Wadau wa mchezo wa masumbwi nchini, wametakiwa kuingilia kati na kutafuta njia sahihi za kuunusuru mchezo huo unaoelekea kupotea kutokana na malumbano yasiyokuwa na tija kati ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na vyama vya michezo.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wadau wa mchezo huo wameshtushwa na malumbano yanayoendelea hivi sasa baina ya baraza na vyama vinavyoongoza mchezo huo.

Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin Abdallah ‘Ustaadh’, anasema ngumi ni mchezo unaopendwa na watu wengi hapa nchini baada ya mchezo wa soka, mchezo huo unazidi kupoteza msisimko wake.

Anasema bila ya jitihada za dhati kuuokoa mchezo wa ngumi ndani ya miaka michache ijayo, utabaki kama historia katika kumbukumbu ndani ya vichwa vya wapenda soka.

Yasini Abdallah anasema mwaka 1866 wakati mtawala wa Queensbury (Marguees of Queensbury)  nchini  Uingereza, alisaidia kutunga sheria mpya zilizotumika kuendesha mchezo wa ngumi, sheria ambazo kwa heshima zilipewa jina lake.

Anasema sheria hizo taratibu zilianza kutumika ndani ya nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya ukoloni wa taifa hilo, na zilihusu ngumi za kulipwa na ridhaa katika nchi husika.

“Sheria nyingi zinazotumika ndani ya nchi zetu hadi leo ni zile tulizorithi kutoka kwa hao wenzetu waliotutangulia katika michezo, kwa hivyo ukitaka kuzibadili ni lazima ufuate taratibu husika,” anasema Abdallah.

Anasema hapa nchini, mchezo wa ngumi za kulipwa haupo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hii ni kwa mujibu wa sheria namba 12 ya mwaka 1967 iliyokuja kufanyiwa marekebisho mwaka 1971 sheria hiyo inaeleza kuwa ngumi za kulipwa hazisimamiwi na Wizara na hata kwenye orodha ya vyama vya michezo inayotambuliwa na Baraza.

Anasema katika orodha hiyo ni ngumi za ridhaa pekee ndizo zinazotambulika kwa kupitia Boxing Federation of Tanzania (BFT) ziko chini ya wizara husika, lakini sasa wadau wa ngumi wanashuhudia mabadiliko ya makubwa kupitia BMT.

Yasin anasema Aprili mwaka huu, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, aliwaita viongozi wa mashirikisho ya ngumi kwa lengo la kuunda kamati ya kutengeneza katiba ambayo ingeunda chombo cha kusimamia ngumi za kulipwa hapa nchini.

Anasema baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, waliirudisha rasimu hiyo kwa kiongozi huyo wa Baraza kwa lengo la kuisoma na kuangalia upungufu na kurekebisha makosa kama yangekuwapo.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Mohamed Kiganja, anasema umefika wakati kwa wale wote wanaojiita wadau wa ngumi za kulipwa kufuata sheria bila shuruti.

Anasema kwa miaka mingi hapa nchini mchezo wa ngumi hasa za kulipwa umekuwa ukiendeshwa kiujanja ujanja, bila kufuata sheria.

Kiganja anasema, BMT ni chombo cha Serikali na tayari wametoa maelekezo kwa mashirikisho yote ya ngumi za kulipwa kuwajibika chini ya Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBC).

“Ni lazima wote tuwe na uwajibikaji wa pamoja hali itakayosaidia kuweza kuangalia nani anafanya nini na wapi na kwa wakati gani,” anasema Kiganja.

Anasema BMT litaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi, hivyo kusimamia michezo hapa nchini ili ichezwe kwa kufuata misingi ya kisheria.

Anasema wao kama watendaji watahakikisha sheria za nchi zinafuatwa na wale wote wanaojihusisha na michezo kwa manufaa mapana ya Watanzania wa leo na wajao.

Wakati Katibu Mkuu wa BMT akitoa msimamo wa araza hilo, Yasini anasema, “Hiki ni kichekesho kinacholetwa na kiongozi mwenye dhamana kuongoza michezo ya nchi hii, TPBC ni kampuni ya watu binafsi.”

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mchezo wa Ngumi za Kulipwa nchini (PST), Anton Lutta, anasema kwa ujumla katika miaka ya hivi karibuni ni kama imekuwa na laana linapokuja suala zima la michezo.

“Ndugu mwandishi, kama siyo laana ni nini… hebu iangalie michezo yote kwa ujumla kuanzia soka, kuogelea, masumbwi, riadha, judo na mingine mingi kila kukicha tunacho shuhudia ni migogoro isiyokuwa na tija, tena mingi ikiwahusisha viongozi,” anasema Lutta.

Anasema tangu Mohamed Kiganja awe Katibu Mkuu wa BMT, kila siku ni majanga, hali ambayo haikuwapo kwa watangulizi wake waliomtangulia kukiongoza chombo hicho kikubwa ndani ya nchi.

“Unapokuja na sera ya mashirikisho yote kuwa chini ya chama ambacho hakina tofauti na vyama vingine, ni kutaka kuchochea mgogoro usiokuwa na maana tena katika kipindi hiki ambapo hali ya michezo si nzuri hapa nchini,” anasema Lutta.

Naye  Rais wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBC), Chaurembo Palasa, anasema kumekuwa na vyama, asasi na vikundi ambavyo vimesajiliwa Brela lakini havikufuata taratibu za sheria na hawana vibali vya kuendesha mchezo wa ngumi nchini.

Anasema ifike wakati kwa wale wote wanaojihusisha na masuala ya mchezo wa ngumi kwa hapa nchini kufuata sheria zinazoongoza mchezo huo kwa maendeleo ya mchezo wa ngumi.

“Kukosekana kwa chombo kimoja kinachosimamia ngumi za kulipwa nchini, ndiyo maana leo tunashuhudia watoto wadogo wanapandishwa ulingoni kupigana bila ya kufuata taratibu,” anasema Palasa.