Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)imeeleza kuwa
kuwa, katika mwaka wa fedha 2024/25 kuanzia mwezi Julai hadi Februari 2025, imeshakusanya shilingi bilioni 212 huku idadi ya watalii ikifikia 830,295 ambayo inayojumuisha watalii wa nje 509,610 na watalii wa ndani 320,685.
Mwenendo huo unaonyesha mamlaka itapata watalii zaidi ya milioni moja na mapato zaidi ya lengo ambalo ilijiwekea la kukusanya shilingi bilioni 230 kwani hadi sasa katika mapato haya, imeshakusanya asilimia 92.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Dkt. Elirehema Doriye amesema hayo leo Machi 10, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mamlaka hiyo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni programu inayoratibiwa na Idara ya Habari – MAELEZO.
Ameongeza kuwa, takwimu zinaonesha kati ya Julai 2021 hadi Februari 2025, jumla ya watalii 2,916,540 wametembelea vivutio vya utalii ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na katika kipindi hicho, mapato ya shilingi bilioni 694 yamekusanywa na kuingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Kutokana na Mafanikio hayo NCAA inatarajia kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2024/25 la kukusanya shilingi bilioni 230 kwani hadi kufikia Februari 2025, tayari imeshakusanya asilimia 92 ya mapato hayo.

Dkt. Doriye amefafanua kuwa, takwimu hizo zinaonesha kuwa juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kupitia filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania zimechangia kutangaza nchi na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya utalii. Vilevile, mikakati mbalimbali ya shirika pamoja na ushirikiano kati ya sekta binafsi na mamlaka za utalii umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo.
Aidha, ameitaja mikakati mbalimbali ya mamlaka hiyo ya kutangaza utalii ikiwemo kwenye matumizi ya teknolojia ya kidijitali, ushirikiano na wadau wa utalii, kampeni za kijamii na utalii wa ndani, matumizi ya Wanahabari na Waandishi wa Habari, uanzishaji na matumizi ya matukio maalum pamoja na ununuzi wa basi jipya lenye uwezo wa kubeba abiria 40.

