Mpita Njia (MN) ni miongoni mwa wale wanaoamini kuwa utandawazi maana yake si kuachia kila kitu kijiendeshe kienyeji.
Anajiuliza, mbona huko ulikozaliwa huo utandawazi kuna mambo mengi yamepigwa kufuli? Mbona huku kwetu kila jambo – lililo baya au lililo jema- linaachiwa tu?
MN amefikia hatua hiyo baada ya kuona hizi nyumba zenye kuendesha michezo ya ‘kubeti’ zinavyoongezeka. Anashangaa kuona Serikali ikiwa imefumba macho kabisa kana kwamba hili la ‘kubeti’ si janga la kitaifa.
Juzi alikuwa Kongwa mkoani Dodoma. Hapo akashuhudia makumi kwa makumi ya vijana wakiwa kwenye mashine za kamari. Hawana kazi nyingine sasa, isipokuwa kushinda na kukesha kwenye mashine za kamari.
Akaendelea na safari hadi mkoani Mara. Akafika kijijini Butiama akilenga kujionea mahali alipozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Akiwa na mwenyeji wake, ukaibuka mjadala ambao chanzo chake ni vijana kuwa wavivu tofauti kabisa na alivyokuwa Mwalimu Nyerere. Mwalimu alipenda kufanya kazi. Alishinda shambani.
MN akaambiwa shida ya Butiama sasa ni mashine za kamari zilizopelekwa na Wachina. Kweli, hazikupita dakika 10, likaonekana gari alilokuwamo raia wa China aliyefika kijijini Butiama kukusanya fedha kutoka kwenye mashine za kamari.
MN akaambiwa siku hizi hata wale vijana waliokuwa mafundi pikipiki wameacha kazi hiyo. Wanashinda na kukesha kwenye vibanda vyenye mashine zinazosambazwa na Wachina. Nguvukazi imepungua.
Akaambiwa yaliyoko Butiama yako pia katika vijiji vingi mkoani Mara na Kanda ya Ziwa kwa jumla. MN akaona hili si jambo la kunyamazia. Kama Serikali ilipiga marufuku michezo ya ‘pool’ saa za kazi, inashindwa nini kudhibiti mashine hizi na pia nyumba za ‘kubeti’?
Bado anajiuliza, nani aliyekaribisha balaa hili ambalo tunaambiwa walimu nao wameanza kulalamika kwa sababu vi-toto haviingii madarasani kwa sababu ya kamari.
MN anauliza, kama kuifuta au kuizuia michezo hii ni kazi ngumu, kwanini kusiwekwe utaratibu maalumu wa kuidhibiti ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho? Kubwa zaidi, nani anayewapa Wachina hawa na Watanzania vibali vya kuendesha michezo hii ya kubahatisha bila uratibu?
MN anadhani muda si mrefu Watanzania wanaweza kubaini kuwa athari za dawa za kulevya zimepungua, lakini madhara makubwa yakawa kwenye hizi kamari za kisasa.