Wiki iliyopita katika hali isiyokuwa ya kawaida kwa miaka mingi, Jeshi la Polisi Tanzania limekuwa miongoni mwa taasisi za kitaifa zilizothibitisha kuwa chombo hicho kimewahi kuhusika kubambikia baadhi ya wananchi kesi.
Baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kudai kuwa Jeshi la Polisi kupitia kwa baadhi ya askari wake walimbambikia kesi mmoja wa wafanyabiashara mkoani Tabora, Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake, Ahmed Msangi, nalo lilijitokeza kukiri udhaifu huo.
Mfanyabiashara aliyebambikiwa kesi ni Mussa Sadiki, ambaye kutokana na hali hiyo, aliwahi kuwasilisha malalamiko yake hayo ya kubambikiwa kesi kwa uongozi wa juu wa jeshi hilo. Kimsingi, Jeshi la Polisi limefikia hatua hii baada ya baadhi ya vyombo vya habari nchini kufichua mara kadhaa kuhusu malalamiko ya baadhi ya askari kubambikia kesi raia.
Katika sakata hili, licha ya vyombo vya habari kuzungumzia suala hilo miaka nenda – rudi, kwa namna fulani Rais John Magufuli anastahili pongezi baada ya kusoma moja ya barua iliyochapishwa katika gazeti moja la kila siku nchini, ikieleza malalamiko ya mfanyabiashara huyo wa Tabora na Rais Magufuli kutaka suala hilo lifanyiwe kazi.
Kimsingi, msukumo wa Jeshi la Polisi kukiri udhaifu wake hadharani kupitia kwa msemaji wake, sambamba na Ofisi ya DPP kuweka bayana kuhusu udhaifu huo, ni matokeo ya uingiliaji alioufanya Rais Magufuli, vinginevyo tunaamini kuwa suala hilo lingeweza ‘kuzimika’ ama ‘kuzimwa’ kimya kimya kama ilivyo kwa malalamiko mengine kadhaa yaliyowahi kujitokeza na kuandikwa mara kwa mara na vyombo vya habari nchini.
Kwa upande wetu, kwa kuzingatia unyeti wa suala hili, tunapenda kutoa ushauri katika maeneo matatu. Kwanza, kama itampendeza, Rais Magufuli aunde tume maalumu yenye wataalamu mchanganyiko, wakiwamo majaji na askari bila kujali ni wastaafu ama la, bali wenye weledi na uadilifu wa kutosha kuchunguza malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi kubambikia kesi raia, ambayo ni mengi mno.
Pili, watakaohusika katika kubambikia kesi wananchi wachukuliwe hatua za kinidhamu jeshini na kufikishwa mahakama za kiraia.
Tatu, serikali itafute namna ya kuwafidia waliobambikiwa kesi kama inavyofanya kwa wanaobomolewa makazi yao kupisha ujenzi wa barabara kwa kadiri wanavyostahili. Kimsingi, yakifanyika haya yatarejesha taswira nzuri ya Jeshi la Polisi nchini.