Ukazaji wa hukumu ni hatua inayochukuliwa na mtu aliyeshinda kesi/shauri kwa kuiomba mahakama kumlazimisha mtu aliyeshindwa katika kesi/shauri kufanya au kutekeleza kile ilichoamua dhidi yake/mshindwa.
Kawaida mtu akishindwa kesi/shauri mahakama huwa inatoa maagizo mbalimbali, mathalani agizo la kulipa fedha, agizo la kurudisha nyumba au mali fulani, agizo la kubomoa, agizo la kuondoka katika pango au katika nyumba, kiwanja fulani, agizo la kujenga, agizo la kulipa fidia, faini, gharama n.k.
Maagizo yako ya aina nyingi, inategemea shauri na shauri.
Hivyo basi, ukazaji hukumu/utekelezaji huwa ni kulazimisha agizo au maagizo ya aina tuliyoona hapo juu yaweze kutekelezwa kama ilivyoamriwa.
2. Ni wakati gani hukumu hutakiwa kukazwa?
Kwa ujumla mahakama inapotoa hukumu, yule aliyeshindwa mara moja au ndani ya muda aliopewa kama amepewa hutakiwa kutekeleza kile kilichoamuliwa kwa hiari yake.
Aliyeshindwa akikataa kutekeleza kile kilichoamuliwa kwa hiari yake, basi ni wakati huu ambapo suala la kukaza/kutekeleza hukumu kwa njia ya mahakama huja.
Kwa maana nyingine, mtu aliyeshindwa akiamua kwa hiari yake kufanya yale aliyoagizwa na mahakama basi suala la ukazaji wa hukumu haliwezi kuwepo.
3. Umuhimu wa kuzuia hukumu kukazwa
Sababu za msingi zinazoweza kuzuia hukumu kukazwa ni pamoja na sababu kuwa umekata rufaa, hivyo ukazaji wa hukumu usimame ili rufaa yako isikilizwe kwanza. Sababu nyingine ni iwapo kesi imeendeshwa bila wewe kujua au kuwepo isipokuwa umeshtukia tu watu wanakuja kukaza hukumu.
Sababu nyingine ni iwapo una masilahi katika mali inayokaziwa hukumu, kwa mfano ni mali ya ndoa na hukuwa na taarifa na kilichoendelea, ni mali yako lakini inataka kuuzwa au kutumika kutekeleza hukumu kwa kesi ambayo si yako na pengine hukuwahi kujua uwepo wake, nk.
4. Kuzuia ukazaji wa hukumu
Ukazaji wa hukumu unazuiwa kwa njia ya mhusika kupeleka maombi ya faragha (chamber application) mahakamani.
Mleta maombi/mlalamikaji atakuwa yule anayezuia ukazaji wa hukumu na mjibu maombi/mlalamikiwa atakuwa yule anayekaza hukumu.
Kadhalika ataunganishwa dalali wa mahakama (court broker) aliyeteuliwa kukaza hukumu kama yupo na wengine ambao watakuwa ni muhimu kuunganishwa ili kutekeleza azima.
Maombi ya kuzuia ukazaji wa hukumu yatafunguliwa katika mahakama ambayo imetoa hukumu husika. Pia maombi haya yanaweza kupelekwa chini ya hati ya dharura ikiwa utekelezaji wa hukumu umeshaanza au ikiwa unaona kuwa uchelewaji wowote unaweza kusababisha utekelezaji kufanyika kabla hata maombi yako ya kuzuia hayajasikilizwa hivyo kukusababishia hasara na usumbufu.
Hati ya dharura husaidia maombi kusikilizwa haraka kuliko ilivyo kawaida.
Maombi ya kuzuia ukazaji au utekelezaji wa hukumu yataambatana na kiapo cha muombaji yakieleza sababu za msingi na za kisheria za kwanini hukumu isitekelezwe.
Watu wa aina mbili ndio wanaweza kufungua maombi haya. Kwanza, mhusika kwenye hukumu hasa yule aliyeshindwa. Pili, mtu yeyote mwenye masilahi katika mali inayotaka kutumika kutekeleza hukumu ambaye alikuwa mhusika katika shauri lililokwisha au hakuwa mhusika, pia kuwepo sababu za msingi kuwa si halali mali hiyo kutumika kutekeleza hukumu.
Maombi haya yakishapokelewa mahakamani yatapangiwa hakimu au jaji wa kuyasikiliza. Na baada ya kusikilizwa inaweza kuamuliwa kuwa utekelezaji/ukazaji wa hukumu usitishwe kwa muda kupisha rufaa au vinginevyo au kuwa si halali kutumia mali hii kukazia hukumu, hivyo kuiondoa mali iliyokuwa inatakiwa kutumika kukaza hukumu katika mchakato huo.