Na Cresensia Kapinga, JamuhuriMedia, Namtumbo
WAKAZI wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kuhakikisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo zinakua endelevu ili kuwafikia wananchi wengi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini.
Wametoa ombi hilo jana,wakati wa zoezi la uchunguzi na matibabu za magonjwa ya moyo zinazotolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya tiba ya magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo.
Said Ngonyani,ameomba Serikali kupitia taasisi hiyo kuwa na utaratibu ya kuwawekea kambi ya madaktari bingwa kama hao angalau mara moja kwa mwezi ili wananchi wengi waweze kupata huduma za kitabibu na kupunguza gharama za usafiri kufuata huduma hizo.
Ngonyani alisema,wananchi wengi wanaishi maeneo ya vijijini na vipato vyao ni vidogo na haviwezi kumudu gharama za kufuata huduma za kibingwa katika Hospitali za rufaa,hivyo wengi wao wanajikuta wakiathirika na kupoteza maisha kwa kukosa matibabu ya kibingwa.
“wananchi wengi vipato vyetu ni vya chini na tunategemea kilimo kuendesha maisha yetu,hivyo hatuwezi kumudu kabisa gharama za kusafiri kwenda nje ya wilaya yetu au mkoa kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa,tunaopata shida ni sisi ambao tumeshakuwa watu wazima,tunaiomba serikali itufikirie katika hili”alisema Ngonyani.
Naye Emelia Ngonyani alisema,wananchi wengi wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali,lakini wanashindwa kusafiri na kufuata huduma za kibingwa kwa kuhofia gharama kubwa,lakini uwepo wa kambi hizo wanaweza kunufaika kwa kupata vipimo sahihi na matibabu bure.
“Nimefika kupata matibabu baada ya kupata taarifa za uwepo wa madaktari bingwa katika wilaya yetu,nimefurahi sana kwani awali tulilazimika kufuata huduma hizi Hospitali kubwa kama Songea au Peramiho,lakini leo zimetufikia hapa hapa Namtumbo”amesema Ngonyani.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa amesema siku ya kwanza wamejitokeza zaidi ya wananchi 168 waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu,na wamebaini wananchi wengi wanahitaji kupata huduma hizo mara kwa mara.
“Ofisi ya mbunge itaendelea kuliangalia jambo hili kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine ili kuwe na utaratibu wa uwepo wa kambi kama hii mara kwa mara ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wananchi”amesema.
Kawawa amesema,wananchi wengi wenye uhitaji ni wale wenye vipato vya chini na hawawezi kumudu kufuata huduma za kibingwa katika Hospitali za rufaa.
Ameongeza kuwa,Ofisi yake imeamua kufadhili kambi hiyo ya madaktari bingwa ili kusaidia kuboresha afya za wana Namtumbo kwa kuhakikisha wanapata vipimo na matibabu ya uhakika yanayotolewa bure.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya ,amewataka wananchi wa Namtumbo kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo kwenda kupata vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo ili kuwa na afya itakayowawezesha kushiriki katika shughuli zao za maendeleo.
Malenya,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Sh.bilioni 1.5 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya afya katika wilaya ya Namtumbo ikiwemo kituo cha afya Lusewa na Sh.bilioni 1.3 kwa ajili ya kununua vifaa tiba.