Nauli za daladala nchini zinatarajia kushuka mwishoni mwa mwezi huu kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta nchini na duniani kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DRCOBOA), Sabri Mabrouk, ameiambia JAMHURI kuwa wamiliki wa daladala watakumbwa na “msiba mkubwa hivi karibuni” kutokana na msimamo wa Serikali ambayo inatarajia kushusha nauli kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta nchini na duniani kwa ujumla.
Amesema pamoja na Serikali kulazimisha ushushwaji wa nauli, imeshindwa kuangalia kwa ukaribu sekta ya usafirishaji wa abiria nchini kutokana na kukumbwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na ongezeko la bima kwa magari hayo.
Mabrouk amesema katika biashara hiyo wamekuwa wakikumbana na gharama za matengenezo ya magari huku mapato yakiwa pale pale kwa kipindi kirefu bila Serikali kuchukua hatua yoyote.
Thamani ya shilingi imeshuka nauli ikiendelea kuwa shilingi 400 katika kipindi cha miaka mitatu bila ongezeko lolote. Kupanda kwa gharama za vipuri umekuwa ni mzigo mkubwa kwao.
“Gharama za vipuri zipo juu sana, hii yote ni kutokana na kushuka kwa fedha zetu, nauli bado ni ndogo haijapanda kwa miaka mitatu, ilitakiwa iwe imepanda lakini jambo la kuumiza ambalo naliita msiba ni mkakati wa kushushwa kwa nauli kama unavyopigiwa debe hivi sasa, na tarehe 18 mwezi huu nauli inaweza kushushwa kutokana na kuwapo na kikao kitakachokaa kulingalia hilo,” amesema.
Pia amezungumzia ongezeko la asilimia 100 la kodi ya makadirio inayolipwa na wenye daladala, na kusema kuwa ongezeko hilo lilifanywa na TRA kutokana na wamiliki wa daladala nchini kuonekana kuwa wanapata fedha nyingi kutokana na biashara hiyo. Katika bajeti ya mwaka wa fedha ya 2015/2016, kodi zitaongezwa zaidi.
Mabrouk anasema Darcoboa ilikutana na Serikali kuangalia uwezekano wa kutoongezeka kwa makadirio lakini juhudi ziligonga mwamba kutokana na mapato yanayotokana na biashara hiyo.
Anasema kawaida daladala zilikuwa zinalipa makadirio kutokana na kutokuwa na kiwango halisi kinachopatikana katika biashara hiyo.
“Baada ya TRA kutopandisha makadirio hayo kwa miaka 10, lakini wanajua kabisa kuwa hapa mjini hakuna daladala ambayo mapato yake ni chini ya shilingi 70,000 kwa siku, hivyo kila mfanyabiashara hii anapata kiasi cha shilingi 200,000 kwa siku kabla ya kuondoa makato. Hivyo kutokana na kiasi hicho zinakusanywa million 60 kwa mwaka, tumeshapita mara tatu ya kiwango cha juu kabisa,” anasema Mabrouk.
Anasema wafanyabiashara ya kuuza viazi vya kungaanga (chips) wao hupata kiasi cha shilingi million 20 kwa mwaka, hivyo hao huwezi kuwalinganisha na wamiliki wa daladala jambo ambalo TRA inaliangalia kwa umakini zaidi katika kipindi hiki.
Hata hivyo, alibainisha kuwa wamefanya makubaliano ya kuongeza viwango hivyo vya kodi kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambapo mapendekezo ya muswada huo unatarajia kupelekwa bungeni katika vikao vijavyo vya Bunge.
Wakati Mabrouk akisema ongezeko litakuwa mwaka 2016/2017, tayari TRA imekwishaanza kutoza kodi hizo kwa wamiliki wa magari. Hiace zilizokuwa zinatozwa kodi ya Sh 364,000 kwa mwaka, kwa maana ya Sh 91,000 kila miezi mitatu, sasa anatozwa Sh 728,000.
DCM na Coaster wanaliokuwa wanalipa Sh 560,000 kwa sasa wanatozwa Sh milioni 1,120,000 na wengine wanakadiriwa zaidi. Maafisa wa TRA walisema viwango hivyo ni kwa mujibu wa sheria na wanalenga kurasimisha biashara katika nchi hii kwa watu wengi kuendesha biashara kama kampuni.
Wamiliki wa mabasi yanayotoa huduma za usafiri katika jiji la Dar es Salaam (daladala) wameilalamikia Serikali kwa kuwapandishia makadirio kwa asilimia 100 jambo ambalo si sahihi katika kipindi hiki cha mfumko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi.
Wakizungumza na JAMHURI baadhi ya wamiliki wa daladala walisema wameshtushwa na kiasi cha fedha walichotakiwa kulipa kwa TRA kwani kimeongezeka mara mbili zaidi ya kile cha awali, na baada ya kuuliza kwa maafisa wa mamlaka hiyo walielezwa kuwa utaratibu huo umeanza tangu mwaka wa fedha wa serikali Julai, 2014.
Mohamed Issa, mkazi wa Magomeni, alisema kawaida alikuwa analipa makadirio Sh 375,000 kwa mwaka lakini baada ya kupanda atatakiwa kulipa mara mbili zaidi ya kiasi hicho cha fedha, jambo ambalo linawaumiza wenye daladala.
Yakub Jumaa, mkazi wa Kinondoni, alieleza kuwa Serikali imeshindwa kumthamini Mtanzania mwenye kipato cha kati na chini kutokana na kufanya kila iwezalo kumkandamiza mara kwa mara.
Aliitaka Serikali kuangalia kwa mapana sekta ya usafiri na usafirishaji jijini Dar es Salaam kutokana na changamoto zilizopo, huku kiwango cha nauli kikishindwa kupandishwa kwa kipindi kirefu.