Kwa wasiofahamu ni kwamba Kocha Jose Mourinho mbali ya kuwa na utani wa jadi na Arsene Wenger wa Arsenal, lakini alikuwa na upinzani mkali hasa wa maneno ya karaha na Sir Alex Ferguson, kocha wa zamani wa Manchester United.
Ferguson aliinoa Manchester United kuanzia mwaka 1986 kabla ya kuitema timu hiyo mwaka 2013 na kumwachia timu raia mwenzake wa Wales, David Moyes aliyetokea Everton.
Hakuna ubishi kwamba Mourinho si kwamba alikuwa mpinzani wa visa wa Ferguson, lakini alikuwa anajifunza mambo mengi kwa mkongwe huyo alitunukiwa cheo cha Sir na Malkia wa Uingereza, Elizabeth II.
Hakuwahi kutamka hadharani, lakini inaonekana alikuwa anaota siku moja kuinoa United inayofahamika zaidi kama Mashetani Wekundu. Ndiyo maana kuna habari ambayo Mourinho hakuwahi kuikanusha.
Mara baada ya Sir Alex Ferguson kustaafu rasmi baada ya kukaa na Mashetani hao Wekundu kwa miaka 27, Mourinho alipiga hesabu za kuinoa United na tayari watendaji kadhaa walimpigia debe.
Taarifa zinasema, dakika za mwisho majina mawili yaliingia kwenye fainali ya nani awe kocha wa United. Majina ya David Moyes na Mourinho. Aliyepewa nafasi ya kumteua mmojawapo, ni babu mwenyewe, Ferguson. Lakini hakupewa kazi ya kuteua tu, bali pia kutoa sababu.
Ndipo Ferguson akamteua Moyes akisema kwamba anahitaji kocha ambaye anaweza kuvumilia na kukaa na timu kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwake. Basi hapo ndipo Moyes akapewa timu.
Wachambuzi wa mambo pia wanaona wazi kuwa Babu Fergie alimpendelea Moyes kwa sababu alimuuzia Wayne Rooney kadhalika dhana ya ukabila kwani wote wanatoka Wales.
Watu wa karibu wa Mourinho wanasema, siku Moyes anatangazwa, kocha huyo raia wa Ureno, aliingia chumbani kwa muda mrefu akilia, akimwaga chozi la uchungu kwa kushindwa kutimiza ndoto zake.
Mourinho ni jina kubwa, alitaka timu kubwa kama United yenye umaarufu zaidi ya Chelsea licha ya kuzinoa timu kama Porto ya Ureno, Inter Milan ya Italia kadhalika Real Madrid ya Hispania.
Kuona hivyo, Mourinho wakati huo akitokea Madrid akaamua kurejea kuinoa Chelsea iliyopata kumtimua kwa aibu mwaka 2009 huku United ikisonga mbele Moyes.
Alirudi kwa mara ya Juni, 2013 na msimu uliopita akawaongoza kushinda Ligi Kuu ya England na Kombe la Ligi.
Sifa za Moyes kwamba anakaa na timu muda mrefu haikuwa kwa United kwani alifundisha kwa miezi 10 tu kabla ya kutimuliwa na nafasi yake kushikwa kwa muda na mchezaji mkongwe wa timu hiyo, Ryan Giggs.
Giggs alikaa na United kwa mechi kadhaa kabla ya kumkabidhi kijiti hicho Louis van Gaal ambaye katika msimu wake wa pili ndani ya United, mashabiki wa mashetani hawana raha naye.
Wengi ni wale walioamini kwamba United ilimfaa Mourinho ambaye kwa sasa hana tena kazi kwani Alhamisi iliyopita, Chelsea ilimfuta kazi baada ya kuona haipi mafanikio timu hiyo iliyojaza wachezaji wenye vipaji. Chelsea maarufu kama The Blues wameshinda mechi tisa kati ya 16 za kwanza Ligi Kuu ya England.
Je, huu ni wakati mwafaka kwa Kocha Jose Mourinho kutimiza ndoto zake? Inawezekana kwa kuwa wakala wake amesema kuwa Mreno huyo hatakwenda likizo baada ya kutemwa.
“Hataenda likizo, hajachoka, hahitaji likizo,” taarifa kutoka kwa wakala anayemwakilisha Mourinho imesema na kuongeza: “Ana matumaini sana na tayari anaganga yajayo.”
“Jose Mourinho ana furaha kwamba alirejea Chelsea kwa sababu aliweza kuwapa mashabiki taji jingine la Ligi ya Premia, ligi ambayo hawakuwa wameshinda kwa miaka mingi,” taarifa ya Mourinho imesema.
Anasema: “Anajivunia sana kushinda mataji nane akiwa Chelsea na anawashukuru mashabiki kwa kumuunga mkono vipindi hivyo viwili alikuwa katika klabu hiyo.
“Wakati wa maisha yake ya ukufunzi, Jose wakati mwingine amekuwa akiamua kuondoka katika klabu, lakini ni Chelsea pekee ambako klabu iliamua anafaa kuondoka.”
Aliyekuwa meneja wa timu ya taifa ya Uholanzi, Guus Hiddink ameteuliwa kuwa kaimu kocha wa Chelsea hadi mwisho wa msimu kuchukua nafasi ya Mourinho.
“Nimefurahia kurejea Stamford Bridge. Chelsea ni moja ya klabu kubwa duniani lakini haimo pale inakofaa kuwa kwa sasa. Hata hivyo nina uhakika tunaweza kubadilisha mambo,” amesema Hiddink.
“Nasubiri kwa hamu kufanya kazi na wachezaji na wakufunzi wenzangu wapya katika klabu hii kubwa na kufufua uhusiano wangu mzuri na mashabiki wa Chelsea,” anasema.
Hiddink, aliwahi kuinoa Chelsea wakati mmoja, alipowasaidia kushinda Kombe la FA mwaka 2009, lakini bado hajatia saini mkataba.
The Blues wamo nambari 16 ligini kwa sasa baada ya kushindwa mechi tisa kati ya 16 walizocheza msimu huu Ligi Kuu Uingereza.
Hiddink alishinda mataji sita ya ligi ya Uholanzi na Kombe la Ulaya akiwa meneja wa PSV Eindhoven ya Uholanzi katika vipindi viwili.
Pia aliongoza timu za taifa za Korea Kusini, Australia na Urusi kabla ya kujiunga na Chelsea mara ya kwanza kujaza pengo lililoachwa na Luiz Felipe Scolari, Februari 2009.
Alijiuzulu wadhifa wake kama mkufunzi wa timu ya Taifa ya Uholanzi mwezi Juni, baada ya kutofanya vyema katika juhudi za kuwasaidia kufuzu kwa Euro 2016.
Ile Mourinho kuondoka tu, Chelsea wamerejea kupata ushindi baada ya kulaza Sunderland 3-1 mechi yao ya kwanza bila Jose Mourinho aliyefutwa Alhamisi.
Uwanjani Old Trafford, mambo yamemwendea mrama Kocha Louis van Gaal baada ya vijana wake wa Manchester United kukabidhiwa kichapo cha 2-1 na Norwich City.
Kutokana na kipigo cha Jumamosi iliyopita, Manchester United sasa wamo nambari tano katika msimamo wa Ligi Kuu baada ya kukusanya pointi 29 sawa na Spurs ambao wamo nafasi ya nne, lakini wanawazidi kwa mabao.
United wamo pointi tisa nyuma ya vinara wa sasa Leicester wenye pointi 38. Nambari mbili na tatu zinashikiliwa na Arsenal (pointi 33) na Manchester City (alama 32).
Hali hiyo inazidi kumfanya Van Gaal kuwa katika wakati mgumu katika timu hiyo kwani naye anatajwa kung’oka. Je, hiyo inaweza kuwa nafasi nyingine kwa Muorinho kuchukua United. Bila shaka ni jambo la kusubiri na kuona.