DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Ni matamanio ya kila shabiki wa soka kuiona klabu anayoishabikia ikipiga hatua na kufikia mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuchukua mataji.
Naam! Ni kama vile kuwafikisha wana wa Israel katika nchi ya ahadi na mara zote kila anayepewa jukumu la kuisimamia timu fulani, hilo ndilo huwa jambo analolitamani zaidi.
Furaha kwa mashabiki. Mashabiki kushangilia ushindi, mashabiki kuyaona mataji. Wachezaji kufurahia kuwamo miongoni mwa wanaoandika na kuandikwa katika historia.
Lakini kwa sasa hali ikoje mitaa ya Jangwani na Twiga, nyumbani kwa moja ya klabu maarufu barani Afrika, Dar es Salaam Young Africans a.k.a Yanga?
Kwa hakika kwa sasa kila mmoja ameshika silaha. Wengine wanavyo vitanzi mikononi tayari kutekeleza hukumu kwa yeyote mwenye kustahili adhabu.
Ni kama vile vitanzi, silaha za moto na zile za jadi zimeelekezwa katika shingo ya mtu mmoja anayedhaniwa kuwa chanzo cha ‘yote’ kwa Yanga.
Huyo ni Mhandisi Heris Said wa pale Yanga. Kila mmoja anamtazama kwa jicho tofauti kama sababu ya Yanga kufika hapa ilipo. Heris amegeuzwa mbuzi wa kafara.
Binafsi nitakuwa mtu wa mwisho kuamini Injinia Heris ameshindwa kuifikisha Yanga katika nchi ya ahadi, Canaan ya Uyahudi.
Wakosoaji wake wengi wanampinga na kumuona kama mtu aliyekuja kusajili wachezaji magarasa katika timu yao. Wengi wanamkosoa hapa.
Lakini twende polepole. Namba kubwa ya wachezaji aliowasajili Injinia walikuja nchini wakiwa na sifa nzuri huko walikotoka. Hawakuja Yanga wakiwa magarasa kama walivyo sasa.
Mtazame Michael Sarpong wa Rwanda. Mwanamume huyu ambaye katika misimu miwili ya ligi ya nchini kwao Rwanda alipiga mabao 24! Baadaye corona ikaja kumharibia.
Msimu wa nyuma yake alifunga mabao 16 na katika msimu unaofuata akafunga mabao tisa, corona ikaja kuumaliza msimu wake. Baada ya hapo akasajiliwa na Yanga ya Dar es Salaam.
Huyu anakuwaje mchezaji garasa? Soka letu limemkataa. Huwa inatokea na wala yeye si wa kwanza, wala hatakuwa wa mwisho.
Carlos Carlinhos. Alikuja Yanga na matarajio makubwa. Alikotoka alikuwa mahiri kweli kweli! Katika eneo lake la kiungo, alicheza michezo saba akafunga mabao matatu. Corona ikaumaliza msimu katika staili hii.
Licha ya hivyo, Carlinhos ameondoka Yanga kama shujaa. Katika michezo yake tisa aliyocheza, amefunga mabao matatu, akatoa ‘assist’ zake mara tatu. Takwimu nzuri hizi.
Ukimtazama Injinia na ‘scouting desk’ yake, alisajili wachezaji wazuri, lakini ndani ya Yanga wameshindwa kuwa wazuri!
Ninarudia tena, huwa inatokea katika maisha ya mpira.
Farouk Shikalo mpaka anaondoka Kenya kuja Yanga ndiye aliyekuwa kipa bora wa Ligi Kuu ya Kenya. Joash Onyango alikuwa beki bora, Shikalo akawa kipa bora katika msimu huo huo, lakini ndani ya Yanga amekuwa hovyo, kosa la Injinia hapa liko wapi?
Yacouba amekuja Yanga na alicheza michezo saba akakaa muda mrefu bila kucheza kutokana na corona. Katika michezo hiyo, hajafunga bao, lakini Yacouba aliwahi kuja nchini na Asante Kotoko. Kila mmoja anaujua ubora wake. Ndiye mfungaji wa Yanga mpaka sasa.
Saidoo Ntibazonkiza na Fiston Abduzarack ni mapendekezo ya kocha aliyeondolewa, Cedric Kaze. Wachezaji hao waliletwa na kocha huyo ambaye naye ni Mrundi kama walivyokuwa wachezaji hao.
Nani asiyejua umahiri wa Bakari Mwamnyeto? Huyu ni mmoja wa wachezaji bora wa msimu uliopita walioingia katika kikosi bora cha msimu wa ligi.
Mtazame na Zawadi Mauya. Alikuwa sehemu ya timu iliyofanya vema katika msimu uliopita alipokuwa na Kagera Sugar, muda huu tuliomuwekea Injinia silaha za moto katika shingo yake na kutaka kumpiga kitanzi, tumshukuru kwa usajili wa kina Tonombe Mukoko na Tuisila Kisinda.