UTAWALA wa Rais wa Marekani Donald Trump umetoa pendekezo la kuweka marufuku mpya ya kusafiri kuingia nchini humo itakayowaathiri raia wa mataifa kadhaa kwa viwango vinavyotofautiana.
Kulingana na gazeti la Marekani la New York Times lililowanukuu maafisa ambao hawakutajwa majina limesema pendekezo hilo linazihusisha nchi 43.
Miongoni mwa nchi hizo ambazo raia wake watazuiwa kabisa kuingia Marekani ni Afghanistan, Libya, Korea Kaskazini, Somalia, Sudan, Syria, Venezuela na Yemen. Kundi jingine ni la nchi nyingine kumi zikiwemo Belarus, Eritrea, Haiti, Pakistan, Russia Sierra Leone, na Sudan Kusini ambazo visa zao zitawekewa vikwazo vikali.
Nchi nyingine 22 zitapewa siku 60 za kushughulikia masuala yanayoipa wasiwasi wa Marekani vinginevyo zitahamishiwa kwenye makundi yaliyowekewa vizingizi vikali zaidi. Itakumbukwa pia kuwa katika muhula wake wa kwanza wa uongozi, Rais wa Marekani Donald Trump aliiamuru serikali kuainisha nchi ambazo raia wake hawapaswi kuingia nchini mwake kwa sababu za kiusalama.
