NA Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Karatu
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema kwamba ipo makini kuhakikisha kuwa kila kaya inayojiandikisha kuhama kwa hiyari ndani ya hifadhi inapata nyumba katika Kijiji cha Msomera kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na kwamba hakuna mtu atakayeweza kupata nyumba kwa njia za udanganyifu.
Akizungumza katika kipindi maalum kilichorushwa na Redio Lumen ya mjini Karatu Mkoani Arusha Kaimu Meneja wa Uhusiano kwa umma wa mamlaka hiyo Bw. Hamis Dambaya amesema kuna baadhi ya watu wameanza kutafuta njia za uongo ili kupata nyumba jambo ambalo mamlaka imelibaini na kuanza kulifanyia kazi.
Amesema baadhi ya watu hao ni wale waliohama miaka mingi iliyopita ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na waliposikia kuwa serikali inatoa nyumba kwa kila kaya inayohitaji kuhama baadhi yao wameanza kutafuta njia za kupita ili waweze kupata nyumba kinyume na utaratibu.
“Kwa ujumla katika zoezi hili serikali kupitia NCAA ipo makini na kila mwananchi anayeishi ndani ya tarafa hii, hakuna mtu yoyote atakayethubutu kupata nyumba kinyume na taratibu kwani taarifa zote muhimu za wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi zipo katika mifumo sahihi”,alisema Bwana Dambaya.
Kuhusiana na taarifa kwamba baadhi ya watu wanatoka Ngorongoro na kwenda Msomera kutembea na hatimaye kutotaka kurudi Ngorongoro bwana Dambaya amewataka wananchi wanaohitaji kuhama kwa hiyari kufuata taratibu na kuhakikisha hawaendi katika Kijiji cha Msomera mpaka mchakato wa stahikli zao uwe umekamilika.
“Msomera imekuwa ni Kijiji cha mfano na mvuto kwa wakazi wa tarafa ya Ngorongoro na baadhi yao inadaiwa wanakwenda huko bila kufuata taratibu, tunawaomba wafuate taratibu na watahamishwa bila shaka yoyote kwa kulipwa stahiki zao,” alisema bwana Dambaya.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mwandamizi wa mamlaka hiyo Kassim Nyaki amesema lengo la serikali kuhamisha wananchi kwa hiyari ni kuboresha maisha yao ili kwenda sambamba na malengo ya kidunia ya kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora za kijamii.
Bwana Nyaki amesema idadi ya watu iliyopo hivi sasa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ya watu zaidi ya laki moja haiendi sambamba na ile iliyokuwepo mwaka 1959 ya watu elfu nane huku ukubwa wa eneo la hifadhi likibakia vile vile lenye ukubwa wa kilomita za mraba 8292.
“Wakati hifadhi inaanza mwaka 1959 kulikuwa na wananchi takribani 8000, mifugo isiyozidi 260,000 na wanyamapori wengi, lakini kwa sasa wananchi wameongezeka kufika zaidi ya 110,000, mifugo zaidi ya laki 8 na wanyamapori pia wameongezeka na eneo likibaki na ukubwa uleule, Vilevile mahitaji ya wananchi yameongezeka kwa kuwa wanahitaji huduma bora kama watanzania wengine, ndio maana serikali inawajengea miundombinu na huduma za kisasa nje ya hifadhi ili kuboresha Maisha yao” aliongeza Nyaki.
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, mikutano ya hadhara na kwenye makongamano ya kidini ili kuwahamisisha wananchi kuhama eneo hilo kwa hiyari.