Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema katika mwaka huu wa fedha serikali itahakikisha inakamilisha mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA) ya Mwaka 2016.

Akihitimisha michango ya wabunge katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma Ijumaa, wiki iliyopita, Nape amesema: “Serikali itahakikisha inafanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 ndani ya mwaka huu wa  fedha.” Nape alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Ester Bulaya, aliyetaka kufahamu ni lini serikali itabadili sheria kandamizi za habari.

Bulaya amesema Sheria ya Huduma za Habari imeleta mfumo wa kusajili magazeti kila mwaka, kwa kukasimu madaraka hayo kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) chini ya kifungu cha 9 na 10 cha Sheria ya MSA, ambacho kimetumika vibaya katika miaka sita iliyopita. Amesema vifungu hivi vimetumika kufungia magazeti na kuyanyamazisha, suala linaloathiri uhuru wa habari.

Amesema sheria hiyo inataka waandishi kusajiliwa na kuwa na kiwango cha angalau diploma ya uandishi wa habari, suala analosema linaibemenda tasnia ya habari kwani tasnia hii kwa sasa inahitaji wataalamu wabobezi wakiwamo watu wenye taaluma mbalimbali kama wanasheria, madaktari, walimu na taaluma nyingine nyingi, hali itakayoimarisha ubora wa kazi za taaluma ya uandishi.

Nape amesema yote hayo yanayolalamikiwa yatabadilishwa katika mchakato wa kubadili sheria unaoendelea likiwamo la mafao ya waandishi wa habari. Ameongeza kuwa nia ya kuanzisha diploma ya uandishi kwa wanahabari, wazo hilo lililenga kuboresha na kuimarisha taaluma ya habari badala ya kuruhusu kila anayejua kusoma na kuandika kujitambulisha kama mwandishi.

Mbunge wa Msalala (CCM), Kassim Idd, ameitaka serikali iangalie masilahi ya waandishi wa habari kwani wanafanya kazi ngumu ila malipo yao ni kidogo. Mbunge wa Kishapu (CCM), Boniphace Butondo, ametaka kubadilishwa kwa muundo na kuruhusu watendaji waliosomea uandishi katika halmashauri za wilaya kuruhusiwa kuwa wasemaji wa halmashauri badala ya wakurugenzi kuendelea kuwa wasemaji.

Katika bajeti ya wizara, Nape ameeleza nia ya serikali kuanzisha Baraza la Ithibati, Baraza Huru la Vyombo vya Habari na Mfuko wa Mafunzo. Wabunge wengi walizungumzia upatikanaji wa mawasiliano ya simu za mkononi kutokuwa mzuri katika baadhi ya maeneo nchini kwa kutokuwapo minara ya simu, zikiwamo kata nane za Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, ambazo ni Nyanga, Kibeta, Kagondo, Kahororo, Buhembe, Nshambya, Ijuganyondo na Kitendaguro. Serikali imeahidi maboresho.

Wadau wa habari wamesema malipo kwa waandishi wa habari yataimarika ikiwa serikali na taasisi zake zitalipa madeni yake kwa vyombo vya habari, likiwamo deni la Daily News ambayo ni kampuni ya serikali, ambalo Waziri Nape amesema bungeni kuwa limefikia Sh bilioni 11. Kwa ujumla vyombo vya habari vinadai karibu Sh bilioni 20 katika wizara, taasisi na mashirika ya umma.