Hakuna shaka kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli imefanya mambo mengi mazuri katika kipindi hiki cha miaka mitatu.
Yapo pia mengine ambayo anakosolewa, na baadhi ya watu wanasema laiti kama angeyatenda kwa kadiri ya mtazamo wao, basi historia yake ingeandikwa kwa wino wa dhahabu kwenye kumbukumbu za uongozi wa taifa letu.
Hili si jambo la ajabu kwa binadamu. Kuna kupatia na kukosea, lakini lililo kubwa ni kwamba ni vigumu mno kuwaridhisha au kuwaudhi binadamu wote. Pamoja na yote, kwa ujumla wake tunaweza kusema mengi aliyoyafanya ndani ya miezi hii 36 ni ya kupigiwa mfano. Sina sababu ya kuyataja, kwani yanajulikana na yanaonekana.
Rais Magufuli na wasaidizi wake ni binadamu. Kiongozi anayejituma kulitumikia taifa huwa mnyonge pale anapokatishwa tamaa hasa anapoona wakosoaji wakijiegemeza zaidi kusaka kasoro na kuyafumbia macho mengi mazuri.
Pamoja na wanaomkosoa, ama kwa nia njema, au kwa husuda tu, pia kumejitokeza baadhi walioamua kusifu tu. Rais hana budi kuwa makini kwa hizi sifa. Asiwe mwepesi wa kuzipokea tu. Azichambue.
Kumwaga sifa pekee bila kukosoa au kushauri ni kumuumiza anayesifiwa. Taratibu, tunaanza kuwaona na kuwasikia baadhi yetu wakijitwika dhima ya kusifu. Ni hao hao watakaokuwa mbele kumkejeli na kumwandama Rais Magufuli akishamaliza ngwe yake. Wale wanaomtakia heri yeye binafsi na nchi yetu wataendelea kumshauri na kumkosoa panapostahili, lakini kumkosoa kwa staha.
Nimesema yapo mengi mazuri ambayo Rais Magufuli ameyafanya. Sina sababu ya kuyarejea hapa. Yanaonekana kila mahali.
Pamoja na yote hayo, mitaani kuna maneno yanayosemwa ambayo kwa mtazamo wa wanaoyasema ni kwamba endapo atayarekebisha atakuwa amejiweka kwenye nafasi ya kuwa kiongozi wa kukumbukwa. Wanazungumzia matukio kama ya watu kutekwa, mauaji yanayofanywa na polisi, kubanwa kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani na kadhalika. Haya wanayasema, japo ni wazi kuwa kila mmoja wetu anaweza kuwa na mtazamo wake kulingana na mahitaji ya nchi kwa wakati husika.
Kwangu niseme moja: Wiki iliyopita tumemsikia Waziri wa Fedha akieleza kuhusu mwelekeo wa uchumi ulivyo. Kwa kuitafsiri mistari ya hotuba yake, hali si nzuri sana kiuchumi. Kwenye mapato, akasema: “Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya mwaka 2017/2018, ni pamoja na zifuatazo: (i) Ugumu wa kukusanya kodi kutoka kwa WAFANYABIASHARA waliopo katika sekta isiyo rasmi kwa kuwa hawana sehemu rasmi na za kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi kumbukumbu…(iv) Upungufu wa wafanyakazi na vitendea kazi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, hivyo kupunguza ufanisi wa utendaji kazi wa Mamlaka…(v) Kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo wakati wa utekelezaji wa bajeti.”
Nianze na kipengele cha kwanza: Haya mambo tumekwisha kuyasema sana kwamba uchumi wa nchi yetu hauwezi kukua kama serikali yenyewe imeamua tuwe nchi ya wachuuzi. Kuyajua haya mambo si lazima mtu awe amesoma uchumi.
Tunakosea mno kuua utaratibu au utamaduni unaowafanya Watanzania kuona kuwa kulipa kodi ni suala la ‘hisani’. Hatuna budi kumfanya kila aliye mzima na timamu kiakili kujiona ana wajibu kwa taifa lake kulipa kodi. Ulipaji wa kodi ni utamaduni unaojengwa kama mtoto anavyoandaliwa kuwa na maadili mema. Ulipaji wa kodi ni kipengele cha maadili ya mtu aliye timamu kiafya – kimwili na kiakili.
Rais Magufuli ameamuru wamachinga waachwe wafanye biashara popote wanapotaka. Amewatetea kwa kuwaamuru viongozi waliothubutu kuwaondoa wawaache. Hii ni huruma ya kiongozi mkuu kwa wananchi wake. Swali la kujiuliza, huruma hii ina tija kwa jamii na nchi? Tija inaweza kuwapo kwa hao wanaosamehewa kwani wataimba na kumshangilia rais. Kwa mwanasiasa huu ni mtaji wa kisiasa, lakini pia wa kiutu.
Matokeo yaliyopo kwenye uamuzi huu ndiyo haya yanayosemwa sasa na Dk. Mpango. Hakuna makusanyo. Hakuna kodi zinazolipwa, sana sana kinachopatikana ni ushuru ambao hauwezi kuwa na faida kubwa kwa maendeleo na uchumi wa nchi.
Ruhusa hii ina athari nyingi kiuchumi, lakini pia kiafya, kimazingira na hata kwa ustaarabu wa jamii. Wamachinga ni wachuuzi, lakini leo tunawaita wafanyabiashara! Mtu anapopanda daraja kutoka kwenye uchuuzi na kuwa mfanyabiashara ni lazima alipe kodi.
Kwa kuamuru wamachinga waachwe watambe kokote wanakotaka, wapo wafanyabiashara waliovaa joho la umachinga. Mfanyabiashara gani atakuwa mjinga akubali kutumia EFD machine kulipa kodi wakati mzigo huo huo wa redio, nguo, masanduku na kila kitu anaweza kuuza yeye au kumpa kijana akauza kwa ujira mdogo na tena bila kulipa kodi?
Tunavyoona sasa kuna ongezeko kubwa la wamachinga. Kisiasa tunaweza kudhani tunawasaidia vijana kujiajiri, lakini kiuhalisia ni kuwa wanaofaidi ni wafanyabiashara, hasa wale wa kati waliogeuka kuwa wamachinga japo hawaonekani umachingani kwa sura zao.
Mbele ya maduka makubwa wamejaa. Wenye maduka makubwa wala hawagombani nao! Kwanini hawagombani ilhali wanazibwa? Wananyang’anywa wateja? Hawagombani kwa sababu zile biashara ni za hao wenye maduka! Kama mfanyabiashara aliuza bidhaa za Sh milioni 5 kwa siku, kwa utaratibu huu atakuwa anauza Sh milioni 2. Zile Sh milioni 3 ziko kwa wamachinga na hazina EFD machine. Je, nini kitazuia mapato ya TRA kushuka?
Biashara nyingi zinafanywa na wamachinga bila EFD halafu waziri anakwenda bungeni kulalama kuwa makusanyo ya kodi si mazuri! Ajabu sana. Waziri amshauri rais utaratibu huu wa wamachinga utazamwe upya. Watengewe maeneo maalumu. Wajulikane walipo ili kodi ikusanywe.
Athari nyingine ya ruhusa hii ni bughudha na mparaganyiko wa mipango miji. Agizo la Rais Magufuli limeathiri mipango miji. Kwa mfano, Arusha si jiji tena, bali ni zizi. Mji ule uliokuwa mzuri kwa watalii wa ndani na nje, leo ni gulio. Mwanza ni hivyo hivyo. Vurugu kila mahali. Barabara zote muhimu zimezibwa na wachuuzi. Hapa kunauzwa mitumba, pembeni kunauzwa sharubati, mbele kuna gereji ya Bajaj, kushoto kuna mahubiri ya dini, kando ya taa za kuongoza magari kuna mama ntilie ameweka mabenchi kwa wateja wake; alimradi kila kitu ni shaghalabaghala.
Katika Jiji la Dar es Salaam, katikati ya jiji kote hakufai. Hakuna sehemu za waenda kwa miguu. Mtaa wa Samora uliokuwa kivutio kwa wageni na wenyeji sasa ni wa sidiria za mitumba, mafenesi, maparachichi, miwa, mihogo, mahindi, viazi, viatu, kina mama ntilie na makundi kwa makundi ya vijana wachuuzi walioshika vitu mikononi.
Eneo la Kariakoo kuna mitaa magari hayapiti tena. Kuna tukio la dereva aliyepigwa na kuuawa kwa kuwa alikanyaga fungu la bamia zilizotandazwa barabarani! Dereva anauawa kwa kukanyaga bamia zilizo kwenye njia ya vyombo vya moto! Hii ni hatari.
Ustaarabu ni kuishi kwa mpangilio. Ustaarabu ni kitu kuwekwa au kuwapo mahali kunakostahili, ndiyo maana anayejisaidia kando ya choo badala ya kutumia shimo huonekana mtu wa ajabu hata kama amefanya hivyo chooni. Ukiingia nyumbani kwa mtu ukakuta soksi zimetunzwa kwenye jokofu badala ya soda, lazima huyo mtu utamshangaa. Tunayoyafanya sasa kwenye miji yetu wageni wanatushangaa kama ambavyo mtu anaweza kumshangaa anayejisaidia sebuleni.
Hawa wamachinga waliopewa ruhusu na rais wauze kokote wanakotaka ni jeshi hatari la baadaye. Iwe ni kwa serikali hii au nyingine itakayokuja, uamuzi wowote wa kuwaondoa wamachinga mitaani ni tangazo la vita! Tutaingia kwenye vurugu kubwa maana wataona wanaonewa! Kwa hiyo ni kama tumekubali miji yetu iwe ya kijima daima na milele.
Kiafya: Leo kila mchuuzi anaweza kuuza matunda na chakula bila kupimwa afya. Matikiti, machungwa na vyakula vya aina zote vinauzwa kiholela. Hakuna kujali vumbi, makohozi, moshi wa magari wala uchafu wa kibinadamu wa anayeuza na wanaonunua kwa kushikashika.
Matokeo ya hali hii ndiko tunakosikia sasa serikali ikitamba kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba! Maana yake nini? Hii ina maana tunahalalisha mazingira machafu ya watu kuugua ili tutenge na tutumie mabilioni kununua dawa hata kwa magonjwa ambayo yangezuiwa kwa mwongozo wa bwana au bibi afya tu. Tunatumia mabilioni kutibu badala ya kutumia maelfu kadhaa kuzuia hali hii.
Hakuna mji mkubwa duniani usiokuwa na wamachinga. Hata Washington DC wapo tele, lakini kuna utaratibu. Wamachinga hawawezi kuzuiwa kwa sababu ajira zenyewe hazipo za kuwatosheleza vijana wote wa taifa hili.
Hata hivyo, ni sharti tuwe na utaratibu, na huo utaratibu ni kuwatengea maeneo maalumu ya kuendeshea biashara zao. Kufanya hivyo kuna faida nyingi. Kwanza, watalipa kodi, maana wanapata fedha, kwa sababu hiyo hawana udhuru wa kutolipa kodi. Kuwaacha waendelee na mfumo huu huria maana yake serikali itaendelea kulialia kila mwaka kwa kukosa mapato.
Maeneo kama Mbezi Mwisho na mengine yanayochipukia kwa kasi, serikali itenge fedha, iwalipe wananchi fidia kisha ijenge masoko kwa wamachinga na wachuuzi wengine.
Uamuzi huo utasaidia mambo mengi. Utaifanya miji yetu ipendeze tofauti na vurugu za sasa. Mapato ya nchi yatakusanywa.
Mwisho, TRA hawana wafanyakazi na vitendea kazi vya kutosha. Haya ni maajabu katika ulimwengu wa maendeleo! Nini kinazuia TRA kuajiri na kupata vitendea kazi ili kupitia kwao serikali ikusanye kodi ya kutosha? Je, rais ndiye amezuia wasiajiri? Dk. Mpango anapolia kwa kukosa wakusanya kodi anataka tumsaidie nini? Anataka sote tushiriki kulia? Hapana.