Uamuzi wa Rais John Magufuli, wa kuwataka Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na Wakili Mkuu wa Serikali (SG) kupitia kesi za watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji ili kuwaachia huru walio tayari kurejesha fedha, umepokewa kwa shangwe kubwa nchini.

Chumba cha habari cha JAMHURI kimepokea simu kutoka kwa watu mbalimbali nchini, hasa wenye ndugu na jamaa wanaoteseka magerezani, wakipongeza uamuzi wa huruma wa Rais Magufuli.

Juzi Jumapili, Rais Magufuli, akizungumza wakati wa kuwaapisha viongozi kadhaa Ikulu jijini Dar es Salaam, alirejea kauli yake ya kutotaka kutawala nchi yenye watu wanaolia. Baadhi ya watu maarufu walioko rumande orodha yao iko mwishoni mwa habari hii.

Ifuatayo ni hotuba ya Rais Magufuli, neno kwa neno kama alivyozungumza Septemba 22, 2019.

Nafahamu kwa Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General) yuko hapa, Mkurugenzi wa Mashitaka pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria mko hapa. Mimi naumia sana, na hili nataka niliseme kwa wazi – kuona watu wako mahabusu au watu wamefungwa ni bahati mbaya kwa sababu sheria zipo.

Lakini mtu anapowekwa mahabusu wakati mwingine miaka mitatu hadi minne huwa inaniumiza sana. Nilishasema kwamba sipendi kuongoza watu wakiwa wanatoa machozi, ni bahati mbaya wakati mwingine si uwezo wangu, lakini kama uwezo huo ningekuwa nimeupata na Mungu akanisaidia ikatokea siku moja hakuna mfungwa, hakuna mahabusu, hakuna nani – ningefurahi kweli ili kusudi hawa askari magereza na kamishna akafanye kazi nyingine.

Juzi kaniandikia barua anaomba niajiri maaskari magereza wengine. Anaomba askari magereza 800. Wala sikumjibu, kwa hiyo yeye anataka niongeze wafungwa kule kusudi – na ukweli ni kwamba sikupi sitaajiri hao. Siwezi. Huwezi mtu kufikiri tu kuongeza watu ili kusudi wafungwe, mimi nataka wafungwa wapungue ili hao wafungwa na mahabusu waje tushirikiane nao katika kazi ya maendelo ya kuijenga Tanzania yetu.

Sasa kwa sababu DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka) uko hapa na umekuwa ukifanya kazi nzuri; mimi nikuombe pamoja na solicitor general na wengine mnaohusika na sheria, wapo watu wamekaa ndani kwa kesi za uhujumu uchumi wengine wana miaka mitatu na kadhalika. Ninawahurumia sana kama ambavyo nawahurumia wengine.

Lakini inawezekana wapo waliokaa ndani ambao wako tayari kuomba msamaha, kwamba mimi nilichukua hizi hela milioni 2,000 (Sh bilioni 2) nikawadhulumu hawa akina mama kwa ajili ya madawa [dawa] yao, nikadhulumu kwa ajili ya elimu, nikadhulumu pesa hizi kwa ajili ya kujengea barabara, kununua ndege, kusomesha watoto bure, ninakiri na niko tayari kuzirudisha.

Kwamba ninakiri nilidhulumu katika kulipa kodi nika-forge (nikagushi) sikulipia kodi kitu hiki… wao wanajua katika dhamira zao, sasa kama wapo watu wa namna hiyo nisije nikahesabika nimeingilia Mahakama, ninashauri kwa DPP mkawasikilize angalau katika kipindi cha siku saba, kuanzia Jumatatu hadi siku ya Jumamosi ya wiki inayokuja (Septemba 23 hadi Septemba 28, 2019) kama wapo watu wa namna hiyo ambao wapo mahabusu kwa sababu ya kesi za uhujumu uchumi ambazo hazitawafanya watoke mapema kwa mujibu wa sheria yetu, lakini wako radhi kurudisha zile fedha na kutubu kwamba wako radhi na hawatarudia, mimi ningeshauri watu wa namna hiyo kama sheria inaruhusu DPP wakatoke humo ndani.

Ukatengeneze mazingira ya wao kurudisha hizo hela walizozichukua kwa ajili ya watumishi hawa na wananchi wanyonge. Ninajua wanateseka. Wapo watu kule wanateseka, ninawaona wanavyopelekwa mahakamani. Wengine wamekonda kweli, inatia huruma, inaumiza. Lakini inawezekana wapo wale ambao wangependa kuomba msamaha waje kwako wewe DPP usimamie hilo mpange namna watakavyorudisha hizo fedha. Warudishe ili waje washiriki katika kuijenga nchi yetu kwa pamoja.

Unamkuta mwingine alishindwa kulipa kodi akagushi, unakuta labda anadaiwa Sh bilioni 2, si aje aombe msamaha kwamba sitarudia tena, alipe hizo fedha halafu kama ana kiwanda aje aendelea kuendesha hicho kiwanda. Wapo wengine walikuwa na fedha za kutakatisha atubu kwamba sitatakatisha tena- kutakata kwangu hapana – nitakuwa natakata katika kufanya bishara ya kweli, kwamba dhambi ya kutakata nimeiacha – aje atoke huko alipe hiyo hela anayodaiwa. Mimi nafikiri ninyi wanasheria mnajua hata mimi natakiwa kutoa mapendekezo. Haya ni mapendekezo. Kwa sababu watu wa Mahakama saa nyingine wanapenda kuwasulubu watu, lakini mimi haya kama kiongozi ninapendekeza hivyo, ningefurahi hivyo.

Nimekuwa nikisikia watu wakishikwa na dhahabu, anakwenda anatubu na dhahabu inataifishwa na anaendelea anakwenda kuchimba nyingine. Nimesikia kwenye Mahakama Mahakama sasa katika hizi nyingine mtu anaweza kutubu na kurudisha fedha aliyotakatisha ili tukaitumie kwa ajili ya wananchi maskini, ikalipie ada za watoto, ikajenge mahospitali, ikanunulie madawa [dawa] ya watu wetu masikini na kadhalika. Lakini aseme kwamba hatarudia, lakini wasipofanya hivyo ndani ya siku saba, ninyi muendelee kuwabana kisawasawa. Nimeona haya ndugu zangu niyazungumze kwa sababu mengine yanatia uchungu.

 

Kutumbuliwa viongozi Morogoro

Nilikuwa najaribu kufiria nizungumze nini hapa, acha nianze na maneno ya kuwapongeza sana mliochaguliwa. Lakini niseme kiukweli kabisa kazi ya kuteua na kutengua ni ngumu sana; na kama kuna kazi ambayo huwa inanipa shida sana, basi ni ile ya mtu unamteua halafu baadaye unamtengua.

Ni kazi ambayo ina machungu ila saa nyingine inabidi mtu ufanye. Mheshimiwa Makamu wa Rais [Samia Suluhu Hassan] amezungumza kuhusu Morogoro na nishukuru aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro [Steven Kebwe] yuko hapa, lakini ukweli bila unafiki kama kuna mkoa uliotusumbua sana katika kuongoza ni Mkoa wa Morogoro. Mambo mengi yalikuwa hayaendi, nisipolisema hili nitakuwa mnafiki na mimi sitaki kuwa mnafiki.

Ukienda kwenye halmashauri matumizi ya fedha ni hovyo. Nilimtuma Mheshimiwa Suleiman Jaffo akatembelea halmashauri zile yeye kama Waziri wa TAMISEMI, akakuta mambo ya hovyo, vituo vya afya tumepeleka fedha kule haviishi, lakini fedha zipo. Migogoro hiyo ya ardhi iko kila mahali kuna wawekezaji pale wa tumbaku nao wanataka kukimbia na kiwanda chao. Kila unapogusa ni hovyo tukaanza kutoa, kwa mfano wakurugenzi – tulimtengua wa Malinyi, tukafikiri tumetibu – hamna.

Tukaenda wa Halmashauri ya Morogoro Vijijini nafikiri na Ulanga, yupo Mkurugenzi ambaye amewahi kununua madawa [dawa] ya mchwa ya Sh milioni 66, anajenga kituo cha afya, lakini madawa [dawa] ya kuua mchwa kwenye eneo lile ni Sh milioni 66 na akanunua ya Sh milioni 1.8 na madawa [dawa] yote hayakutumika; yakatumika robo tu and he don’t care (wala hakujali).

Aliyekuwa Katibu Tawala wa pale [Morogoro] nilimwambia Katibu Mkuu Kiongozi astaafu mapema. Yeye kazi yake ni kupanga walimu wa shule za sekondari pamoja na zile za msingi. Anawatoa vijijini na kuwaleta mjini wanaozungumza naye vizuri. Sasa ukishajiuliza mkoa na una Mkuu wa Mkoa yuko pale unajuaautomatically kwamba Mkuu wa Mkoa ameshindwa kuhimili mkoa wake. Ukishapewa mahali na umeaminika kwa Watanzania wote halafu hakuna kinachofanyika, walioko chini yako wanafanya mambo ya hovyo maana yake wewe hutoshi.

Ukishaona mkuu wa wilaya na mkurugenzi wanagombana na wanachogombania ni maslahi, mkuu wa mkoa hujawahi hata kukemea, hata kuchukua hatua maana yake hutoshi. Na ndiyo maana kwa upendo mkubwa sana Dk. Kebwe mimi nampenda sana ni daktari kwa taaluma, lakini kwenye uongozi wa mkoa ulimshinda. Kila mahali unazungumza na sehemu nyingine unazungumza kwa parables Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa shughulikia hili, naye anajibu nitashughulikia mzee na ndiyo maana tukasema hapana. Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) amekwenda kule ananiambia mzee huku ni shida.

Sasa nazungumza hili kwa mfano tu kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, haiwezekani watendaji wote walioko chini yako wana-underperform na wewe uko hapo juu ujisifu kwamba wewe ni mkuu wa mkoa haiwezekani. Haiwezekani ukawa waziri na watu walioko chini yako hawa-perform na ukajiita wewe ni waziri; ndiyo maana tukasema ngoja tubadilishe uongozi wa mkoa huo na nikasema ngoja nimpeleke huyu aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha (Loata Sanare).

Najua ninampeleka mahala penye changamoto na huu ni mtego mkubwa kama alivyozungumza Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa sababu wafugaji kule anawajua ni watu gani. Inawezekana labda na yeye akawa mfugaji kule sasa nimempeleka huko huko akatatue matatizo ya wafugaji kulishia mifugo kwenye mashamba ya wakulima na wakulima kwenda kulima kwenye maeneo ya wafugaji. Kwa hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa una changamoto kubwa, lakini nataka ukaitatue – lakini ukatatue pia migogoro katika halmashauri maana baadhi ya wakurugenzi watendaji katika Mkoa wa Morogoro huwa wanachangishana fedha za kuleta makao makuu na ndiyo maana miradi haiendi.

Unapeleka fedha Sh bilioni 1.3 za kujenga hospitali ya wilaya inakaa miezi sita hata jengo halijaanza kujengwa. Tunawanyima haki wananchi maskini ambao hizo fedha ni kodi zao kwa hiyo ndiyo maana tumechukua hatua hii; na ndio maana tunasema mtaona wote wateuliwa hawa kila mmoja alikuwa mahali Fulani, siyo wapya – ni kama kuwahamisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Ndugu Kalobero – sina hakika kama wengi wanafahamu, kwamba Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji kama wapo waliowahi kumsikia ni wachache. Ninasema ukweli sijawahi kusikia amekaa hata na makandarasi. Sijawahi kusikia amesimamisha hata kandarasi kule au wapi. Kalobero alikuwepo pale tu ametulia analoa kwenye wizara, nasema ukweli bila unafiki. [Kalobero ni jina la Kizinza lenye maana ya kuloa samaki].

Ni mhandisi kwa taaluma ana shahada ya pili, amesomea mpaka Uholanzi, lakini alishindwa kukemea pale, ndiyo maana tukasema ngoja tumpeleke Morogoro. Amewahi kuwa mhandisi pale kabla hajapata promotion ya kupelekwa Mwanza na baadaye Babati na baadaye akawa Katibu Tawala Katavi.

Tumemrudisha kwenye mkoa anaoujua akatumie taaluma yake, ni hatua nyingine ya kwenda  Morogoro kwa sababu alipokuwa mhandisi pale alifanya kazi nzuri. Alipokuwa Mkurugenzi Mwanza alifanya kazi nzuri. Alipokuja Wizara ya Maji kama Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji hakuna. Ndiyo maana tumemchukua huyo [Anthony] Sanga Mhandisi wa Maji Kanda ya Ziwa – amefufua miradi yote ya maji, ulizeni hata watu wa kawaida.

Katika Wizara ya Maji mtu ambaye amefanya vizuri kwa wakurugenzi wote kwenye miradi ya maji ni huyu Sanga, ndiyo maana nikasema ngoja aje hapa kwenye Wizara ya Maji – aliyoyafanya kule Kanda ya Ziwa ayafumue hapo sasa akija akalala tena hapo ndipo “atasangalila”. Unajua ndugu zangu lazima tuambizane ukweli maana sisi tuko hapa hizi ni kazi za watu -ni watumishi wa watu hasa watu masikini. Hatupeani kazi kwa kufurahiana wala kwa sherehe.

Huyu Tixon Nzunda amekuwa Naibu Katibu Mkuu tangu enzi za Mzee Jakaya Kikwete. Nafikiri ndiye Naibu Katibu Mkuu aliyekaa kwa muda mrefu. Amefanya kazi kidogo na baadaye tukampeleka Rukwa, Sumbawanga kuwa Katibu Tawala akachapa kazi vizuri tukam-promote na kumleta TAMISEMI. Akiwa hapo amesimamia ujenzi wa shule. Amesimamia Sh bilioni 23 zinazotolewa kila mwezi na amezunguka kila mahali mpaka wakamchukia. Wametengeneza majungu wee, tukasema haya akayasimamie vizuri kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, tukam-promote awe Katibu Mkuu. Ndugu zangu, najitahidi kuzungumza bila unafiki kwa hiyo ndugu Posi Ally [aliyekuwa Naibu Wakili wa Serikali] amejitahidi, amefanya kazi yake vizuri tukaona ngoja tumuongeze awe Naibu Katibu Mkuu aka-promote kule na michezo ya ndugu zetu walemavu.

Wakili wa Serikali

Ndugu Malata [Gabriel], kama alivyosema Jaji Mkuu [Profesa Ibrahim Juma] ni mwanasheria mzuri sana, amesaidia sana Serikali kushinda kesi na baadhi ya kesi ambazo aliacha tumeshinda alivyotoka tumeshindwa; alisimamia kwa uadilifu mkubwa. Tumempeleka pale Wizara ya Kazi kama Kamishna kila mmoja alikuwa analalamika kwamba hatupati vibali, ukiona mtu hadi wazungu wanalalamika ujue huyu ndiye mwenyewe, na ndiyo maana najiuliza nitampataje Kamishna mwingine wa Kazi ambaye ni tough kama huyu.

Vibali vilikuwa vinatolewa tu, lakini pia kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali huko tulikuwa tunahitaji mtu mwenye uzoefu wa kutosha ili kesi nyingine zilizofunguliwa hata miaka mitano iliyopita ili awe anazijua. Ilibidi nimtume Afrika Kusini yeye ni Kamishna wa Kazi, lakini nikampeleka Afrika Kusini kwa sababu ile kesi anaijua na utapeli wote aliujua na wakati wa kuifufua ile kesi alizuiliwa na mabosi wake.

Inawezekana walipomuona Afrika Kusini walishangaa kwamba mbona yuko huku, na alikwenda na taarifa na nyaraka zote zilizokuwepo za utapeli uliokuwa unafanywa. Mengine siwezi nikayazungumza sana. Kwa sababu ilibidi tufanye kazi kubwa na tukasema huyu arudi pale kwa sababu walikuwa wanapelekwa vijana wadogo wadogo hawana uzoefu wametoka wilayani kule wanakwenda kusimamia kesi kubwa.

Kwa hiyo ndugu zangu kazi ya kuteua na kutengua ni ngumu sana, changamoto ni nyingi katika kuongoza hii nchi.

Makonda ashughulikiwa

Juzi juzi nilikuwa kwenye ziara ya Dar es Salaam,  Mkuu wa Mkoa yuko hapa mambo ya hovyo yanafanyika. Nimekwenda kwenye kiwanda cha machinjio jengo la ghorofa moja linajengwa kwa Sh bilioni 14, na nimeenda pale nimekuta watu watatu hivi ama wanne, huwezi kuamini kama kuna viongozi katika mkoa huu.

Baada ya kuzungumza pale siku moja baadaye nikaona Meya (Kinondoni-Benjamin Sitta) anakwenda kumkabidhi kandarasi eneo la mradi; ni mambo ya ajabu tu. Wewe meya ukakabidhi eneo la kandarasi ni wapi na wapi? Lakini eneo la mradi linalokwenda kukabidhiwa kwa gharama ya Sh bilioni 14 maswali ni mengi mno ya kujiuliza. Kandarasi mwenyewe ndiye aliyejenga soko la Mwanjelwa (Mbeya) akashindwa, ana mradi mwingine tena hajaukamilisha – amekwenda anapelekwa Coco Beach, lakini kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira huwezi kujenga majengo makubwa ndani ya mita 60 kutoka bahari au ziwa.

Lakini cha kushangaza zaidi mradi mahala alipokabidhiwa mkandarasi kuna mradi mwingine wa Daraja la Selander ambapo kuna barabara nne, kuna dual carriage wayambayo inatoka huku Hospitali ya Aga Khan na ninyi mmeshaanza kuiona, itapita juu ya daraja inaenda mpaka Coco Beach na kibao kipo – sasa unajiuliza hii miradi yote ni ya Serikali huu mradi mkubwa ambao tumelipa takribani Sh bilioni 200 utapita wapi?

 

Mtazamo kuhusu sheria

Julai, mwaka huu, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, alipendekeza kufanyike marekebisho ya sheria yatakayoruhusu watuhumiwa wa makosa yote yakiwamo ya mauaji na uhujumu uchumi kupewa dhamana ili kupunguza msongamano magerezani.

Kauli yake ilikuja siku chache baada ya Rais John Magufuli alipotembelea Gereza la Butimba jijini Mwanza na kukuta idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu, na kusema baadhi wamebambikiwa kesi huku wengine wakiwa na kesi ndogondogo.

Agosti, mwaka jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, aliliambia Bunge kuwa magerezani kuna zaidi ya wafungwa 40,000 wakati uwezo wake ni wafungwa 30,000.

Profesa Juma akizungumza wakati wa mahafali ya 60 ya mawakili wapya katika Shule ya Sheria, Dar es Salaam, alisema ikiwa mahakama itaachiwa haki ya kusimamia dhamana kwa kuifanya sheria isizuie dhamana kwa baadhi ya makosa kama ilivyo nchini Kenya, itasaidia kuondoa msongamano magerezani.

“Sisi mahakama tuna mapendekezo ya kutoa, kwanza tuwe kama Kenya, makosa yote yapewe dhamana, makosa yote mahakama iachiwe haki ya kusimamia dhamana, yaani sheria isifunge dhamana, hatutakuwa na hilo tatizo.

“Kenya hata kesi za mauaji mahakama inatoa dhamana, nadhani mnafuatilia na kuona inawezekana kabisa. Vilevile masharti ya dhamana inabidi tuyalegeze, kwa mfano sasa hivi wananchi wengi wana vitambulisho vya taifa, kwanini visitumike kama dhamana bila kumtaka mwananchi aoneshe mali?” Alihoji Profesa Juma.

Tangu aingie madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli ameongoza mapambano dhidi ya rushwa, kwa kuhakikisha watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha wanafikishwa mahakamani.

Baadhi ya watu maarufu wako mahabusu wakishitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha. Baadhi ya watu hao maarufu ni:

Harry Kitilya

Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (EGMA), Harry Kitilya na waliokuwa maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Sumari wako rumande wakituhumiwa kutakatisha fedha.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola milioni 550 za Marekani kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Chartered Uingereza.

Wanadaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia dola milioni sita za Marekani, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya EGMA (T) Ltd.

Wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha dola milioni sita za Marekani katika akaunti tofauti tofauti za benki.

Rugemalira na Sethi

Mfanyabiashara Harbinder Sethi na James  Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi na matano ya kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh 309,461,300,158.27.

Kesi hiyo ipo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu Kisutu. Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia serikali hasara na kutakatisha fedha.

Katika shtaka la kwanza, Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL), na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Pan-African Power Solutions (PAP), wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Kwa upande wa shtaka la tatu, Sethi anadaiwa  kuwa  Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio, Ilala jijini Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu Na. 887 Mtaa wa Mrikau, Masaki wakati akijua ni uongo.

Sethi katika shtaka la nne anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14a ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera, kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka la tano, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya  Novemba 28/29, 2011 na Januari 23, 2014 Makao Makuu ya Benki ya Stanbic, Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi la St. Joseph, kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh 309, 461,300,158.27.

Katika shtaka la sita la kusababisha hasara, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic Tawi Kuu Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya USD 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Inadaiwa kuwa Novemba 29, 2013 katika Tawi Kuu la Benki ya Stanbic Tanzania, Wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua BoT dola 22,198,544.60 za Marekani wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Malinzi, Aveva

Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, pamoja na Katibu wake, Mwesiga Celestine, wanakabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha.

Kati ya mashtaka hayo, Malinzi pekee anakabiliwa na mashtaka 22 ya kughushi risiti mbalimbali zinazoonyesha kuwa aliikopesha TFF fedha kwa nyakati tofauti.

Mashtaka mengine yanawahusu Selestine na Nsinde Mwanga, huku shtaka moja likiwahusu wote.

Pia, aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evance  Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange (Kaburu), nao wanatuhumiwa kwa makosa matano likiwamo la kughushi nyaraka na kutakatisha fedha.

Aveva na Nyange wanakabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha, dola 300,000 za Marekani.

 

Hanspope

Takukuru imetangaza donge la fedha kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hanspope.

Mbali na Hanspope, Mkurugenzi Mtendaji na mmiliki wa Kampuni ya Ranky Infrasture and Engineering, Franklin Lauwo, naye ametakiwa kujisalimisha Takukuru ili ahojiwe.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbung’o, aliwambia waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa Hanspope kwa kushirikiana na washtakiwa wengine – Evans Aveva na Geofrey Nyange – walitoa maelezo ya uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu ununuzi wa nyasi bandia.

Inadaiwa kwamba washtakiwa walisema uongo kuwa walinunua nyasi bandia kutoka kwa Kampuni ya Ninah Guangzhou Trading kwa dola 40,577 za Marekani (Sh milioni 92.5); na kwamba ukweli ni kuwa walinunua kwa dola 109,499 za Marekani (Sh milioni 249.6).

Lauwo anakabiliwa na kosa la kufanya biashara ya ukandarasi bila kusajiliwa kwenye Bodi ya Makandarasi nchini. Inadaiwa kuwa alijenga Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Simba uliopo Bunju, Manispaa ya Kinondoni na kulipwa Sh milioni 249.9.

Hanspope ambaye anadaiwa kuwa na hati tatu za kusafiria, aliondoka nchini Aprili, mwaka huu kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga kwa kutumia hati ya kusafiria ya Afrika Mashariki.

Robert Kisena

Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena (46) na wenzake wanne wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wiki iliyopita, Wakili wa Serikali alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Rwizile aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana dhamana kisheria.

Mbali na Kisena washitakiwa wengine ni mkewe Kisena, Florencia Membe; Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na raia wa China, Cheni Shi (32) ambao kwa pamoja wanawakilishwa na Wakili Nehemia Nkoko. Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 19 ikiwemo kusababisha hasara kwa UDART ya Sh bilioni 2.41.

Katika mashitaka hayo yapo ya kuongoza genge la uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa, wizi wa mafuta na utakatishaji fedha wa Sh bilioni 1.2, kughushi na kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.4.

Isack Mollel

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii ya Otterlo Business Corporation (OBC) inayofanya shughuli zake Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha Isack Mollel (59), kupitia OBC akakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi.

OBC inadaiwa kuingiza nchini magari bila kuyalipia ushuru. Mollel amewekwa rumande tangu Februari, mwaka huu lakini kabla ya hapo alishikiliwa Takukuru kwa wiki zaidi ya mbili.

Akisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Osward Tibabyekomya akisaidiwa na Materius Marandu na Dismas Mwigunyiza mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, OBC inadaiwa kukwepa kodi ya Sh bilioni 2.8.

Hata hivyo, tangu wakati huo kesi hiyo imekuwa ikitajwa, lakini baada ya Takukuru, nje ya Mahakama, waliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema kampuni hiyo inadaiwa Sh bilioni 12.6. Lakini kabla ya hapo, taarifa zilisema OBC walikuwa wanatakiwa walipe Sh bilioni 8.6; jambo ambalo kampuni hiyo imekuwa ikihoji kwa maelezo kuwa hata kama ingekuwa ni ununuzi wa magari mapya gharama zingefikia kiwango hicho.

Mmoja wa ndugu wa Mollel amenukuliwa akisema inashangaza kuona kwenye hati ya mashitaka kiwango ni Sh bilioni 2.8, lakini taarifa zisizo za kimaandishi zinasema OBC wanatakiwa kulipa Sh bilioni 8.6 na baadaye tena kiwango hicho kikapandishwa hadi Sh bilioni 12.6.

“Tukiomba ufafanuzi tunaukosa, tunauliza kiwango hicho kinachozungumza na hata kutangazwa na Takukuru kwa waandishi wa habari nje ya mahakama cha Sh bilioni 12.6 wamekipata kwa kutumia kikotoo gani? Hawana majibu. Tunawambia basi waache zilipwe Sh bilioni 8.6 hata kama hazina justification, hatupati majibu. Ndugu yetu anateseka mahabusu bila kosa.

“Kuna magari tunajua yameingizwa kwenye madai wakati yana hati zote za msamaha wa serikali na nyaraka zote zipo,” amesema.