Wiki iliyopita Kampuni ya Mwananchi ilifanya jambo la maana sana. Iliandaa mjadala muhimu sana uliohusu athari za biashara na matumizi ya mkaa nchini. Nasikitika kutoshiriki mjadala huo.

Hizi picha zinazoonekana hapa nilizipata wiki mbili zilizopita bila kujua kungekuwapo mjadala wa aina hiyo. Laiti kama ningejua, nina hakika ningepata nzuri zaidi.

Picha hizi ni tone ndani ya bahari. Wote hawa wanaoonekana hapa ni wachuuzi wa mkaa niliowaona katika Barabara ya Morogoro;  eneo la Kibaha kuelekea Chalinze.

Kwa mpenda mazingira, hali hii ni chukizo kubwa. Bahati mbaya maafa haya ya kimazingira yanafanywa wakati viongozi wetu na watu wengine wanaopaswa kusimamia sheria wakiwa kama hamnazo.

Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani linajua aina hii ya usafirishaji mizigo ni kinyume cha sheria za nchi lakini wamekaa kimya kabisa. Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) wanajua kisheria vyombo hivi haviruhusiwi kusafirisha mizigo ya aina hii. Ni hatari kwa wasafirishaji na watumiaji wengine. Vituo vya ukaguzi wa mazao ya misitu vipo, vinatazama mamia kwa maelfu ya magunia ya mkaa yakipita bila vikwazo vyovyote.

Mamlaka za vijiji, kata na wilaya ziko kimya zikishuhudia mauaji haya ya mazingira bila kuchukua hatua zozote. Wasimamizi wakuu wa masuala ya misitu nchini – TFS ni kama vile wamesusa wakitamani siku moja waone jangwa linafanana vipi.

Mawaziri wenye dhamana ya kulinda rasilimali hii adhimu wako kimya kabisa. Wana hofu kuwaudhi ‘wapigakura’. Kwao kura ni muhimu sana kuliko mazingira.

Pikipiki zinazosafirisha mkaa zimeongezeka mno kipindi hiki. Nimewadadisi baadhi ya wasafirishaji hawa. Wanasema wameongezeka kwa sababu mamlaka haziwezi kuwagusa! Kwanini haziwagusi? Haziwagusi kwa sababu huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mwaka kesho kuna Uchaguzi Mkuu. Basi, tutarajie kifo cha misitu cha kutisha kwa miaka hii miwili.

Ndugu zangu, tunaweza kudhani tunawafurahisha ‘maskini’ kwa kuwaacha watende makosa haya ilhali ukweli ni kuwa haya tunayoyaacha yatamalaki ni maafa makubwa kwa uhai wetu wenyewe.

Misitu ya Mkoa wa Pwani inamalizwa. Haina mwenyewe. Vyanzo vya maji vinamalizwa huku serikali ikihaha kusambaza maji hata kule yalikokuwa yakitoka.

Tunafanya makosa makubwa sana kuamini kuwa pikipiki hizi hazina madhara kwa sababu wanasafirisha ‘vi-gunia’. Tunajidanganya. Tukumbuke wahenga walisema “bandubandu humaliza gogo.” Nimetulia mahali kwa saa tatu nikahesabu pikipiki zaidi ya 600 zikiwa na mkaa – kila moja ikiwa na wastani wa magunia matatu makubwa hadi manne.

Kuna dhana kwamba bei ya gesi ni kubwa, na kwamba ndiyo maana matumizi ya mkaa yanaongezeka. Hii si kweli hata kidogo. Unafuu wa mkaa ni kwa sababu mtu ananunua kibaba kwa kiasi kidogo cha fedha, lakini akiziweka pamoja kwa mwezi mzima fedha anazotumia ni nyingi kuliko kama angetumia gesi.

Kweli bei ya mtungi, gesi na jiko inaweza kuwa kubwa kwa wakati mmoja. Je, serikali haiwezi kuja na mpango wa ruzuku kwa wafanyabiashara au punguzo la kodi kwa vifaa hivi ili kila nyumba imudu matumizi ya gesi?

Bahati nzuri sasa gesi inauzwa hadi vijijini – ndani kabisa. Madai kwamba gesi haipo hayana ukweli wowote. Na wale walioacha uhafidhina wakaamua kutumia gesi watumike kuhubiri neema iliyomo kwenye matumizi ya majiko ya gesi badala ya mkaa.

Lakini wapo walioamua kutumia mkaa kwa sababu upo. Wapo wanaotumia kwa sababu wanaamini chakula kinachopikwa kwa kutumia nishati hiyo ni kitamu zaidi kuliko kile kinachopikwa kwa moto wa gesi.

Mwito wangu, mamlaka zisaidie kupunguza kasi ya pikipiki kumaliza misitu hii. Kama zitaruhusiwa [jambo ambalo litakuwa haramu kabisa], basi walau maduhuli yakusanywe kisha yatumike kurejesha uoto unaoharibiwa sasa.

Tanzania imekuwa kama haina mwenyewe. Watu wanaingia misituni wanakata miti kana kwamba tumeambiwa mwisho wa dunia umewadia! Hakuna tena hofu kwa serikali wala kwa Mungu. Bila mazingira maisha yetu yatakuwa ya aina gani?

Miti ya asili kwa sababu imemalizwa kwa sehemu kubwa, leo mafedhuli hawa wamegeukia miembe. Pwani yote inakatwa miembe ili kuchoma mkaa. Hii itaibua utapiamlo, maana makabwela waliokula maembe na kupata Vitamini C hawapati tena fursa hiyo. Maeneo kama Kibaha ambayo yalifunikwa kwa miembe, hali sasa ni tofauti. Miembe inakatwa kana kwamba hakuna tena ujio wa wajukuu.

Tusimame pamoja kukabiliana na hali hii ambayo kwangu naona ni dhambi kubwa. Mamlaka zinazohusika zizuie uharamia huu. Nchi inateketea. Nauliza, tumelogwa na nani? Mbona hatueleweki?