Napongeza uamuzi wa kutazamwa upya msimamo wa safari za usiku kwa magari, hasa mabasi.

Uamuzi wa kuzuia mabasi kusafirisha abiria usiku ulitolewa wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Pili kama suluhisho la ajali za mabasi kwa nyakati hizo. Aliyetangaza uamuzi huo ni Waziri Mkuu wa wakati huo, mzee John Malecela.

Ukiacha sababu ya ajali, sababu nyingine iliyokuwapo, japo viongozi hawakuwa na ujasiri wa kuitamka wazi wazi, ilikuwa ni ongezeko la ujambazi – utekaji wa mabasi na magari mengine nyakati za usiku.

Tumeendelea na utaratibu huo hadi hivi karibuni ambapo mamlaka husika zimeonyesha kuyakubali mabadiliko walau kwa kubadili muda wa mabasi kuanza na kuhitimisha safari. Badala ya saa 12, sasa mabasi yanaweza kusafiri kuanzia saa 11 alfajiri.

Uamuzi wa serikali kwa wakati huo wa kuzuia mabasi kusafiri usiku ulisaidia kwa kiwango fulani kupunguza ajali, lakini kadiri siku zilivyosonga ndivyo ilivyothibitika kuwa tatizo la ajali si usiku pekee, bali yapo mambo mengine mengi. Mathalani, ajali nyingi na mbaya zaidi zilizoua makumi ya abiria ziliendelea kutokea nyakati za mchana. Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kukabiliana na janga hili kwa kiwango cha kuleta matumaini.

Chanzo cha ajali au ujambazi ni zaidi ya giza. Hili limekwisha kuthibitika vizuri. Kwa kuwa ajali zimeendelea kutokea mchana, ile dhana kwamba usiku ndiyo balaa, inafutika.

Pia utafiti uliofanywa na watu na taasisi mbalimbali umebaini kuwa uzembe/upuuzi wa madereva, wembamba wa barabara na matumizi mabaya kwa watumiaji wengine wa barabara ni vyanzo vikuu vya ajali.

Kwa kuzingatia majibu ya utafiti huo, hatuna budi kupata tiba ya vyanzo hivyo ili barabara zetu ziendelee kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Hoja yangu hapa ni kwamba hatuna budi kujitazama upya kama kweli tunahitaji kuibadili nchi yetu. Kuibadilisha nchi yetu maana yake tufanye kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki.

Malengo mengi mazuri hatuwezi kuyafikia endapo tutaendelea kupangiana muda wa kuamka, muda wa kufanya kazi na muda wa kulala. Mabasi na hizo treni za umeme zinazokuja vinapaswa kufanya kazi kwa saa 24.

Hatuwezi kujitanabaisha kuwa nchi ya amani, lakini tukawa ndio wa kwanza kufunga maduka ili kuwakwepa majambazi na wahalifu wengine. Jiji la Kampala ambalo lipo kwenye nchi yenye misukosuko mingi kiusalama, maduka yanafanya kazi karibu saa 24. Sisi Kariakoo ambako ndiko kwenye roho ya biashara nyingi za nchi hii, kunafungwa saa 11 jioni! Hili si jambo jema.

Wafanyabiashara kutoka mikoani ambao wangependa kufika Kariakoo kuchukua bidhaa kwao hilo lingewezekana kama wangekuwa na usafiri wa uhakika wa usiku, pia kukawapo maduka mengi makubwa yanayofunguliwa kwa muda mrefu zaidi.

Hatuwezi kupata maendeleo kama tunatumia saa 12 pekee kufanya mambo ya kimaendeleo, na zile zinazobaki tuzitumie ‘kupumzika.’  Hatuna raha hiyo.

Nimewaona wajenzi wa ‘daraja la juu’ pale  Ubungo, Dar es Salaam namna kazi zao zinavyopamba moto usiku wa manane. Ndugu zetu Wachina muda wao wa kufanya kazi ni usiku, tena usiku kucha. Hawana utitiri wa siku za mapumziko kama hapa kwetu. Karibu nusu ya siku 365 za mwaka tunazitumia kwa mapumziko ya wikiendi na sikukuu. Hizo chache zinazobaki nazo tunazitumia kwa udhuru na mambo mengine mengi – na hapo ni mbali kabisa na likizo kwa wale walioajiriwa.