujengwe ukuta. Ninafurahi kuwa tumejenga ukuta. Baada ya ujenzi wa ukuta wa Mirerani, tayari tumeshafunga kamera za usalama (CCTV). Kwa sasa wizi, utoroshaji wa tanzanite, vimedhibitiwa na ndiyo maana mapato yameongezeka na ukusanyaji madini umeongezeka.
“Utoroshaji umepungua kwa kiasi fulani, sisemi utoroshaji umekwisha, lakini kwa kiwango fulani utoroshaji umepungua sana na hata mapato yenyewe yamekuwa makubwa zaidi ukilinganisha na hapo awali,” amesema.
Takwimu zinaonyesha kuwa kabla ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017; mwaka wa fedha wa 2016/2017 tanzanite iliyochimbwa ni kilo 196.6 na serikali iliambulia mrabaha wa Sh milioni 71.9 pekee.
Mwaka 2017/2018 tanzanite iliyotajwa kuchimbwa ni kilo147.7 pekee na mapato yaliyoingia serikalini kutokana na vito hivyo ni Sh milioni 166.1 tu.
Baada ya ujenzi wa ukuta tu, kiwango cha vito vya tanzanite kilichorekodiwa kwa mwaka 2018/2019 kilikuwa kilo 781.2 ambazo ziliiwezesha serikali kupata mrabaha wa Sh bilioni 1.437.
“Utaona kuna mafanikio makubwa sana. Mwaka 2018/2019 (Juni) tanzanite iliyorekodiwa ni tani 1.09; na serikali imepata mrabaha wa Sh bilioni 2.829. Mwaka 2019/2020 tumekusudia kupata zaidi. Haya ni mafanikio makubwa. Bado tunaamini tunaweza kupata kiwango kikubwa zaidi kuliko hicho,” amesema Waziri Biteko.
Katika kuhakikisha kuwa tanzanite inaendelea kudhibitiwa ili taifa lifaidike zaidi, Ofisi ya Madini Mirerani imetoa mwongozo unaotaka shughuli zote za uchimbaji na uongezaji thamani madini hayo zifanyike ndani ya eneo la ukuta Mirerani.
Wamiliki wa migodi na wenye leseni za madini ya vito, wafanyabiashara, wachakataji na wadau wa tanzanite wametangaziwa kuwa kuanzia Novemba Mosi, mwaka huu baada ya kufanyiwa uthaminishaji na kulipa tozo mbalimbali, wanatakiwa kufanya yafuatayo:
Kuhakikisha kuwa madini ghafi yote yawe yameongezewa thamani kabla ya kuruhusiwa kutoka nje ya ukuta wa Mirerani.
Endapo madini yatakuwa hayajaongezewa thamani, yatahifadhiwa ndani ya ukuta wa Mirerani katika jengo la soko (one stop centre) hadi yatakapoongezewa thamani na mhusika.
Wanunuzi wakubwa (dealers) wametakiwa wafike katika ofisi ya madini Mirerani wapewe utaratibu na maeneo ya ujenzi wa ofisi zao ili wanunue na waongeze thamani madini ndani ya ukuta wa Mirerani kabla ya kuruhusiwa kuyatoa nje kwa ajili ya kusafirisha ndani na nje ya nchi.
Kina mama wa ‘magonga’ wao wataendelea na utaratibu wa kila siku wakati ofisi ya madini ikiendelea kuwatafutia masoko.
Madini ghafi yote yaliyopo nje ya ukuta ambayo hayajaongezewa thamani, wenye madini hayo wanatakiwa wayarudishe ndani ya ukuta wa Mirerani kwa ajili ya kuhifadhiwa na kuongezewa thamani.
Taarifa hiyo imehitimisha kwa kuonya: “Yeyote atakaepatikana na madini ghafi nje ya ukuta wa Mirerani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.”
Kwa upande wao, baadhi ya wachimbaji na wauza madini waliozungumza na JAMHURI wamekosoa agizo hilo wakisema biashara ya madini inafanywa kutokana na mwenye madini anavyoona akiuza kwa wakati fulani atapata faida.
Wamesema madini yakishachimbwa na kulipiwa kodi na tozo zote, yanakuwa mali ya mhusika, kwa hiyo yeye ndiye anayestahili kuamua auze kwa wakati gani.
“Tunalazimishwa kuchonga madini, huwezi kuchonga madini kama unavyomenya muwa, kwani katika kuchonga unachonga kulingana na mahitaji ya mteja. Kuna aina nyingi sana za uchongaji madini. Unaweza kuchonga kwa namna ambayo mteja haitaki, hapo utafanyaje? Ni vizuri tutunze madini na tuyachonge baada ya kumpata mteja.
“Sheria hii [mwaka 2017] inahitaji marekebisho kwa sababu inatuzuia kukaa na madini hata kama tunataka kujua kwanza mteja anataka achongewe madini kwa mchongo upi,” amesema mmoja wa wauza madini.
Waziri Biteko kwa upande wake amesema sekta ya madini ni muhimu katika ukuzaji uchumi wa taifa, na ametoa tahadhari kuwa yasiposimamiwa vizuri yatanufaisha nchi nyingine.
“Tutaendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapa maeneo ya kuchimba, kufanya utafiti na kusimamia masoko ili wauze kwa tija – kwa kuwaondolea urasimu na kodi mbalimbali ambazo zinawakwaza.
“Tulikuwa na kodi nyingi ambazo baadhi Mheshimiwa Rais aliagiza ziondolewe. Tunataka Watanzania waishi kama wachimbaji wa daraja la kwanza na wasije kuonekana kama wachimbaji haramu,” ameeleza Biteko.