Wakati mwingine Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete mwenyewe anatuanzishia mada zinazotufanya tumjadili. Hatupendi kumwandama Rais wetu, lakini kauli zake zinatufanya tujitose kumkosoa kwa sababu ya kuweka rekodi sawa sawa.
Wiki iliyopita alinukuliwa akitetea uamuzi wa Serikali yake, ambao kimsingi ni uamuzi wake, wa kulifanya deni la Taifa sasa kugota Sh trilioni 40.
Mwezi Juni, mwaka huu, Waziri wa Fedha aliliambia Bunge kwamba deni la Taifa ni dola za Marekani bilioni 19. Dola hizo ukiziweka kwenye shilingi, deni limeshavuka Sh trilioni 40.
Rais Kikwete na washauri wake wa uchumi wanatetea ukubwa wa deni hili. Wanajitahidi kuwaaminisha Watanzania kuwa ukubwa huo si hoja!


Rais anasema fedha nyingi zilizokopwa wakati wa uongozi wake zimetumika kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kulipa madeni ya kale. Akatoa mfano wa mtu mwenye duka anayeogopa kukopa, akisema duka lake haliwezi kustawi.
Mimi si mtaalamu wa masuala ya uchumi. Pamoja na umbumbumbu wangu kwenye uchumi, bado akili ya kawaida inanisukuma niamini kuwa hicho kinachowekwa na mfanyabiashara kwenye duka lake, kinapaswa kuuzwa na faida yake ikaonekana. Lakini pia mfanyabiashara mwenye weledi atahakikisha bidhaa inayohitajika zaidi ndiyo anayoiweka dukani kwake. Ukiona mfanyabiashara anauza leso wakati wa baridi, utakuwa na shaka na umakini wake.


Mfanyabiashara kupata sifa tu ya kukopa benki, akanunua bidhaa ambazo mwisho wa siku zinaishia kuliwa na mapanya yaliyojazana ndani na nje ya duka lake, sidhani kama ni busara.
Siku ya kulipa deni, mwenye benki hataangalia kama mwenye duka kauza au hakuuza bidhaa zilizotokana na mkopo aliompa. Hatahangaika kujua idadi ya mapanya yaliyokula ngano na mali nyingine ndani ya duka. Atakachotaka ni kuona analipwa mkopo na riba yake, basi.
Rais Kikwete anajua mikopo inaishia midomoni mwa mapanya ambao yeye mwaka 2005 akiomba urais aliwaita “mchwa”. Kabla ya kulijadili hili, hebu tuangalie hadhari iliyotolewa mwaka jana na Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD).
Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Hebron Mwakagenda, alipendekeza Serikali kuondoa misamaha ya kodi ili fedha zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ziweze kutumika katika uendeshaji wa Serikali.
Pia akashauri Serikali iwe na utaratibu wa kisheria wa kuomba kibali cha Bunge kila inapotaka kukopa ili sababu za kufanya hivyo ziweze kujulikana na kusimamia utekelezaji wa fedha zinazokopwa.


Baada ya ushauri huo wa TCDD, tujiulize hivi ni kweli ukubwa wa deni la Taifa umetokana na fedha zilizokopwa kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania? Kama jibu ni ndiyo, je, fedha hizo zimetumika ilivyokusudiwa? Nani mwenye ujasiri wa kusema fedha zilizokopwa zimetumika kufanya kile kilichokusudiwa?
Hebu tupitie Ripoti za Kamati za Bunge za PAC na LAAC. Kamati hizo kwa kutumia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2013 zilibaini wizi mkubwa.
Kwa mfano, Rais Kikwete, ambaye aliisoma ripoti hiyo, aliona kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) pekee ilitumia Sh bilioni 10 kwa ajili ya kulipana posho za vikao na masurufu ya safari! Watumbuaji hao walitumia kiasi hicho cha fedha bila kibali cha Hazina.


Fikiria, watu wanakaa, wanapanga utumbuaji wa aina hii, na mwishowe Bandari inapotaka kufanya jambo lolote la maendeleo, fedha zinakopwa kutoka nje. Hatimaye mlipaji ni maskini Mtanzania wa kawaida. Yule gwiji aliyesimamia ulaji huu, tumeambiwa anapangiwa kazi nyingine! Pengine anapangiwa ili aendelee kuliumiza Taifa. Huyu angekuwa China tungekuwa tumeshahau hata lilipo kaburi lake, lakini kwa sababu Serikali yetu ni “sikivu”, yupo!
Rais Kikwete anajua Watanzania walipakodi wanalipa deni la Sh bilioni 80 kwa kampuni ya ndege ya Wallis Inc. ya Hong Kong baada ya Manejimenti ya ATCL mwaka 2007 kutiliana saini kukodi ndege ambayo haikuwahi kufanya kazi. Tayari Serikali ilishalipa Sh bilioni 45.


Waliohusika kwenye ufisadi huu wapo. Wanajulikana, na kama kweli Serikali ilikuwa na nia njema ya kupambana na uharamia huu wa kiuchumi, kitu gani kinamzuia Mheshimiwa Rais kuwaeleza Watanzania namna wahusika walivyofilisiwa. Hatima ya malipo ya deni hili ipo vichwani mwa makabwela wa nchi hii.
Rais Kikwete siku hizi anaona fahari kuwapokea wageni wake kwa sababu pale uwanjani kuna sehemu nzuri imetengenezwa. Ujenzi wa nyumba hiyo ya wageni mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere; Sh bilioni 9 zimetumika nje ya gharama halisi na hakuna maelezo. Walioshiriki mpango huu wanajulikana. Wapo; na hatujasikia wakishughulikiwa. Hatima ya fedha hizo ipo migongoni mwa Watanzania maskini.


Serikali hii hii ambayo kila uchao haiachi kupita huku na kule kusaka mikopo na misaada, hadi mwaka jana ilikuwa imepoteza wastani wa Sh trilioni 1.8 kutokana na misamaha ya kodi. Sijui huu ni uchumi wa aina gani ambao unaisukuma nchi yetu kusamehe kodi kwa kiwango kikubwa namna hiyo, na wakati huo huo ikawa radhi kwenda kupata mikopo; na hata kuomba misaada!
Kwa kuyasema haya simaanishi kuwa mikopo haijasaidia kuleta maendeleo. Imeleta, kwa kiasi chake. Tatizo kubwa la Serikali yetu ni udhaifu katika kuhakikisha fedha zinazokopwa au tunazosaidiwa; mosi, zinatumika kwenye miradi iliyokusudiwa, pili, thamani ya fedha hizo inaonekana; na tatu, mikopo hiyo inaelekezwa kwenye sehemu za uzalishaji.


Mkopo ni mbegu ambayo anayeipata hana budi kuhakikisha anaiotesha kwenye udongo wenye rutuba ili itoe mazao yenye tija kwa mkopaji, na kwa sababu hiyo, iwe chachu ya maendeleo.
Sasa tuangalie matumizi ya fedha hizi za mikopo. Fedha nyingi mno zinakopwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami nchini kote. Hili ni jambo jema, lakini lingekuwa jema zaidi kama Rais Kikwete na wasaidizi wake wangetambua kuwa kimaendeleo huwezi kuanza na barabara. Unaanza na reli ili faida itakayotoka kwenye reli, ijengwe barabara. Unaanza na meli, na kadhalika.
Mabilioni ya shilingi yanaishia kwenye barabara. Ikimalizwa kujengwa barabara moja, hata kabla ya kuzinduliwa, imeshachakaa! Kwanini zinachakaa? Zinachakaa kwa sababu malori ni mengi, yanazidisha uzito na wakati mwingine wasimamizi wa barabara hizi wanashiriki kuchakachua. Upana wa Barabara ya Kimara-Kivukoni ni ushahidi wa uchakachuaji. Ile ni barabara ya bajaji.


Wenye malori wameizidi nguvu Serikali. Hata pale waziri mwenye dhamana alipothubutu kusimamia sheria, Waziri Mkuu aliingilia kati kumzuia. Matokeo yake barabara nyingi zinaharibiwa.
Serikali inasema mapato yake yanayozidi asilimia 80 yanatoka Dar es Salaam. Angalia barabara za Dar es Salaam! Angalia ile inayoitwa barabara ya mabasi yaendayo kasi. Ina tija gani? Benki ya Dunia wametupatia mkopo ambao mwisho wa siku ni maumivu makubwa kwetu. Ile barabara si lolote wala chochote katika kupunguza foleni. Bila fly over Ubungo na kwenye makutano mengine, hii barabara ni kazi bure.
Angalia, miaka zaidi ya 50 ya Uhuru barabara kuu inayohudumia nchi zaidi ya nane ndiyo hii ya Chalinze-Ubungo! Aibu. Serikali haina uamuzi sahihi wa ianze na nini na wapi!


Rais Kikwete ni mchumi. Wengi tuliamini kuwa kwa ujuzi wake angeweka mkazo kwenye ufufuaji na ujenzi wa reli za kisasa. Hilo hakuliona. Amebariki malori. Ndiyo maana wapo wanaosema hawezi kuyazuia kwa sababu biashara hiyo ipo hadi kwa watu walio karibu naye.
Jambo jingine; Serikali chini ya uongozi wa Rais Kikwete imeshindwa kudhibiti matumizi ya Serikali. Juzi tu, mtandao mmoja wa kimataifa umeitaja Tanzania kuwa inaongoza duniani kwa nchi ambazo zina matumizi mabaya ya fedha au mali za umma.
Kulithibitisha hili si kazi ngumu. Keti kando ya barabara yoyote kuu. Angalia SU, SM, STK, STL, DFPA na jamii nyingine ya magari hayo. Fedha za mikopo zinaishia kwenye magari ya kifahari. Ukiyaona barabarani utadhani yanapeleka wageni wa uwindaji wa kitalii maporini. Magari yanayotumiwa na Serikali ya Tanzania na idara zake ni ya thamani kubwa mno. Hapo bado vipuri na mafuta.


Juzi tu, Mheshimiwa Rais alikuwa India. Yale magari aina ya Ambassador hakuyaona? Sambamba na hilo, Rais anajua namna viongozi wa Tanzania wanavyosafiri ughaibuni. Hawatulii. Hapa kuna mawaziri ambao Marekani wanaweza kwenda mara mbili au tatu ndani ya mwezi mmoja. Wanakwenda kwa fedha za umma. Katika ndege wanapanda daraja la kwanza. Hoteli wanamolala ni za hadhi ya nyota tano, wakikosa; na kwa shingo upande hulala za nyota nne! Serikali iko radhi ikope ili kuwawezesha viongozi wasafiri. Wakubwa wanapishana kama mchwa wanaojenga kichuguu. Anayetaka kuyathibitisha haya akubali kupoteza siku yake moja tu pale Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ajionee. Mzigo wote huu unabebwa na walipakodi wa Tanzania.
Rais Kikwete mwenyewe hili la viongozi kusafiri hajawahi kulikemea na naamini ataondoka madarakani bila kulikemea. Hajalikemea kwa sababu yeye mwenyewe amevunja rekodi kwa marais wa Tanzania, na pengine wa Afrika kusafiri ughaibuni. Hizi safari za nje ni mabilioni ya shilingi bila kujali ni za pamba au mikopo kutoka taasisi za kifedha za kimataifa.


Rais ajaye atakuwa na wakati mgumu kulipa deni. Gesi tunayojivuna kuipata itatumika kulipa madeni haya. Ndani ya miaka 10 deni limepanda kwa trilioni zaidi ya 30. Huu ni mzigo mkubwa sana kwa rais ajaye.
Ukiyatafakari haya na mengine mengi ambayo hayakupata nafasi hapa, unaona kabisa kuwa Rais Kikwete utetezi wake kwenye deni la Taifa si mzito.
Amejitahidi kukopa ili kujaza bidhaa ndani ya duka ambalo limejaa mapanya. Matokeo yake, bidhaa zimetafunwa. Lingekuwa jambo la msingi kama angeanza kuwafurusha hayo mapanya. Hakuyafurusha mapanya hata alipoelekezwa na CAG na magazeti mahali walikojificha. Matumizi mabaya ya fedha za umma na ukosefu wa vipaumbele umelifanya deni la Taifa liwe zigo ambalo ni uonevu kuwabebesha walipakodi makabwela wa nchi yetu. Rais ajaye ajue ana kazi kubwa mno.