Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetangaza utaratibu ambao utatumika kuwahoji viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika Sensa ya watu na makazi, Agosti 23, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, imesema kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atahojiwa saa 7:00 hadi saa 7:30 mchana wakati Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo atahojiwa kuanzia saa 8:00 hadi saa 8:30 mchana.
Dk. Chuwa amesema kwa msingi huo anaomba viongozi katika ngazi ya Mkoa Mwenyekiti wa CCM na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi ifanyike kama hivyo.
Aidha, katika ngazi ya wilaya pia itafanyika hivyo hivyo, huku akifafanua kuwa zoezi hilo litarekodiwa na vyombo vya habari na baadae kurushwa katika vyombo vya habari.
Pia, amesema ifahamike kuwa wakati viongozi wanahojiwa vyombo havitaruhusiwa kurekodi mazungumzo kati yao na makarani wa sensa.
Amewakumbusha Watanzania kuwa, Agosti 23, 2022, ni siku ya sensa ya watu na makazi nchini ambapo watu wote watakaolala nchini watahesabiwa na kukusanya taarifa zinazohusu umri, jinsia, uraia, simu ya kiganjani kwa watu wote wenye umri wa miaka 15 na kuendelea.
Amesema kila mwanakaya atatoa taarifa ya elimu, shughuli za kiuchumi, hali ya uzazi kwa akina mama vifo kwenye makazi wanayoishi.