Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mgombea Mwenza wa Ngome ya Vijana, Nassor Ahmed Marhun amewaahidi vijana wa ACT Wazalendo kuwa endapo watachaguliwa wamejipanga kutafuta na kutetea ushindi wa chama chao katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Marhun ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akichukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili akiwa na Mwenyekiti wa Ngome hiyo Abdul Nondo.
“Tutasimama imara kuitetea nchi yetu na haki za vijana kwa ujumla. Na mpango kazi wetu ifikapo 2025 ni kuhakikisha ACT Wazalendo inashinda kwa kishindo kikubwa na kuongoza Serikali zote mbili, ya Muungano na Zanzibar,” amesema Marhun.
Kwa upande wake Nondo, amezungumzia utekelezaji wa vipaumbele alivyoahidi katika uongozi wake kwa kipindi kinachomalizika, ambapo amesema aliahidi kuifanya Ngome ya vijana kuwa chombo cha utetezi na kusemea masuala yote yanayohusu maslahi ya vijana nchini.
“Nimefanya kazi hiyo na viongozi wenzangu na tumeifanya Ngome kuwa sauti ya kusemea changamoto mbalimbali za vijana, ajira, uonevu, mikopo ya elimu ya juu.
“Tumefanya kazi hii kwa jasho na jitihada zetu zote na ndiyo maana Ngome ya Vijana ACT Wazalendo kuwa kimbilio la vijana nchini hasa wanapohitaji msaada wa utetezi na kusemewa, na mara nyingi sauti yetu imekuwa yenye nguvu kwa Serikali pindi tunapozungumza” amesema.