Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

SERIKALI imesema kuwa sheria ya mwaka 2016 ilitungwa ili kupunguza mikono ya Serikali kuendesha vyombo vya habari kwani sheria ya mwaka 1976 ilikuwa imeweka mikono mingi sana.

Akizungumza katika kipindi cha Televisheni cha BBC, Dira ya Dunia
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ,Nape Nnauye,amesema kuwa sehemu kubwa ya usimamizi wa vyombo vya habari ibaki kwa wanataaluma wenyewe tofauti na sheria ya habari ya mwaka 1976 ambayo iliingiza mikono mingi katika kusimamia vyombo vya habari.

“Sheria hii tukatamani ipunguze, na namna ya kupunguza ilikuwa ni pamoja na kuunda Baraza Huru la Wanahabari ili yale ya kitaaluma wayamalize huko.

“Tulipotunga sheria ya mwaka 2016, lengo lake ilikuwa ni kwamba tupunguze mikono ya serikali kuendesha vyombo vya habari Serikali iliamini kwamba ikipita njia hiyo, itakuwa imefanikiwa kupunguza madaraka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo aliyopewa na sheria yam waka 1976.

“Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), ndiye mwakilishi wa serikali katika kusimamia vyombo vya habari, tunataka madaraka yake yapungue kadri inavyowezekana,” amesema.

Amesema kuwa waandishi wa habari kama wanataaluma wengine wakiwemo wanasheria wajisimamie wenyewe, na kwa hilo inawezekana.

“Sisi kama serikali tubaki na vitu vichache sana vinavyolinda nchi, usalama na afya ya jamii.

“Lakini mengine mengi yafanywe na wanahabari wenyewe na inawezekana maana madaktari wamefanya imewezekana, wanasheria wamefanya imewezekana na wanahabari inawezekana,” amesema.