Desemba 6, 2011 kwenye toleo la kwanza la Gazeti JAMHURI, tuliweka bayana msimamo wetu juu ya masuala yanayolihusu Taifa letu.

Miongoni mwa mambo hayo ni kutumia uwezo wetu wote kulilinda na kulitetea Taifa letu bila woga. Amani, utulivu, ulinzi wa Muungano na kulinda rasilimali za Tanzania ni mambo tuliyoapa kuyalinda na kuyaenzi kwa weledi wetu wote.

 

Tuliweka bayana msimamo wetu kwa kuamini kuwa Tanzania ndiyo mama na baba yetu. Tanzania ndipo mahali pekee panapotufaa sisi tunaoishi sasa, na kwa vizazi vijavyo. Imani yetu imekuwa kwamba bila kulinda mihimili hii, tutapoteza tunu na zawadi hii ya nchi nzuri na tajiri tuliyopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

 

Haishangazi kuona kwa muda wote huu tumekuwa miongoni mwa wakereketwa wakuu wa kuhubiri amani, matumizi sahihi ya rasilimali, kupiga vita aina zote za ubaguzi – dini, rangi, ukanda, jinsi, hali – na kadhalika.

 

Ni kwa msimamo huo, mimi binafsi, kama sehemu ya kiapo hicho, nimekuwa miongoni mwa Watanzania tunaopinga hali ya mambo inayoendelea Loliondo. Kwa makusudi, watu wachache, kwa tamaa zao za utajiri, wameamua kuifanya Loliondo kuwa kwenye ramani ya vurugu.

 

Nimeandika makala nyingi, tena zenye utafiti wa kina, nikieleza namna Loliondo inavyoweza kurejea kwenye hali yake ya amani na utulivu. Nimewataja wavurugaji wa Loliondo, lakini nchi imekuwa kama haina mwenyewe! Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

 

Makala ya karibuni kabisa ilikuwa na kichwa cha habari, “Bila kudhibiti NGOs Loliondo haitatulia”. Nilieleza kwa kina namna mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) yanavyotibua amani katika eneo hilo. Nashukuru kwamba kwa kupitia makala hayo, wengi wameweza kutambua siri iliyofichika Loliondo.

 

Huwezi kuzungumzia suala la Loliondo bila kuuhusisha udhaifu wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Katika hili naomba vyombo hivi viniwie radhi, maana siku hizi ukizungumza sana masuala haya unaweza kujikuta katika mazingira hatari, ingawa inawezekana “wabaya” hupitia mwanya huo huo kutekeleza uhalifu wao.

 

Kwenye hotuba ya bajeti za wizara za Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na ile ya Mambo ya Ndani ya Nchi, bila shaka tutasikia tambo za “mipaka yetu ni salama, na hali ya nchi ni tulivu!” Hayo maneno yakikosekana kwenye hotuba hizo, ukiweka na ile ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, nitashangaa! Nitashangaa kwa sababu tumekubaliana, kama Taifa, kulishana maneno ya uongo na faraja alimradi siku zinakwenda!

 

Naandika waraka huu nikiwa na uchungu na vyombo vya ulinzi na usalama, kwa namna vilivyozubaa katika kushughulikia mambo yanayolihusu Taifa letu. Loliondo ni mfano wangu wa leo.

 

Wiki iliyopita, waandishi wa habari wanaojiita wa Kituo cha CNN, waliingia Loliondo kwa mwaliko wa NGOs. Namba zao za mkononi ni +254720734411 na +254712307708. Wakashiriki mkutano ulioitishwa na mawakala hao wanaotaka kuona Loliondo ikiendelea kutopea katika vurugu. Namba hizo ukizitazama vizuri unabaini kuwa ni za Kenya.

 

Wanahabari hawa wameingia kufanya kazi ya kukusanya habari ndani ya nchi isiyo yao, bila vibali kutoka mamlaka halali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tena basi, nasikia hata hawakumtafuta Waziri mwenye dhamana kwa masuala ya maliasili na utalii.

 

Kwa kawaida, mwanahabari yeyote wa kigeni anayeingia nchini kwa shughuli kama hizo, ni lazima apate kibali kutoka Wizara yenye kushughulika na habari. Kwa hapa, mtoa kibali ni Idara ya Habari (MAELEZO). Suala la kuingia kufukunyua mambo ya nchi nyingine linaugusa usalama wa nchi. Kwa hiyo, ni lazima kuwajua wenye nia nzuri, na wenye nia mbaya. Watanzania lazima tuipende nchi yetu kwanza.

 

Wakenya hawa wameingia Loliondo bila kibali kutoka MAELEZO. Hawakupata kibali cha Mkuu wa Mkoa. Hawakuwa na kibali kutoka kwa waziri yeyote. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro (ilipo Loliondo), yupo yupo tu! Huyu eti ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya!

 

Nimepata kwenda Marekani kwa mwaliko wa nchi hiyo. Pamoja na ofa hiyo, bado suala la kibali cha kuendesha shughuli za uandishi ndani ya nchi hiyo lilihitaji viza maalumu (I Visa). Kama Marekani ndiyo wanaojiita mababa wa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari, kwanini waweke utaratibu huo? Kama wao wanauweka kwa masilahi ya nchi yao, seuze Tanzania?

 

Kwa hili la Wakenya, linathibitisha maelezo yangu ya miaka yote kwamba Wakenya wanashiriki sana kwenye mgogoro wa Loliondo. Wana masilahi yao. Wanataka Loliondo ivurugike ili wafaidi wanachokitaka.

 

Mosi, waendelee kupata malisho ya mifugo yao; pili ikiwezekana wawekezaji wakimbilie kwao; tatu ionekane Tanzania haina amani kama tunavyojinasibu duniani kote. Kwa maneno rahisi kabisa ni kwamba kinachoendelea Loliondo ni vita ya uchumi iliyoasisiwa na kusimamiwa vilivyo na Wakenya kadhaa.

 

Ndiyo maana nauliza, polisi wapo wapi? Hadi watu hawa wavuke mpaka, Uhamiaji wanafanya nini? Je, tuna Usalama wa Taifa au Usalama wa Viongozi? Katika hili tukivishutumu vyombo vya ulinzi na usalama tutakuwa tunatenda kosa? Tena basi, hii si mara ya kwanza kwa Wakenya kuingia nchini bila kufuata taratibu. Kwa mara ya kwanza, mwaka juzi wanajeshi wa Kenya waliovalia sare za jeshi la nchi hiyo waliingia Loliondo kwa “Babu”. JWTZ wakakiri kuwa hilo ni kosa. Jiulize, wanajeshi wanaingia katika taifa jingine wakiwa katika sare bila kibali?

 

Haya na mengine ndiyo yanayowafanya wengi waamini kuwa kama ile Vita ya Kagera ingelikuwa leo, Tanzania tungechapwa kama mende ndani ya kabati!

 

Wakati huu tukiwa kwenye mgogoro na Malawi, wengi wetu tunapata mpasuko wa roho kila tunapojiuliza suala la uzalendo na mapenzi yetu kwa nchi yetu. Kwa kudharau au kupuuza kuwashughulikia hawa majasusi, Serikali ijiandae kutumia gharama kubwa kukanusha uongo na uzandiki utakaotangazwa CNN, Al Jazeera na vyombo vingine vya kimataifa. Turejeshe moyo wa kuipenda nchi yetu.