Wiki iliyopita, nilitaja thumni ya mali na rasilimali zote nilizonazo juu na chini ya ardhi na baharini. Utajiri huo mkubwa unanipa hadhi na heshima ya kukimbiliwa na majirani na marafiki zangu. Si kufuata mali tu, bali pia kufuata maongezi, ucheshi, utulivu na amani niliojaaliwa.
Namshukuru Muumba wangu amenipa mali nyingi katika ardhi yenye tambarare, miinuko, majabali, mapango na mabonde. Hewa safi na majira ya kiangazi na kilimo. Maporomoko ya maji na chemchemi zenye maji baridi na matamu. Vyote hivyo ni vivutio kwa vizazi vyangu, wageni na watalii.
Ijapokuwa majirani na marafiki hunitembelea na kunipa furaha ya moyo, nafsi yangu bado inasononeka kwa sababu baadhi ya tamaduni na tabia zao ni mbaya. Kama vile za kughilibu na kushawishi vizazi vyangu kutenda uchafu, ufisadi na kulazimisha ndoa ya jinsia moja.
Sipendi vitukuu na vilembwe kuhusudu kucheza michezo ya ajabu na hatari na kuvaa nguo nusu mwili. Wenyewe (vizazi) wanaita ‘fasion’  na kwenda na wakati kwa kutumia gia ya utandawazi. Vizazi vimejaa kedi, ukaidi na shari. Wako tayari kuuana na kudhulumiana mali zilizopo.
Ukweli vizazi, majirani na marafiki wananipa sudusi ya raha niitakayo. Hiki ni kiasi kidogo sana. Sehemu kubwa haijapatikana. Wahusika wa kujaza sehemu hiyo ni vizazi vyangu ambao havitambui kupanga na kuchagua, kutenda na kutathmini mambo wakitumia akili kupata mafanikio mazuri.
La kushangaza; viongozi wa vizazi wanakubali kuwa watumwa wa sera na utamaduni wa wale watokao ng’ambo ya mto (marafiki). Nasikia kuna dalali mkuu wao mmoja (vizazi) hataki na anapinga sera, utamaduni na tabia za marafiki za kuhujumu na kudhulumu uchumi, mali na rasilimali zangu.
Lakini wapo wachuuzi na makuwadi wa siasa wanampinga na kumfanyia njama asifanikiwe malengo yake ya kudhibiti mali zangu, kuwafuta wachochole wote katika vizazi hivi na kuweka hali ya maisha iliyosawa kwa wote. Wao wanaona heri kupoteza kuliko kuwa nacho!
Kinachonisikitisha na kunikondesha hata ndugu yangu amekuwa mpiga debe mkubwa, vizazi visipewe hidaya wala misaada, kwa sababu kilembwe wake hakupewa udalali mkuu wa soko na wanasoko wenyewe, kwa maelezo ya kufanyiwa njama na hujuma na vizazi vyenyewe.
Hadi leo nahuzunika na baadhi ya vizazi ama havitaki au havioni umuhimu wa ‘AKILI’  welevu kutoka ng’ambo ya mto wanatumia mbinu ya kughilibu AKILI zao na kuwafanya kuwa maskini wakubwa wa AKILI. Sitashangaa siku zijazo nikawa na wachochole wengi katka vizazi hivi.
Akili ina nafasi kubwa sana katika kuendesha maisha ya binadamu. Akili ni kituo cha uelewa kwa binadamu kufanya shughuli za kila siku. Akili isipotumiwa vyema huwa ni maangamizi na kaburi la binadamu aliye hai. Akili ni nyezo kuu katika kujenga maendeleo mema ya binadamu.
Wapo vitukuu na vilembwe hawatumii AKILI. Wanakubali kuchezewa na kutumika akili zao kwa faida ya wengine. Wamekuwa kama mazuzu walioghilibiwa kwa kupewa vipande vya chupa na kuaminishwa ndiyo almasi na kunyang’anywa almasi halisi –  wakifurahi na kuchekelea.
Marafiki na majirani tangu enzi hadi leo wanatumia vita vya fikra (akili) kutisha, kuhadaa, kujaza kasumba na kucheza na akili za vizazi vyangu. Mimi naita huo ni ‘MPANGO AKILI’ (Mind Programming). Wachuuzi wa siasa wanatumiwa katika nija hiyo na wao wanatumia kutia uzuzu  wanunuzi na walaji wa siasa.
Sema usemavyo, zindua uzinduavyo, wao wanakuangalia na kukubeza. Wanakubali MABAYA na wanakataa MEMA. Ama hakika ni ajabu ya mwezi kuandama mchana. Hivi ndivyo vilivyo vizazi vyangu! Jamani zindukeni mali zinateketea na uhai unapita kama moshi. Haurudi unapotea.
Wazazi wenu walizinduka na kudai Uhuru wenu. Walitumia AKILI kuweka mipango ya maendeleo. Wasaliti wachache (wachuuzi wa siasa) wakavuruga. Leo si shwari. Vitukuu na vilembwe amkeni mrudishe heshima yangu na mlinde na kutunza rasilinali ambao ni  utajiri wetu. Inawezekana.
Chemchemi ya furaha ama nipe tumaini,
Kila mara kwako niwe nikiburudika,
Nakupenda hasa hata nikakufasiri,
Nitalalamika kukuacha Tanzania.