Nani anaharibu nchi yetu?
Naikumbuka siku uliyofariki Mwalimu. Nilikuwa mdogo, mwanafunzi pale Sekondari ya Baptist. Siku uliyofariki Baba wa Taifa letu, na siku kadhaa zilizofuata, kulijaa utulivu wa hali ya juu, lakini utulivu huo haukudumu maana palianza kusikika vilio vya hapa na pale.
Kilio kikuu ni itakuwaje kuanzia sasa? Mheshimiwa Rais alitangaza kwa sauti iliyojaa kitetemeshi pale alipotangaza msiba wa Taifa. Utulivu ulikuwa ni wa kutafakari, watu wote walijiona yatima, kelele na vilio vilikuwa ni vya uchungu, wakimililia baba yao. Nikiikumbuka siku hiyo na siku zilizofuata baada ya hapo hadi Baba wa Taifa hili ulipozikwa, najiuliza swali la msingi lifuatalo:
“HIVI WEWE BABA WA TAIFA UMEONDOKA NA UMOJA WAKO, AMANI YAKO, UPENDO WAKO NA TANZANIA YAKO NDANI YA KITABU CHAKO CHA ‘AZIMIO LA ARUSHA’?”
Naomba nikuulize Baba maana huku ulipotuacha sidhani kama kuna majibu ya kuniridhisha, naona mipira ikirushwa hewani, watoto wako wakipigana vita na vijambe kwa kile ambacho kilikuwa hadithi hapa nchini. Eti tumeanza kupigana mabomu!
Nikuulize wewe kwani sioni wa kumuuliza na naogopa kuuliza maana nikiuliza sidhani kama nitaweza kupata jibu sahihi; zitapigwa kelele na kila mmoja atazungumza lake na mwisho nikiwa nimesimama katikati sitapata majibu. Siwezi kuyapata hayo majibu Baba zaidi ya kuchanganyikiwa.
Nikimuuliza Chadema yeye anaweza kusema ni CCM, tena anaweza kutoa ushahidi ambao naweza kubabaika kuukataa. Naye CCM ukimuuliza anaweza kumrushia mpira Chadema na akatengeneza hoja ambayo itazua mijadala lukuki na tusielewane. CUF, NCCR-Mageuzi na TLP wanaweza kusema sisi, hatumo!
Labda tuseme ni huyu mwanao mkubwa, CCM. Yeye ana mamlaka, ambayo ameyakamata na kuyarithi kutoka kwako, sasa labda tuseme anatishwa na huyu mdogo wake, ambaye ameonekana msumbufu kweliweli.
Swali langu: Je, ni kweli kabisa huyu mwenye mamlaka afanye kosa au mashambulizi ambayo mwishowe ushahidi utamlenga yeye mwenyewe? Kisa tu anataka awatishe wananchi kuonesha kuwa huyu mdogo analeta vurugu? Au kuna mtu mwenye kutumia mbinu zake kwa kutumia jina lake kwa kuharibu jina la CCM?
Hivi utakuwa ni utoto wa aina gani kufanya uvamizi wa kijambazi na uache viashiria vya kurudi kwako mwenyewe? Kama ni kweli basi utakuwa ni utoto wa hali ya juu. Lakini kama si huyu, atakuwa nani basi?
Baba, labda tuseme ni huyu mwanao mdogo anatafuta mbinu za kujipa umaarufu na kuonewa huruma ili apendwe na wafuasi wengi. Labda tuseme anajenga umaarufu huo ili athibitishe kuwa kaka yake ni mdhaifu ambaye hawezi kuongoza nchi.
Lakini inawezekana kweli bila kuwa na shaka hata kidogo wala ghiliba kuwa huyu afanye mashambulizi ndani ya nyumba yake mwenyewe? Kweli kabisa atoke ajirushie bomu mwenyewe na yeye akiwa humo humo ndani? Kabisa, huyu mwenye kusaka mamlaka ya umma aubomoe huu umma ambao yeye ana ndoto ya kuuongoza. Haiwezekani hata kidogo kwa mtoto huyu mwenye ndoto kubwa hivi ajidhuru ili atafute umaarufu tu. Sidhani Baba, nakwambia sidhani.
Baba, mbona matukio haya yanatisha, padri kauwa, makanisa yamechomwa, kanisa limelipuliwa kwa bomu, waandishi wametekwa na kuuawa. Mbona Baba yetu Mwalimu, haya matukio kama yanafanana? Tena ufanano wao ni uleule wa kutenda na kutokomea, na ukweli halisi hauonekani.
Baba, au kuna kamtandao ambako kameona udhaifu wa watoto wako wote wawili na wameamua kutengeneza mtandao ambao utawavuruga hawa wote wawili ili wao na ajenda zao za siri ziweze kufanikishwa. Inawezekana kabisa kukawa na mtandao ambao kwa kutambua udhaifu wa pande zote mbili pamoja na vyombo vya habari basi wakawachonganisha ili kuvuruga kabisa msimamo wa kitaifa.
Lakini kama kamtandao hako kapo, basi na wao ni wapuuzi maana akili wanayoifanya ni upuuzi mtupu, yaani anataka kuchonganisha kila idara, achonganishe dini zipigane, waumini wakipigana na huku kwenye siasa nako wakapigana patakuwa na vurugu na ajenda yao isiyofahamika inaweza kugundulika.
Tatizo Baba yangu, kama mtandao huu upo, utakuwa umeenea kiasi gani na chanzo chake kitakuwa wapi? Nani mkuu wa mtandao huo, yuko ndani au nje ya nchi? Ajenda yake ni ipi?
Natamani mzee Elvis Musiba angekuwapo au Ben R. Mtobwa angekuwapo – niwaulize kama wao wangekuwa wanatunga hadithi hii, Joram Kiango na Willy Gamba wangeanzia wapi kutanzua vifundo vya matukio haya?
Nasikia Shafi yupo, labda atafutwe atuambie, maana najua vijana wenzangu kwake si ngumu kama wasingeweza kutatua labda Hussein tu wanaweza kujitahidi kidogo.
Cha msingi Baba yangu, huyu anaweza kuwa anayafanya haya akiwa na uhakika kabisa hawezi kukamatwa na akawa amepenya kila idara, yaani akawa amejaa tele nyumbani kwa Chadema, akawa anapepea CCM na kuambaaambaa katika viunga vya serikali, sasa akabaki kuwazungusha vichwa wote – CCM, Chadema pamoja na watendaji wa serikali, huku vyombo vya habari vikibakia mashabiki wasioelewa kitu.
Baba, hebu tupatie utashi wa mambo haya hata kama tulikuwa wabishi tusiosikia na hata kama tulikukwaza, maana ungekuwa katika nchi nyingine zenye kuamini vyema mababu zao kama India, basi ungewambwa katika sehemu za ibada na wangekuomba mchana na usiku ili uwapatie baraka na hekima.
Nimekuuliza maswali haya kabla sijaulizwa na wanafunzi wangu, lakini shaka ni kwamba sijui kama haya yalishawahi kukukuta, yaani ukajiuliza maswali unayoweza kuulizwa na hata kabla hujaulizwa ukawa huna majibu.
Mungu ailaze roho yako Mahali Pema Peponi, Amina. Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki Watanzania.
0767 260325