Mwezi mmoja uliopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari “Barua ya biashara kwa BRELA”. Brela ni Mamlaka ya Uandikishaji Biashara na Leseni. Baada ya kuitoa gazetini niliituma pia barua hiyo huko Brela kwa njia ya barua pepe.
Hadi sasa sijapata majibu wala mrejesho wowote kutoka huko japo akili yangu inanituma kwa asilimia mia moja kwamba imewafikia. Bado sijaacha kuamini kwamba Mamlaka hiyo ni taasisi makini na inayothamini michango na maoni ya wadau wa biashara katika kuboresha huduma zake.
Kutokana na imani yangu hii; natambua bila shaka yoyote kwamba ipo siku nitashuhudia maboresho makubwa ndani ya taasisi hiyo yatakayoondoa vikwazo kwa wajasiriamali wengi wanaostahili kushikwa mikono zaidi.
Niachane na Brela kwanza nigeukie matokeo ya barua ile jinsi ilivyopokelewa na mamia ya wasomaji. Wengi kutoka kundi la wajasiriamali waliguswa mno na mapendekezo niliyowapa Brela, na inaonekana ni kama nilikwangua viwango vya mioyo yao.
Wengi wameelezea kilio chao cha namna wanavyoteseka kufanikisha usajili wa biashara zao kutokana na Brela kuwapo Dar es Salaam. Ikumbukwe kwamba kwa sasa taasisi nyingi za fedha hazitoi mikopo hadi biashara iwe imesajiliwa Brela. Ukiacha hilo, wajasiriamali wengi wana kilio cha usaidizi wa kiushauri na kitaalamu kabla, wakati na baada ya kusajili biashara zao.
Kutokana na rundo la barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na simu nilizopokea; nimeguswa na kuumizwa sana na changamoto anazopata mjasiriamali anayeitwa Ponsian Rweyemamu Baitatafe kutoka Kijiji cha Kisenene, Kata ya Kasharunga, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.
Ndugu huyu baada ya kupitia ile barua ya biashara aliwasiliana nami kwa njia ya simu na baadaye akanitumia makabrasha ya biashara yake kwa njia ya EMS. Hatua ya kunitumia makabrasha hayo ilinipa picha ya namna alivyokwama kupata msaada wa kitaalamu kwa muda mrefu.
Nimechagua maoni na changamoto za mjasiriamali huyu kwa sababu zinachagiza maudhui ya makala niliyoiandika wiki mbili zilizopita – iliyokuwa na kichwa cha habari “Njooni shambani mtajirike”. Kwa kuwa mjasiriamali huyu anajishughulisha na kilimo cha miti; ndiyo maana nimevutiwa sana kumsemea kitu ninachoamini tutajifunza na Mamlaka husika zitahakikisha zinamsaidia.
Pamoja na makabrasha hayo aliambatanisha na barua; nami napenda kunukuu sehemu mbili katika barua hiyo: Nukuu ya kwanza; “…baada ya kusoma makala nzima nimejikuta nami ni mwathirika, nahitaji kutiwa moyo, nahitaji ushauri wa kitaalamu na wa kisayansi, nimegundua kuwa wewe ni mmoja wa watu ninaowahitaji wanisaidie.”
Nukuu ya pili; “Ukweli ni kuwa makala yako imetutia moyo na tumeona kuwa waweza kuwa mwalimu wa wajasiriamali walio na uthubutu wa hali ya juu katika shughuli zao. Lakini wanakosa mwongozo wa kuyafikia malengo waliyojiwekea. Njia zote za kupata msaada ni ngumu mno hasa sisi tuishio vijijini. Kwa pamoja tunaweza kuwa washindi kiuchumi. Hatuwezi kukata tamaa.”
Moyo wangu uliugua sana niliposoma barua yao na makabrasha yale yenye kurasa zaidi ya 25 pamoja na santuri (DVD) inayoonesha picha za mwendo (video) za mradi wake. Mjasiriamali huyu anajishughulisha na kilimo cha miti na kwa mujibu wa taarifa zake ni kwamba hadi sasa ana takribani ekari mia moja ambazo hazijafikia muda kamili wa kuvunwa.
Mjasiriamali huyu yuko na wenzake sita kama wanahisa katika mradi huu ni mfano halisi wa msaada wanaohitaji wajasiriamali kabla, wakati na baada ya kusajili kampuni ama biashara zao. Ponsian na wenzake wamesajili mradi wao pale Brela kwa jina la Porweba Investment Co. na wamepewa hati na vyeti vyote vya usajili.
Kwanza nilishangaa na nikawapongeza wadau hawa walioko kijijini mno; kuona kwamba wamepiga hatua kubwa ya walau kusajili mradi wao katika mfumo rasmi. Tatizo kubwa lililowapata na ambalo limekuwa ndiyo kilio changu ni mwongozo kabla na baada ya kusajili mradi wao.
Kwa kweli wamefanya kazi kubwa ambayo licha ya kuwa ni mradi wa kibiashara lakini una tija kubwa kwa mazingira. Wamenieleza kwamba wameshapata tuzo ya utunzaji wa mazingira katika ngazi ya kata. Pamoja na changamoto kadhaa za kiuendeshaji, lakini hii ni hatua kubwa hasa kwa mjasiriamali mvuja jasho.
Mjasiriamali huyu na wenzake wamejikuta wanakwama kuendelea mbele kutokana na kuchanganya malengo ya mradi wao. Wana mawazo mawili ambayo ingawa yana tija lakini hayabebani. Mradi wao wameusajili kibiashara na wakati huo huo wamekuwa wakisumbuka kuuendesha kiasasi.
Lengo la kwanza lilikuwa ni kumiliki kampuni ya kibiashara inayojishughulisha na kilimo cha miti; lakini wamejikuta wanachepuka na kuanza kukimbizana na harakati za kimazingira. Kama nilivyosema awali, wajasiriamali kama hawa ni kwamba wanakosa mwongozo sahihi pengine kutoka taasisi maalumu.
Kwa sababu ya kukosa taarifa, urasimu na hata mazingira yasiyo rafiki kwa biashara maeneo yao wanajikuta hawapigi hatua katika kufikia malengo yao. Mjasiriamali anapokosa ushauri wa kitaalamu mara nyingi hujikuta anapokea kila aina ya ushauri kutoka kwa yeyote. Mathalani; kwake Ponsian kuna watu walimshauri afuatilie watu wa mazingira wamsaidie.
Wengine walimwambia afungue kampuni atasaidika. Mfano kama lengo ni kupata misaada, ufadhili na udhamini kutoka kwa watu wa mazingira mradi wa Porweba haukutakiwa kusajiliwa kama kampuni ya kibiashara; badala yake ungesajiliwa kama taasisi ya kiraia (NGO).
Unaposajili mradi kuwa kampuni ya kibiashara rafiki zako wanatakiwa kuwa benki na taasisi nyingine zinazosaidia shughuli za utengenezaji faida. Haya yote ni mambo ambayo wajasiriamali hawayafahamu na wanapopiga mbizi kuelekea mafanikio njiani wanakutana na “majitu” (watu wanaokwamisha).
“Majitu” wengi ni wale ambao aidha wanawapa ushauri wa kupotosha ama wanakaa kimya wakishuhudia wajasiriamali wakipotea njia. Kama kungekuwa na kitengo maalumu kinachozalisha na kukuza wafanyabiashara; ingekuwa rahisi sana kusikiliza wazo la mtu, kuliweka katika makundi (biashara ama asasi) na kisha kuelekeza mahali pa kusajili (ni Brela ama Wizara ya Ustawi wa Jamii).
Hata hivyo, hawa Porweba Investment Co. licha ya kuwa na mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 100 na maelfu ya miti lakini wamekuwa na kilio kilichonihuzunisha. Hawana fedha kwa sababu mikopo kwao ni mithili ya mfupa mgumu. Hili ni tatizo jingine linalowatafuna wajasiriamali wengi. Mabenki na taasisi za fedha zinahitaji dhamana rasmi ili kuweza kutoa mikopo.
Kwa bahati mbaya wajasiriamali wengi hawana dhamana rasmi. Ninaposema dhamana rasmi ninamaanisha kuwa na hati ya mali zisizohamishika. Huyu mjasiriamali kutoka Muleba ana mamia ya ekari lakini hana hati, hivyo kila anakopiga hodi kuomba mkopo wanamwekea ngumu. Ni jambo la kuhuzunisha mtu kuwa na utajiri mkubwa namna hii halafu awe “masikini”.
Niliposoma makabrasha ya mjasiriamali huyu na kisha kuendelea kuwasiliana naye kwa simu nilibaini kuwa ana ndoto nyingi sana lakini hajui pa kuanzia. Kiu na malengo yake ni kupata mashine za kupasua mbao, kujenga kiwanda katika mashamba yake na kununua lori.
Lakini hana mtaji wowote wa kuanzia. Kama kawaida ya benki, wanamtaka apeleke hati ya mashamba yake ili wampe “mkwanja”. Kwa maana hii napenda kutumia wasaa huu, kuwaomba wadau wanaohusika wamuangalie mjasiriamali huyu na wengine wenye nia, kiu na mikwamo kama hii nchini. Kilio cha wajasiriamali wengi ni kupata hati za mashamba, nyumba, n.k.
Nitumie wasaa huu kuwashukuru wasomaji wengi wanaovutiwa na ujasiriamali, biashara na uwekezaji ambao wamekuwa wakifuatilia safu hii kwa ukaribu. Nimekuwa nikiwasiliana na mamia na wengi nimeendelea kuwapa ushauri kadiri niwezavyo. Kama ambavyo nimekuwa nikisema siku zote; kwamba binadamu tunazaliwa kwa ajili ya wengine.
Kusudi la kuzaliwa kwangu ni kuzalisha na kuendeleza wafanyabiashara na wawekezaji kwa maelfu hadi naingia kaburini. Mafanikio ya safu hii – Anga za Uchumi na Biashara – ni pale wasomaji wengi watakapofaidika iwe ni moja kwa moja; katika biashara, vitegauchumi ama mawazo yao ya kijasiriamali.
Kwa maana hii napenda kutumia wasaa huu kuwaomba wadau wanaohusika (hasa Serikali) wamuangalie mjasiriamali huyu na wengine wenye nia, kiu na mikwamo kama hii nchi nzima. Wajasiriamali tunahitaji ushindi wa kiuchumi na kimaisha.