Kurasimisha biashara kuna namna nyingi. Kufungua kampuni ni moja ya namna ya kurasimisha biashara. Kusajili jina la biashara nayo ni namna nyingine ya kurasimisha biashara. 

Makala hii itazungumzia kusajili jina la biashara. Na hii ni kwa sababu hii ni njia nyepesi ya haraka na ya gharama ndogo sana. Mfano wa jina la biashara ni kama HK Bazaar, Kinondoni Investment, Congo Traders, Karoli Ltd na mengine yanayofanana na hayo.

 

1. Nini maana ya jina la biashara

Jina la biashara ni lile jina linalotumiwa na mtu kama jina la utambulisho wa biashara yake inayofanywa katika mfumo ambao si kampuni. Kampuni zina majina lakini majina hayo hayawezi kuitwa majina ya biashara bali ni majina ya kampuni.

Jina la biashara ni kwa yule ambaye biashara yake imesajiliwalakini si kampuni. 

Aidha, mwenye biashara ambayo haijasajiliwa lakini analo jina fulani analotumia kisheria, huyo hana jina la biashara. Hilo jina si lake na mtu mwingine anaweza kulisajili naakamtaka huyu ambaye hajalisajili kuacha mara moja kulitumia. 

Ili sheria ikutambue kuwa una jina la biashara ni pale tu unapokuwa umesajili jina hilo. 

 

2. Wapi unaweza kusajili jina la biashara

Jina la biashara husajiliwa kwa Msajili wa Biashara na Makampuni (BRELA). Ukifika hapo  utawaeleza kuwa unataka kusajili jina la biashara na watakupa fomu maalumu utaijaza. Lakini kabla ya hapo utatakiwa utume maombi maalumu hapo hapo Brela. Ukitaka kujua iwapo jina ulilochagua kuwa la biashara yupo mtu mwingine analitumia au la.

Hii ni kwa sababu jina ni moja Tanzania nzima. Hakuwezi kuwa na majina mawili au zaidi yanayofanana huku yote yakiwa yamesajiliwa.

 

3. Ada ya usajili ni kiasi gani

Ada ya usajili wa jina si kubwa. Mara ya mwisho mwaka 2015 ilikuwa Tshs 6,000/- ( Sh elfu sita tu). Kwa hiyo ni rahisi sana na hata kama imepanda bila shaka haiwezi kuzidi 20,000/- (Sh elfu ishirini).

 

4. Kupata namba ya mlipakodi 

Katika kurasimisha biashara kupata namba ya mlipakodi (TIN number) ni hatua ya muhimu sana. Karibu kila ofisi ya TRA pote hata mikoani hutoa namba hizi. Wanazo taratibu ikiwa ni pamoja na kuleta barua kutoka serikali za mitaa kwa anayehitaji kupata namba hiyo. Kwa hiyo ni lazima pia upate namba hii.

 

5. Kupata leseni ya biashara

Ukiwa tayari umesajili jina na umepata nambari ya mlipa kodi, basi hatua inayofuata ni kutafuta leseni ya biashara. Leseni hizi hupatikana manispaa. Kila manispaa ina utaratibu wa kutoa leseni . Viambatanisho utakavyotakiwa kuwa navyo ni pamoja na ushahidi kuwa unayo namba ya mlipakodi.

 

6. Faida za kurasimisha biashara

Moja, ni kuwa unaweza kukopesheka katika taasisi za fedha. Lakini pia hata zile fedha zinazotolewa na Serikali kwenye halmashauri kwa ajili ya wajasiriamali unaweza kuomba na ukapewa. Si rahisi kupata fedha hizi kama hujarasimisha biashara kisheria.

Pili, ni kinga ya biashara zako kwa kuwa unaweza kupata bima ya majanga kama moto n.k pale tu unapokuwa umerasimisha. Si rahisi kupata bima ya biashara ikiwa hujarasimisha.

Tatu, unaondoka katika kufanya biashara kienyeji na kuanza kufanya biashara kisasa na katika mfumo rasmi bila kujali udogo wa biashara zako. Hizi ni baadhi tu lakini faida ni nyingi mno.

 

Kuhususheriazaardhi, mirathi, makampuni, ndoan.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.