Nimetembelea hivi karibuni maonyesho ya wakulima yaliyoadhimishwa kitaifa Nyakabindi, Simiyu, kilomita 20 kutoka Bariadi.
Kwa miaka kadhaa nilidhamiria kuhudhuria maonyesho hayo baada ya kujitumbukiza kwenye kilimo, nikiamini ingekuwa sehemu muhimu ya kujiongezea elimu na maarifa kwenye shughuli ambayo sina uzoefu nayo.
Nimetoka huko nikithibitisha tu yale niliyoyatarajia. Mkulima, mfugaji, au mvuvi atajifunza mengi ya manufaa kwa kuhudhuria maonyesho hayo na mengine ya aina yake.
Maonyesho ya Nane Nane kitaifa yanajumuisha washiriki zaidi ya 300 kutoka wizara mbalimbali, taasisi za umma, halmashauri, mashirika, kampuni, na watu binafsi.
Ni maonyesho ambayo yamesheheni wataalamu wanaotoa elimu muhimu kabisa kwa Watanzania ambao wanazalisha katika sekta hizi tatu.
Nimepata elimu ya umwagiliaji kama nyenzo ya kunihakikishia uzalishaji bila kutegemea mvua zisizotabirika. Nimepata elimu ya ufugaji nyuki ambao badala ya kuendelea kunishambulia nyumbani sasa nakusudia kuwatumia kuzalisha asali na nta. Aidha, nilitembelea banda la wataalamu wa ufugaji samaki nikaondoka na elimu juu ya ufugaji wa kwenye matangi ambao ni rahisi zaidi kuanzisha na kusimamia kuliko ufugaji wa mabwawa.
Si eneo la wataalamu kufundisha tu, bali pia ni sehemu wao kujifunza. Uzoefu ni suala ambalo halipatikani darasani pekee. Wakulima, wafugaji, na wavuvi nao wana uzoefu wa kuwapa wataalamu.
Nyakabindi nimekutana na mwanakijiji mwenzangu, Nashon Musiba Jirabi, mfugaji mahiri wa ng’ombe wa maziwa aliyeshiriki kwenye maonyesho, akiwa amepeleka ng’ombe wawili wa maziwa kutoka kwenye kundi lake la ng’ombe 16.
Alianza ufugaji miaka zaidi ya kumi iliyopita na ng’ombe mmoja na ameboresha uzao wa ng’ombe hao, na kuongeza uzalishaji hadi kufikia lita 100 kwa siku. Kwa kiwanda siyo kiwango kikubwa, lakini ni msingi mzuri wa kuanzisha kiwanda kidogo cha bidhaa zinazotokana na maziwa, suala ambalo anapanga kutimiza.
Ameniambia kajifunza mengi tangu aanze kushiriki maonyesho hayo mwaka jana. Lakini nimegundua kuwa anayo ya kufundisha pia. Nilishuhudia akitoa ushauri kwa baadhi ya wataalamu juu ya, mathalani, uboreshaji wa mashine zilizoletwa kwenye maonyesho. Wataalamu huamini kuwa kila teknolojia mpya husaidia kurahisisha uzalishaji, lakini yapo mazingira yanayolazimu kubaki na teknolojia ya zamani ili kuhakikisha uzalishaji hausitishwi.
Nashon alishauri kuwa mashine ya kusaga nafaka inayozungushwa kwa mkono inampa uhakika zaidi wa kuzalisha kuliko mashine hiyo hiyo iliyounganishwa na injini ndogo. Mkono hautumii dizeli, na ni nadra kuhitaji vipuri. Ni ushauri ambao mtaalamu aliondoka nao na labda ataufanyia kazi mwakani.
Ni muhimu sana kwamba, kila yanapoisha maonyesho, ile elimu na maarifa viendelee kuenezwa. Kilimo ni sekta muhimu kabisa kwenye uchumi wa Tanzania. Inakadiriwa kati ya asilimia 70 hadi 80 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo. Takwimu za Shirika la Chakula Duniani zinaonyesha kuwa sekta ya kilimo nchini inachangia asilimia 27 tu ya pato la taifa. Sekta ya mifugo inachangia asilimia 7.2 ya pato.
Kwenye kilimo tija inaweza kupanda sana kwa kuongeza uzalishaji, kupanua mashamba, kutumia umwagiliaji, kutumia mbegu bora, na pembejeo.
Kwenye mifugo tija inaweza kuongezeka kwa kuboresha kiwango cha kuzaliana kwa mifugo, kupunguza vifo vya mifugo, na kuhimiza kinga dhidi ya magonjwa.
Ni kwa kufikisha tu elimu na maarifa kwa wazalishaji ndiyo huu upungufu uliyomo kwenye sekta hizi unaweza kupunguzwa au kumalizika na wazalishaji kunufaika na ongezeko la bidhaa na mapato, na hatimaye kukuza pato la sekta hizi na pato la taifa.
Anayehudhuria maonyesho yale anaweza kupata sehemu tu ya elimu na maarifa yale, lakini hayo kidogo yanaweza kuwa mwongozo mzuri wa kumwelekeza mdau kwenye kuboresha uzalishaji.
Lakini tunafahamu kuwa si kila mmoja ana uwezo wa kuhudhuria. Ni kwa sababu hiyo basi upo ulazima wa kuwapo mikakati madhubuti ya kueneza ile elimu na maarifa kwa wadau wengi iwezekanavyo.
Tunaweza kudhani wale wataalamu wa sekta hizi ambao wapo kwenye halmashauri wanaweza kusambaza elimu hii bila kuwapo haja ya maonyesho ya aina hiyo, lakini uzoefu unaonyesha vipo vizingiti vingi – muda, gharama, na hata uthubutu tu – vinavyomzuia mzalishaji kufunga safari kwenda kumtafuta mtaalamu ampe ushauri.
Naamini kuwa njia bora ya kueneza elimu na maarifa haya ni kupitia vipindi maalumu vya redio zilizoenea nchi nzima. Nimewahi kusikia kipindi cha mawaidha ya kilimo kwenye redio moja inayosikika Butiama, lakini sina hakika kama ni vipindi ambavyo vinatumika sana kwingineko.
Nikiwa kwenye maonyesho nilijiandikisha kwenye mfumo wa utabiri wa hali ya hewa unaomtumia mkulima taarifa za hali ya hewa pamoja na ushauri juu ya maandalizi muhimu ya kilimo, pamoja na kushauri aina ya mazao ya kupanda kutegemea na hali ya mvua.
Kuenea kwa simu za viganja kunatoa fursa nyingine nzuri na rahisi ya kufikisha ujumbe kwa wadau.
Maonyesho ya Nane Nane ni darasa muhimu sana la sekta ya kilimo, mifugo, na uvuvi, lakini ni darasa linalonufaisha wachache. Ni muhimu iwepo mikakati madhubuti ya kueneza zaidi manufaa ya darasa hilo kwa wengi nchini kote.
Maoni: [email protected]