Vyama vya siasa vilivyowahi kuanzishwa kati ya mwaka 1927 na 2015 katika nchi ya Tanganyika, Zanzibar hata Tanzania havikubahatika kubuniwa, kuasisiwa wala kuongozwa na wanawake bali ni wanaume tu. Huu ni msiba mkubwa kwa akinamama, lau kama zipo sababu za utetezi.
Hata kama wanawake hawakujimudu kubuni, au kuasisi vyama vya siasa, ukweli waliweza kushawishi, kuhamasisha na kuvuta wake kwa waume kujazana ndani ya vyama hivyo na ndani ya vyama vya ushirika, wafanyakazi na vingi vinginevyo.
Kutokana na usiri walionao wa kuwezeshwa na hatimaye kuweza, wamethubutu kuunda vyama na taasisi zao katika mikondo ya elimu na taaluma, biashara, uchumi, ushirika na kutia vigingi katika vyama vya siasa wakitafuta haki zao na fursa za usawa katika uamuzi.
Tunashuhudia kuwapo kwa chama cha wanawake wanasheria Tanzania (TAWLA), chama cha wanawake waandishi wa habari (TAMWA), chama cha maendeleo wanawake (WAMA) na taasisi ya wanawake-ULINGO na vinginevyo. Vyote hivyo vinashughulika kuwapa uwezo na kushika vyombo vya uongozi na utawala.
Naweza kusema pia vyama na taasisi hizo zimebuniwa na kuasisiwa kwa malengo na madhumuni ya kumkomboa mwanamke wa Tanzania kifikra, kitamaduni na kiuchumi ili aweze kuongoza mamlaka zenye uamuzi wa juu bila shida wala mashaka.
Leo, tunashuhudia wanawake wengi wamesoma na wana elimu ya juu hata kuwapita baadhi ya wanaume. Hili halikanushiki hata chembe. Ndipo hapo wanapopata jeuri na ujasiri kuulani na kuusakama mfumo dume kuwa ni kandamizi kwa wanawake, lau kama mfumo jike nao unataka kutawala mfumo dume na kupata hadhi! Katika ofisi zetu za Serikali, mashirika, makampuni, mashule na vyuoni bila kusahau majeshini na mahakamani wamejaa tele wanawake wakichapa kazi ukilinganisha na miaka 30 iliyopita katika maeneo hayo. Sababu wamewezeshwa na wameweza.
Ndani ya vyama vya siasa na bungeni wanawake ni tishio na huko mitaani kwenye sekta binafsi na ujasiriamali usiseme. Jaribu kuvinjari kwenye madhehebu fulani fulani ya dini utawakuta wanawake wamechanua mithili ya mpunga kitopeni.
Kusherehesha fasihi yangu, Chama Cha Mapinduzi kimetuhemesha Watanzania pale kilipochomoka na makada na wanachama wake wakitangaza nia ya kugombea kiti cha urais. Wanawake wapatao sita (wakati naandika fasihi hii) wanaomba ridhaa ya chama chao hadharani kwa mara ya kwanza.
Akina mama hao ni Helena Elinawinga, Rita Ngowi, Monica Mbega, Dk. Asha-Rose Migiro, Dk. Mwele Malecela na Balozi Amina Salum Ali. Wote hao wamekwishashika madaraka makubwa ndani na nje ya chama chao na serikalini, huku wakitia fora katika utendaji kazi zao. Nawapa kongole.
Wamejitokeza hadharani kututanabahisha wananchi, sasa wanataka kushika hatamu za kuongoza nchi katika nafasi muhimu na nzito kimadaraka na kiutendaji.
Wamedhamiria kutuonesha uwezo walionao na watakavyomudu kuiongoza nchi pasi na vikwazo vya rushwa, ufisadi, ombaomba, umaskini na kujenga Taifa lenye uchumi imara. Mambo hayo yamo ndani ya uwezo wao.
Usione eti ni viroja mwanamke kutaka kuwa mkuu wa nchi mbele ya wanaume. Hapana. Hapana hata punje. Tangu enzi wanawake walipewa fursa ya kuongoza himaya na miliki za nchi, iwe ni Asia, Afrika, Ulaya na Marekani. Ndiyo hao wanaoitwa Malkia. Si kwa sababu tu eti wameolewa na watemi, masultani au wafalme. La hasha.
Mifano inapatikana katika nchi za Malawi, Liberia, Uganda, India, Brazil, Australia, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na katika nchi nyingine nyingi. Wanawake wamepata kushika nafasi za waziri mkuu, makamu wa rais na rais na kuonesha uwezo wa kuweza.
Mbali na akina mama hao wapatao sita wa CCM, na wengine huenda wakajitokeza kutangaza nia na wengine kutoka vyama vingine vya siasa wakigombea nafasi hiyo, wasipuuzwe ndani ya vikao vyao vya chama wala wasibezwe na wananchi watakapoletwa mbele yao kuwachagua kuwa viongozi wakuu wa nchi.
Endapo kweli wananchi tunataka mageuzi ya kisiasa na mapinduzi ya fikra na matendo, kuanzia kwa wananchi wenyewe hadi kwa viongozi hatuna budi kuangalia tena tunakotaka kwenda. Kwa sababu njia yetu ya kwenda huko twendako ni nyembamba mno na imepakatwa na kingo mbili za rushwa na umaskini kila upande. Tukiteleza tu tumetumbukia kwenye kingo hizo.
Kwa miaka kadhaa, tumesafiri na chombo hiki hiki na nahodha huyu huyu tukiwa salama salimini, lakini kwenye misukosuko ya mawimbi ya rushwa, ufisadi na umaskini. Tumechoka na bado hatujafika twendako!
Hoja au swali ni kujiuliza, tatizo ni nini, chombo tunachosafiria au nahodha anayetupeleka? Mwiko wa kusongea ugali jikoni, unawezekana kutumika kama fimbo ya kumcharaza mtoto aliyedokoa kinofu cha nyama kikaangoni. Upo?
Natoa inthari kwa mababa na akina mama wanawake wanaojitokeza kutangaza nia hawafanyi majaribio. Wamekusudia. Tunachohitaji ni kuwaangalia wana uwezo na sifa zitakiwazo? Kama wanazo sifa vipi tusiwape urais? KUMBUKA NJIA YETU NI NYEMBAMBA.