Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshatimiza mwaka mmoja tangu ashike wadhifa huo.
Ukimtazama usoni, unamuona Majaliwa tofauti na yule aliyeonekana siku jina lake likisomwa bungeni Dodoma kushika wadhifa huo. Huyu ni Majaliwa aliyejaa msongo wa kazi nyingi alizokubali kuzibeba kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.
Katika kipindi chake cha mwaka mmoja, Waziri Mkuu ameonesha kuwa uamuzi wa Rais John Magufuli kumteua kushika wadhifa huo, ulikuwa sahihi.
Nimepata fursa ya kuzungumza na Waziri Mkuu mara kadhaa. Nimebaini mambo kadhaa muhimu kutoka kwake – anaipenda Tanzania na Watanzania. Ana maono ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya kupigiwa mfano kimaendeleo. Ana kasi ya utendaji mambo bila kigugumizi. Waziri Mkuu hana mzaha dhidi ya watendaji wazembe au wanaofanya kazi kwa mazoea. Kwa mwaka huu mmoja amethibitisha pasi shaka kuwa anaimudu nafasi hiyo.
Wanasema kazi ya wanahabari si kupongeza. Siamini katika nadharia hiyo. Siamini kwa sababu niliwahi kusema katika mazingira ya ‘vita’, mwanahabari wa kweli anapaswa kuwa upande wa serikali/nchi yake.
Nchi yetu kwa sasa ni kama iko katika vita – vita dhidi ya rushwa, vita dhidi ya uzembe, vita dhidi ya ufisadi, vita dhidi ya tabia za utendaji kazi kwa mazoea, vita ya kimaendeleo; na kwa jumla ni vita ya kuibadili Tanzania kutoka ile iliyoimbwa kwenye maandiko, na kuwa Tanzania ya vitendo vinavyoonekana.
Katika mazingira ya aina hiyo, kuwapongeza viongozi wetu wanapofanya mambo mema, ni jambo la busara; na kuwakosoa pale tunapodhani kunahitajika kukosolewa, ni wajibu wetu halali.
Waziri Mkuu ndani ya mwaka mmoja amefanya kazi kubwa katika maeneo mengi. Hapa ijulikane kuwa huyu ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za kila siku za Serikali. Kama ingekuwa gerezani, basi yeye ndiye mnyapara mkuu!
Wakati akijielekeza kuuanza mwaka wa pili, namuomba sana Waziri Mkuu ajielekeze kwenye mambo mawili ambayo kwangu naona ni muhimu pia.
Mosi, suala la uzazi wa mpango. Idadi ya ongezeko la watu nchini mwetu halipewi msukumo unaostahili. Nakumbuka wakati fulani Rais Magufuli aliwatania watani zake kwa kuwaambia ‘wafyatue watoto’ kwa sababu elimu sasa ni bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne! Wapo waliotambua kwamba ule ulikuwa utani uliolenga kukoleza mazungumzo, lakini wapo wanaoamini kuwa kauli ile ilikuwa ni muhuri wa kuhalalisha uzazi usio na kikomo! Tunashukuru kuwa baadaye mawaziri wanaohusika walitoa ufafanuzi kwa suala hilo wakisema Rais hakumaanisha sasa kuwapo mashindano ya uzazi!
Sitaki kurejea kwenye takwimu, lakini Tanzania ni miongoni mwa nchi tano duniani ambazo kasi yake ya uzazi si ya kawaida. Hili linathibitishwa na idadi ya vijana. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia zaidi ya 60 ya Watanzania ni vijana wanaogota kwenye miaka 35. Kasi hii ya uzazi haiendani kabisa na ukuaji wa uchumi. Hata kama leo uchumi wetu unakua kwa wastani wa asilimia 7.2; kiwango hicho kinaweza kisiwe lolote wala chochote endapo kasi ya uzazi itaendelea kuwa kama hii tunayoshuhudia sasa.
Serikali sasa isione tabu kuwahimiza wananchi kuzingatia uzazi wa mpango. Faida za aina hiyo ya uzazi ni nyingi mno. Utafiti unaonesha kuwa familia yenye idadi ya watoto wanaohimilika kimatunzo, mara nyingine imekuwa na maisha mazuri kuanzia kwenye afya, malazi hadi kimaendeleo. Wazazi wanaozaa kwa mpangilio wana nafasi nzuri ya kuwasomesha na hata kuwalisha watoto wao; kuliko familia zinazoamini kila mtoto anakuja na riziki yake!
Pili, ni suala la mazingira. Nimekuwa mkereketwa mkuu wa masuala ya mazingira na uhifadhi. Ukataji miti kwa ajili ya mkaa umenitoa machozi mara kadhaa.
Nashukuru kuona hivi karibuni Waziri Januari Makamba, ambaye ana dhamana na Mazingira, alifanya ziara katika mikoa na kushuhudia kiama cha uharibifu wa mazingira.
Uharibifu wa mazingira nchini mwetu ni janga kubwa mno. Athari za ukataji miti ovyo zimeanza kuonekana nchini kote. Tumekuwa na majibu mepesi ya kwamba haya ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na viwanda vya mataifa yaliyoendelea. Si kweli hata kidogo! Athari kubwa za kimazingira tunazokabiliana nayo sasa ni matokeo ya ukataji miti ovyo na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Waziri Mkuu afanye ziara katika maeneo mbalimbali nchini ajionee hali ilivyo. Kasi hii ikiachwa, miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa dude jingine la ajabu kabisa!
Kuna taarifa kuwa Waziri Mkuu hivi karibuni anaweza kuwa na ziara katika mikoa kadhaa ya Kaskazini mwa nchi yetu. Namuomba sana, endapo atakwenda mkoani Arusha, asisite hata kidogo kwenda Ngorongoro. Waziri Mkuu nenda ujionee namna Hifadhi ya Ngorongoro inavyokufa! Aende aone namna siasa na wanasiasa zinavyoondoa utajiri huu.
Mtangulizi wake, Mizengo Pinda, alipotangaza kugawa chakula kwa wafugaji, tupo tuliohoji! Hatukusikilizwa. Matokeo yake yakawa makundi kwa makundi ya wafugaji kuhama kwenye vijiji vyao na kuingia Ngorongoro-wakifuata huduma za bure!
Leo watalii wanachofaidi Ngorongoro ni wingi wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda vihongwe na nyumba za bati zinazokinzana na uhifadhi! Aende ajionee. Bahati mbaya Naibu Waziri mwenye dhamana na mifugo ndiye mmoja wa wahamasishaji wa uharibifu huu!
Waziri Mkuu aende Loliondo ajionee namna mapori yanavyokatwa kwa ajili ya kilimo na ujenzi! Loliondo haina wanyama sasa! Shughuli za kibinadamu zimetibua kila kitu. Kuna mashamba ya Wakenya ambao watetezi wao ni NGOs, Wakenya wenzao waliojopachika Utanzania na Wazungu ambao kuishi kwao kunatokana na uimara wa migogoro.
Aende aone namna Wachina walivyoingia Samunge na sasa wanachimba dhahabu wakishirikiana na madiwani wa CCM!
Aende aone kampuni za utalii wa picha zinavyovuna mabilioni bila kulipa chochote serikalini. Aende aone, kwa barabara na kwa anga, namna mifugo ilivyofurika Loliondo, eneo ambalo ndilo mazaria ya wanyamapori, hasa nyumbu!
Waziri Mkuu kama kweli atakuwa na ziara eneo hilo la Kaskazini, asisite kukagua vyanzo vya maji vilivyovamiwa na wananchi na kujengwa maboma, na hivyo kuifanya Loliondo na Serengeti ianze kukauka. Aende Arash, Digodigo, Enduleni, Malambo, Nainokanoka, Oldonyo-Sambu, Orgosorok, Pinyinyi, Soit Sambu, Ololosokwan, Oloipiri,
Enguserosambu na kwingineko aone hali ilivyo. Asikubali kusomewa ripoti pekee. Ahoji mabilioni yanayotolewa na wafadhili, yanawanufaisha nani kama si viongozi wa kisiasa, umma na wenzao wenye NGOs?
Waziri Mkuu asisite kuingia katika Hifadhi ya Taifa Serengeti aone namna mashamba na nyumba vilivyozingira alama za mipaka ya hifadhi! Aende Maswa, Kijereshi akaone mamia kama si maelfu ya nyumbu na swala wanavyouawa na majahili!
Waziri Mkuu apite kando ya barabara kuu zote za nchi yetu – kwa wakati utakaofaa – aone biashara ya mkaa unaotokana na miti ‘isiyo na mwenyewe’. Mkaa unasafirishwa Kenya, Comoro na Uarabuni! Mkaa sasa ndiyo shughuli inayoweza kufanywa na yoyote atakaye – awe raia au mgeni!
Akihitimisha ziara yake atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuamua kama hizi pikipiki na ‘chain saw’ ni mkombozi wa wananchi au ni vifaa vya kuiangamiza nchi.
Narejea kumpongeza Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika muda wa mwaka mmoja. Tatizo ni kuwa mengi mazuri hayaonekani sana kwa kuwa yanamezwa na mabaya yaliyokuwa yametamalaki kila mahali katika nchi yetu.
Utendaji kazi uendelee kwa kasi zaidi. Muda uliobakizwa na Serikali ya Awamu ya Tano ni miaka mitatu tu, yaani 2017, 2018 na 2019. Huu ni muda mfupi, lakini ni mrefu na sahihi wa kuleta mabadiliko kwa viongozi walioamua kuwajibika. Kasi ilivyooneshwa katika mwaka mmoja huu imeleta matumaini. Hongera Waziri Mkuu.